Moshi. Idadi ya watu waliofariki dunia katika ajali iliyohusisha gari aina ya Noah na lori mkoani Kilimanjaro wakitokea harusini Tanga, imefikia sita baada ya majeruhi wengine kufariki dunia.
Waliofariki dunia katika ajali hiyo ni Rebecca Tarimo, Asia Lyimo, Zainabu Lyimo, Farida Mazimu, Maira Lyimo na Samwel Nyerembe.
Ajali hiyo ilitokea jana Septemba 28, 2025 eneo la Njiapanda Wilaya ya Moshi mkoani hapa baada ya dereva wa gari dogo kushindwa kulimudu kutokana na mwendokasi na kwenda kuligonga lori la mizigo.
Hata hivyo, jana, Septemba 28, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo alisema chanzo chake ni mwendokasi wa dereva wa gari dogo ambaye alishindwa kumudu gari lake na kwenda kuligonga lori.
Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 29, 2025, Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya KCMC, Gabriel Chisseo amesema Septemba 28, 2025 walipokea miili ya watu watano na majeruhi wanne ambapo majeruhi mmoja amefariki dunia leo asubuhi na kufanya idadi ya waliofariki kufikia sita.
“Jana alfajiri tulipokea miili mitano ambayo ilipata ajali na majeruhi wanne akiwemo mtoto wa miezi minane ambaye alikuwa ameumia sana, alipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) lakini baadaye alifariki dunia na kufanya miili kuwa sita,” amesema Chisseo.
Aidha, amesema majeruhi wengine watatu walipatiwa matibabu hospitalini hapo na baada ya afya zao kuimarika wameruhusiwa kwenda nyumbani.
Madereva teksi mjini Moshi, akiwamo Joseph Daud, amesema kifo cha mwenzao Samwel Nyerembe kimewahuzunisha kwa kuwa ni mtu ambaye wameishi naye kwa muda mrefu mjini hapa katika harakati za kutafuta maisha.
“Kwa masikitiko makubwa sana tumepokea taarifa za kifo cha mwenzetu Samwel Nyerembe tulikuwa tukishirikiana naye katika shughuli mbalimbali,” amesema dereva teksi huyo.
Amesema Nyerembe alikuwa ni mtu ambaye wameishi naye vizuri wakishauriana mambo mbalimbali ya maisha.
“Tunaendelea kumuombea kwa sababu sisi wote ni wa kupita katika dunia hii, hivyo nawaomba madereva wenzangu wanaoendesha vyombo vya moto wachukue tahadhari na kuwa makini barabarani maana ni pigo kubwa kwetu na kwa familia,” amesema dereva huyo.
Dereva teksi mwingine mjini Moshi, Yusuf Munga amesema wameishi na Nyerembe tangu mwaka 1995 wakitafuta maisha na walizoeana kwenye mambo mbalimbali.
“Tulipokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa sana kama dereva mwenzetu, tumekuwa tukikaa naye kijiweni kucheza mchezo wa draft, tukishirikiana naye katika mambo mbalimbali,” amesema Munga.
Amesema: “Nyerembe alikuwa ni mcheshi na mwenye utani mwingi, tutamkumbuka sana maana tumejuana naye tangu mwaka 1995 na tumekuwa naye karibu sana.”
Kwa upande wake, mkazi wa Moshi mjini ambaye alikuwa ni rafiki, Rodrick Mmary amesema: “Tumetuhuzunishwa sana na kifo chake kwa kuwa alikuwa ni rafiki yetu na mtani mzuri hasa katika suala zima mpira.”