Wakulima Pemba wachekelea mpango wa hati miliki za mashamba ya karafuu

Pemba. Baada ya kuahidiwa kupatiwa hati-miliki za mashamba, wakulima wa karafuu kisiwani Pemba wameeleza matumaini ma-kubwa kuwa hatua hiyo itawaondolea dhu-luma na migogoro inayojitokeza kila msimu wa mavuno.

Kwa muda mrefu, baadhi ya wakulima wamekuwa wakikumbana na changamoto za uvamizi na kudhulumiwa mashamba, licha ya mashamba hayo kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi au kupewa na Serikali bila hati rasmi za umiliki.

Akizindua kampeni kisiwani humo hivi ka-ribuni, mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi, alisema Serikali inakwenda kumaliza changamoto hiyo kwa kutoa hatimiliki za mashamba ya karafuu.

Ratiba ya ugawaji wa hati hizo, iliyopangwa kufanyika Jumamosi, Septemba 26, ilia-hirishwa kutokana na msiba wa Abbas Mwinyi.

Wakizungumza na Mwananchi leo, Jumatatu Septemba 29, 2025, kwa nyakati tofauti, wakulima wa karafuu wamesema hatua hiyo ni ya kihistoria na wanasubiri kwa hamu kubwa kuona ikitekelezwa.

“Tumechoshwa na migogoro ya mara kwa mara ya mashamba haya. Kupatiwa hati ku-taimarisha uchumi wetu kwa kuwa tutaweza kupata mikopo benki na kuvutia wawe-kezaji,” amesema Mohamed Ali Kombo, mkazi wa Kalani.

Wakulima wa karafuu katika kijiji cha Ngomani wakipakia zao hilo kwa ajili ya kuuza Mkoa wa Kusini Pemba. Picha  na Jesse Mikofu



Ameongeza kuwa hatimiliki zitasaidia kupan-ga matumizi bora ya ardhi na kulinda mas-hamba dhidi ya shughuli holela zinazoharibu mazingira, huku akiomba Serikali pia iwa-saidie miche ya mikarafuu ili kuendeleza zao hilo lenye manufaa makubwa kwa taifa.

Naye Juma Ayoub Khamis amesema karafuu ni neema ya Pemba na akapongeza hatua ya Serikali kuliweka zao hilo kuwa la kipaum-bele.

“Kupatiwa hatimiliki kutaondoa udanganyifu, maana wapo wanaoingia mashambani yasiyo yao na hata kughushi nyaraka. Tukipatiwa hati, udhalimu huu utakwisha,” amesema.

Kwa upande wake, Talib Mohammed Bakar wa Shemkani amesema ni vema kwanza kufanyika utafiti ili kubaini wamiliki halali kabla ya kugawa hati hizo, akisema hiyo ita-saidia kuepusha migogoro mipya.

Wakulima wengine, akiwamo Juma Khamis Rajab wa Kibapo Chonga na Ridhia Khamis Mussa wa Ngomeni, wamesisitiza kuwa hati zitapunguza uvamizi wa mashamba na ku-wapa uhakika wa umiliki.

“Kila msimu wa karafuu hukusanyika sura mpya, na mara nyingi ni watu wasio na haki,” amesema Ridhia.

Wakati Ridhia akiyasema hayo, baadhi ya wakulima, akiwamo Maryam Abdalla Khamis, ameiomba Serikali kuongeza bei ya karafuu na kutatua changamoto ya upatikanaji wa umeme, akieleza kuwa wanawake pia wananufaika pakubwa na zao hilo.

Kwa upande wake, Mussa Khamis Muusa kutoka Kaskazini Pemba amesema hatimiliki zitasaidia wakulima kupata mikopo na kuji-patia maendeleo zaidi.

Akizungumzia mpango huo, Katibu wa Itika-di, Uenezi na Mafunzo wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto, amesema chama kimefurahia msimamo wa Dk Mwinyi, kwa sababu hatua hiyo itasaidia kuendeleza zao la karafuu na kulifanya kuwa nguzo thabiti ya uchumi wa Zanzibar.