Aliyeshtakiwa kwa kumuua mama yake atiwa hatiani, asubiri amri ya Rais

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dodoma imemkuta Peter Kaguli na hatia ya mauaji ya mama yake mzazi, Helena Lechipya na kuelekeza afungwe kwa amri ya Rais na ashughulikiwe kwa mujibu wa vifungu vya 237(2) na (3) vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo kwa kuzingatia hali ya mshtakiwa ya kuchanganyikiwa katika mwenendo mzima wa shauri hilo, majibu yake yasiyo na mantiki katika utetezi na ushahidi wa shahidi wa tatu wa mashtaka kuhusu historia ya matatizo ya akili ya mshtakiwa.

Peter alishtakiwa kwa mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, kosa alilodaiwa kutenda Juni 17, 2024 katika Kijiji cha Igoji, Wilaya ya Mpapwa mkoani Dodoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Dk Juliana Masabo ametoa hukumu hiyo Septemba 26, 2025 na nakala ya uamuzi huo kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

“Kwa kuzingatia hali ya mshtakiwa ya kuchanganyikiwa katika mwenendo mzima wa shauri hili, majibu yake yasiyo na mantiki katika utetezi wake, na ushahidi wa PW3 kuhusu historia ya matatizo ya akili ya mshtakiwa, ninaamini kuwa hakuwa na uwezo wa kufuatilia mwenendo wa kesi.

“Hivyo basi, anaangukia chini ya kifungu cha 237(1)(b) cha CPA ambacho kinaeleza wazi kuwa iwapo mahakama, baada ya kusikiliza upande wa mashtaka na utetezi, itabaini kuwa mshtakiwa ametenda kosa aliloshtakiwa nalo, basi atahukumiwa kufungwa kwa amri ya Rais.

“Kwa hiyo, namhukumu mshtakiwa Peter afungwe kwa amri ya Rais na ashughulikiwe kwa mujibu wa vifungu vya 237(2) na (3) vya CPA,” amesema.

Kwa mujibu wa kifungu cha 237(1)(b) kinaeleza kuwa: “Iwapo mahakama, baada ya kusikiliza upande wa mashtaka na utetezi, itabaini kwamba mshtakiwa ametenda kosa aliloshtakiwa nalo, lakini akawa hana akili timamu kiasi cha kutoweza kufuatilia mwenendo wa shauri, basi mahakama itamhukumu kufungwa kwa amri ya Rais.

Aidha kifungu cha 237(2), kinaeleza kuwa: “Baada ya mshtakiwa kuhukumiwa kufungwa kwa amri ya Rais, Mahakama italazimika kuwasilisha taarifa ya uamuzi huo kwa Rais, na mshtakiwa atapelekwa gerezani au hospitali ya wagonjwa wa akili au sehemu nyingine atakayopangiwa, hadi pale Rais atakapotoa maelekezo kuhusu namna atakavyoshughulikiwa.

Kifungu cha 237(3) kinaeleza kuwa: “Rais atakuwa na mamlaka ya kutoa maelekezo yoyote anayoona yanafaa kuhusu namna ya kushughulika na mtu huyo (aliyehukumiwa kwa amri yake), ikiwemo kuamuru aachiliwe, aendelee kushikiliwa au apelekwe sehemu nyingine kwa matibabu au uangalizi maalumu.”

Wakati wa usikilizwaji wa hoja za awali, wakili wa utetezi, Joanitha Paul alionyesha kuwa mshtakiwa alikusudia kutegemea utetezi wa wazimu.

Aliomba mshtakiwa kupelekwa katika Taasisi ya Kitaifa ya Akili ya Isanga ili afanyiwe uchunguzi wa kimatibabu ili kubaini hali ya afya yake ya akili wakati wa kutenda kosa aliloshtakiwa ambapo alifanyiwa uchunguzi katika Taasisi ya Taifa ya Akili Mirembe.

Aidha, kumbukumbu za shauri hilo zinazonyesha kuwa ripoti ya uchunguzi huo, iliyotumwa kwa mahakama hiyo inaonyesha kuwa mshtakiwa hakuthibitishwa kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Akili.

Kesi hiyo iliendelea kusikilizwa kwa taratibu za kawaida ambapo usikilizwaji wa awali ulifanyika ambapo mshtakiwa alionekana kuwa hakuweza kufahamu mwenendo wa kesi hiyo.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwakilishwa na mawakili wawili wakiongozwa na Boaz Zephania ambapo uliwasilisha mashahidi watatu.

Kama ilivyokuwa katika hatua ya awali ya usikilizwaji, mshtakiwa alionekana kuchanganyikiwa kabisa na hakuweza kuelewa mwenendo wa kesi kwa njia yoyote ile.

Shahidi wa kwanza,  Dk Hamduni Mohamed, aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, alidai mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha makubwa mawili, moja lilikuwa kwenye paji la uso na lingine kwenye kichwa upande wa nyuma na yalionekana kupigwa na kitu butu na kuhitimisha kuwa chanzo kilikuwa ni jeraha kuwa la ubongo.

