Mbeya. Zikiwa zimepita siku 13 tangu kuuawa kwa aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu Mzumbe ndaki ya Mbeya, Shyrose Mabula (21), Jeshi la Polisi limewatia mbaroni watuhumiwa watatu wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo, ambao baadaye walifariki dunia wakati wakipelekwa hospitali.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga iliyotolewa leo Septemba 29, 2025, watuhumiwa hao walipigwa risasi baada ya kukaidi amri ya polisi na kuwatishia askari kwa silaha za jadi ikiwamo panga na kisu.
Mabula aliyekuwa mwanafunzi wa Kitivo cha Sheria, aliripotiwa kupotea Septemba 14, 2025 na baba yake, Dk Mabula Mahande kabla ya mwili wake kupatikana Septemba 16, 2025 katika maeneo ya Nane Nane, Kata ya Isyesye, jijini Mbeya akiwa ameuawa na kuchomwa moto.
Kamanda Kuzaga amesema uchunguzi wa awali ulionesha waliotekeleza mauaji hayo walikuwa na lengo la kujipatia fedha kutoka kwa familia ya marehemu kupitia vitendo vya utekaji nyara.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi kwa simu leo, baba mzazi wa marehemu, Dk Mahande amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kutimiza wajibu wao kwa weledi katika uchunguzi wa tukio la kifo cha mwanawe.
Aidha, amesema wananchi wanao wajibu wa kufichua wahalifu katika maeneo yao.
Dk Mahande amelishukuru Jeshi la Polisi kwa ushirikiano lililoutoa kwa familia yake katika kila hatua ya uchunguzi na ameliomba kuongeza nguvu zaidi katika operesheni za kukabiliana na vitendo vya uhalifu nchini.
“Nawapongeza jeshi letu kwa kutimiza majukumu yake. Naomba waongezewe vifaa vya kisasa kwa kuwa wahalifu wanabadilisha mbinu kila siku, wakiwa na vifaa bora vya mawasiliano watafanya kazi yao kwa ufanisi zaidi,” amesema.
Dk Mahede amewaomba wananchi kuwafichua wahalifu kwa kuwa ni watu wanaoishi nao mitaani huku akiwasihi kufanya kazi badala ya kutegemea udanganyifu na njia haramu za kujipata fedha.
Ukamataji ulivyokuwa
Kamanda Kuzaga amesema Septemba 24, 2025, Jeshi la Polisi lilimkamata Marwa John (25), mkazi wa Uzunguni A, aliyekiri kuhusika katika njama hizo na kuwataja wenzake ambao ni Edward Kayuni na Websta Mwantembele.
“Inadaiwa baada ya kumteka (Shyrose), walijaribu kuwasiliana na familia ya marehemu kwa nia ya kupata fedha, lakini iliposhindikana waliamua kumuua ili kuficha ushahidi. Awali, walimnywesha dawa ya kuulia magugu aina ya Round Up na baada ya kushindikana wakamnyonga kwa kamba kisha kumchoma moto,” amedai Kamanda Kuzaga.
Aidha, Mwantembele ambaye ni mlinzi, baada ya kuhojiwa na polisi, naye alikiri kushiriki katika tukio hilo na baadaye kuonesha maeneo walipokuwa wamejificha wenzake wilayani Chunya.
Kamanda Kuzaga amebinisha Septemba 27, 2025 katika Kijiji cha Chalangwa, Chunya, mtuhumiwa Mwantembele aliwapeleka askari kwenye eneo walilopanga kukutana na Edward Kayuni.
Walipofika na kutaka kumkamata mtuhumiwa huyo, alitoa kisu na kutaka kuwajeruhi askari hali iliyosababisha wamfyatue risasi za tahadhari kabla ya kumpiga risasi mguuni.
Wakati huo, mtuhumiwa Mwantembele naye alijaribu kukimbia na kukaidi amri ya polisi licha ya risasi kadhaa kufyatuliwa hewani.
“Baadaye alipigwa risasi mguuni na mgongoni, na wote wawili walikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Chunya na walifariki dunia wakiwa wanapatiwa matibabu,” amesema kamanda huyo.
Amesema Kamanda Kuzaga ameongeza kuwa mtuhumiwa Marwa naye alifariki dunia baada ya kujirusha kutoka kwenye gari la polisi akiwa njiani kuelekeza askari kwa mganga wa jadi aliyedai kuficha baadhi ya vielelezo vilivyotumika kwenye mauaji hayo.
Vitu vilivyokutwa
Katika upekuzi, watuhumiwa walikutwa na pingu mbili, vitambulisho viwili vya bandia vya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), simu zenye picha za uhalifu na ushahidi wa vitendo vya utekaji pamoja na nguo za ndani za marehemu zinazodaiwa zilikuwa zimepelekwa kwa mganga wa jadi kwa ajili ya zindiko.
“Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi kuacha tamaa ya kupata fedha na mali kwa njia za haramu. Uhalifu haulipi na mkono wa sheria utawafikia popote pale walipo,” amesema.