Unguja. Mgombea urais wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohamed amesema chama hicho kikichaguliwa ndani ya mwaka mmoja kitazalisha tani 150,000 za mchele kwa kutumia hekta 5,000.
Hayo ameyasema leo Jumanne Septemba 30, 2025 katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema, ikiwa wakulima wa Zanzibar watapatiwa vifaa na utaalamu wa kuvitumia hakuna sababu ya kushindwa kuzalisha tani hizo na hekta zinatosha kukilisha kisiwa hicho.
“Eendapo chama hichi kitachaguliwa ndani ya mwaka mmoja kitazalisha tani 150,000 za mchele kwa kutumia hekta 5,000, hayo yote tunafanya kwani tunahitaji wananchi wapate chakula,” amesema Hamad.
Amesema, hekta hizo zinatosha kuilisha Zanzibar kwa mwaka mmoja, huku kikiendelea kujipanga zaidi kuondoa njaa kwa wananchi wote kisiwani hapa kwa kutumia fursa ya kilimo.
Mbali na hilo, amesema uvuvi unaweza kuwatoa wananchi wa Makunduchi katika umasikini kwa kuwajengea utaalamu wa namna ya kuvua samaki baharini.
Hata hivyo, amewaomba wananchi kuheshimu mifumo iliyowekwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na wasishawishike kuingia barabarani kufanya vitendo ambavyo vinachochea uvunjifu wa amani, kwani wanasiasa wanazungumza ahadi ambazo hazitekelezeki.
Amesema, hakuna sababu ya kuvunja amani ya nchi kwa maana hiyo atakayekosa akubali kushidwa kwa sababu kila shari na kheri inatoka kwa Mungu.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Bara, Innocent Gabriel amesema siasa ni chakula na chakula ni siasa hivyo chama hicho kuja na mapinduzi ya kilimo kwa kuifanya Zanzibar ya kijani.
“Ili shibe iwe nzuri Makunduchi italima kilimo cha umwagiliaji kwa lengo la kila mwananchi kuongeza kipato,” amesema.
Amesema, eneo hilo ni utalii hivyo chama hicho kitaifaidisha jamii kupitia utalii na kitahakikisha mapato yanayotokana na utalii yanarudi kwa wanakijiji hicho.
Naye, Mwenyekiti wa Wanawake wa chama hicho, Nadhera Haji amesema wamechoka mikopo ya kausha damu na malengo yao hayawezi kutimia kwa madhila wanayokutana nayo.
“Kura yako pekee ndio itawagomboa na mikopo hiyo ili kupata mitaji ya kufanyiabiashara zao na kujiendeleza,” amesema.
Pia, amewataka waandishi wa habari wasitumike kisiasa kwa masilahi ya mtu binafsi badala yake wazitumie kalamu zao kuhamasisha amani kwa wananchi.
Amewataka, wanakijiji hao kubadilisha mazingira kwa kumchagua mwakilishi na mbunge wa chama cha ADC kufanya mageuzi kwa lengo la kuleta maendeleo yanayohitajika.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Mtumwa Faidh Sadick amewasihi vijana kufanya uamuzi mgumu kwa kumchagua mwakilishi wa chama hicho na kutatua changamoto za jimbo hilo.
Naye, Mgombea Uwakilishi wa Makunduchi, Issa Juma Msuri amesema endapo atachagulia kwa kila kijana ambaye anahitaji kuolewa atatoa vijora 30 na ambaye hajaoa atampa Sh500,000 kama mchango wake.