Aina nne za ndege zawania taji la ‘Ndege bora wa mwaka 2026’

Arusha. Aina nne za ndege wanaoishi kwenye nyasi, zimeingia katika kinyang’anyiro cha kuwania taji la ‘Ndege bora wa mwaka 2026.”

Wanaogombea taji hilo ni ndege aina ya Mbuni wa Kawaida (Common Ostrich), Kanga Shingo Nyekundu (Red-necked Spurfowl), Korobustadi (Kori Bustard) na Kibibi Ardhi Kusini (Southern Ground Hornbill).

Ndege hao wanashindana kumrithi kwezi maridadi (Superb Starling) ambaye ndiye anashikilia taji la ndege wa mwaka 2025 na kipindi chake kitamalizika Desemba 2025.

Mashindano hayo yaliyoratibiwa na taasisi ya Nature Tanzania, yanashirikisha Watanzania waliopo ndani ya nchi, wale walioko ughaibuni, pamoja na watalii na wapenda ndege kutoka kila pembe ya dunia.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo jijini Arusha, Ofisa Masoko Mkuu wa Nature Tanzania, Gaudensia Mariki amesema kuwa tayari wanatarajia kura 10,000 kupigwa na mshindi kupatikana.

Amesema kampeni ya “Ndege wa Mwaka” iliyozinduliwa mwaka 2023 wakati Tai Sekreteria aliposhinda kama mshindi wa kwanza, inalenga kuongeza uelewa na kuhamasisha Watanzania kulinda mazingira ya kila siku kabla hayajaharibika.

“Kampeni hii inalenga kuhamasisha Watanzania kulinda mazingira yetu ya kila siku na kuelewa kwamba hata spishi za kawaida ziko hatarini kutoweka zisipotunzwa,” amesema na kuongeza;

“Kwa mwaka huu, tunawahimiza wote kushiriki na kufanya sauti zao zisiwe za kupuuzwa, ama ana kwa ana au mtandaoni,” amesema.

Amesema tayari wanafunzi wa shule ya msingi Manyara Ranch, Shule ya Sekondari Tumaini na Shule ya Sekondari Edward Lowassa wameanza kupiga kura kupitia kampeni ya ana kwa ana waliyofanya katika taasisi hizo.

“Tulifanya kampeni ya kijamii pia katika soko la Makuyuni ambapo wakazi walitambulishwa na kushirikishwa katika shughuli hii la upigaji kura, kama sehemu ya jitihada zetu za kuwafanya watu kuthamini ndege na kulinda mazingira,” amesema Mariki.

Ofisa Mipango wa Nature Tanzania, Edwin Kamugisha amesema upigaji kura ulioanza Septemba 7, 2025, utaendelea kwa muda wa wiki nne hadi Octoba 7, 2025.

“Tunatarajia ifikapo Desemba 2025, ‘Ndege wa Mwaka 2026’ atatangazwa rasmi baada ya kuhesabu kura zaidi ya 10,000 zilizopigwa kupitia mtandao na kwa njia za moja kwa moja,” amesema Kamugisha.

Miongoni mwa wagombea hao, Korobustadi (Kori Bustard) anajitokeza kama balozi mashuhuri wa savanna za Afrika, akichangia pakubwa kwenye ikolojia kwa kudhibiti idadi ya wadudu na kusambaza mbegu.

Mbuni wa Kawaida (Common Ostrich), mwingine wa wagombea, ni kielelezo cha savanna za Tanzania kutokana na mwendo wake mrefu na uwepo wake wa nguvu.

Aidha, akiwa mla majani na wadudu, huchangia kwa kiasi kikubwa katika kudumisha usawa wa mazingira, ingawa anatishiwa na uwindaji haramu na kupotea kwa makazi yake.

Kanga Shingo Nyekundu (Red-necked Spurfowl) huongeza uhai katika nyasi na mashamba kwa kusambaza mbegu na kudhibiti wadudu, lakini anatishiwa na uharibifu wa makazi na uwindaji kupita kiasi.

Kibibi Ardhi Kusini (Southern Ground Hornbill), anayejulikana kwa milio yake mikubwa inayotikisa mandhari, ambapo akiwa ndege wa ardhini mwenye kuzaa taratibu, ana mchango mkubwa katika ikolojia lakini yuko hatarini kutokana na vitisho vya mazingira.

Kwa upande mwingine, kwezi maridadi (superb starling), anayemaliza kipindi chake cha kushikilia taji, akiwa na manyoya yake yenye rangi angavu na tabia za kijamii, ni kielelezo cha kuwa hata aina za kawaida zinakabiliwa na changamoto za uhifadhi.

Mkurugenzi wa Nature Tanzania, Emmanuel Mgimwa amesema wameamua kufanya mashindani hayo yanayoenda sambamba na utoaji elimu wa ndege na sifa zake ili kunusuru kizazi chao.

“Baadhi ya ndege wamekuwa wakiwindwa sana kwa chakula na matumizi mengine lakini baadhi wanapoteza malazi, hivyo kushindwa kuhimili kuendelea kustawi na hii hufanya tishio kubwa la uendelevu wake ndio maana tunafanya hivi kuongea na jamii na kuwatambua ili kupunguza madhara haya kwao,” amesema.