Shahidi wa pili ambaye alikuwa mtoto mwenye umri wa miaka 14 (jina lilihifadhiwa), aliyekuwa mjukuu wa marehemu, aliiambia Mahakama kuwa alikuwa akiishi na marehemu (bibi yake) na mshtakiwa akiishi nyumba ya pili.

Alidai kwamba siku ya tukio yeye na bibi yake (marehemu) walienda shambani kuvuna mahindi na baada ya kumalizia walichuma mboga na kuanza kurudi nyumbani walikutana na mshtakiwa, kisha wakaongozana kurudi nyumbani pamoja.

Alidai kwamba alipofika nyumbani bibi yake alianza kuandaa mboga walizotoka nazo shambani ila ghafla mshitakiwa alimsogelea na kuanza kumshambulia kwa fimbo.

Shahidi huyo alieleza ili kujiokoa, bibi huyo (marehemu kwa sasa) alianza kukimbia kuzunguka nguzo ya umeme huku akilia kuomba msaada lakini Peter hakumuachia na kuwa alimfuata huku akimshambulia hadi akaanguka chini ambapo alichukua mchi na kuanza kumpiga nao kwenye paji la uso na kichwani huku akivuja damu nyingi.

Shahidi wa tatu, Juma Kaguli ambaye ni mtoto wa marehemu na mdogo wa mshtakiwa,aliiambai mahakama kuwa wakati huo hakuwepo eneo la tukio kwani alikuwa amekwenda kijiji cha Fufu na akiwa huko kaka yake mwingine (James Kaguli), alimjulisha kwa njia ya simu kuwa mshtakiwa alimuua mama yao.

Alidai kurudi haraka kijijini na kuwataarifu viongozi wa kijiji na kuieleza mahakama kuwa mshitakiwa huyo alikuwa na kifafa kwa muda mrefu na hali yake si shwari kiasi kwamba kuna wakati anakuwa mkorofi, mwenye kupiga watu ovyo na hivyo kulazimu familia kumfunga kamba na kumpeleka hospitali ya Mirembe kwa matibabu.

Alidai kuwa mshtakiwa alikuwa analazwa kwa muda wa wiki mbili hadi tatu kabla ya kuruhusiwa na kuwa mshtakiwa alishawahi kusema kuwa atawaua yeye (Juma) na mama yao kwa vile walikuwa wakimlazimisha kumeza dawa.

Shahidi huyo alipohojiwa kuhusu mshitakiwa alikuwa na hali hiyo kwa muda gani, alijibu kuwa ni muda mrefu kwani alikumbuka kuwa, alipokuwa mtoto, aligundua kuwa kaka yake mkubwa alikuwa na kifafa na baba yao alimpeleka kwa wafanga wa kienyeji ila baada ya baba yao kufariki, hawakumpeleka tena.

Baada ya ushahidi wa mashtaka, mshtakiwa alitakiwa kujibu kesi hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 312(2) cha CPA ambapo jibu lake halikuwa la maana lakini kwa msaada wa wakili wa utetezi, alioneakana kufahamu na kujitetea chini ya kiapo.

Kumbukumbu za shauri hilo zinaonyesha, hata hivyo, utetezi ulipofunguliwa, hakuweza kutoa majibu yenye mantiki kwa maswali aliyoulizwa na wakili wake ambapo alikuwa akisema kila mara kuwa kuna watu wanampiga ngoma kichwani na wanataka kumuua.

Kutokana na hali hiyo, wakili huyo aliomba kuthibitisha kesi yake na akaiomba mahakama hii kushughulikia kesi hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 237 cha CPA.

Jaji Masabo amesema katika kosa la mauaji upande wa mashtaka una wajibu mkubwa wa kuthibitisha bila kuacha shaka kuwa mshitakiwa huyo kwa nia mbaya alisababisha kifo cha marehemu kinyume cha sheria.

Jaji amesema miongoni mwa masuala mahakama inayoyazingatia ni iwapo Helena amefariki,kama kifo chake kilikuwa cha kawaida, iwapo mshtakiwa ndiye alisababisha kifo hicho.

Amesema ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka umethibitisha Helena amefariki dunia, kifo chake hakikuwa cha kawaida kwani kilitokana na jeraha lililosababisha kiwewe kwenye ubongo na kuvuja damu ndani ya fuvu.

Jaji Masabo amesema ushahidi wa mashtaka unamhusisha Peter na mauaji hayo na kuwa ushahidi wa shahidi wa pili aliieleza mahakama kumuona mshtakiwa akimshambulia marehemu kwa fimbo na mchi kichwani hadi kupoteza fahamu huku akivuja damu.

Kuhusu iwapo mauaji hayo yalifanyika kwa nia mbaya au la, Jaji amesema katika kesi hiyo, shahidi wa pili aliieleza mahakama namna tukio lilivyotokea huku shahidi wa tatu akieleza kuwa mshtakiwa aliwahi kusema angemuua yeye na mama yake (marehemu kwa sasa).

Baada ya kupitia ushahidi wa pande zote, Jaji Masabo amesema mshtakiwa alikuwa na nia mbaya ya kukatisha maisha ya mama yake.

Kuhusu utetezi wa mshtakiwa, Jaji Masabo amesema mshtakiwa hakutoa utetezi wa maana kwani alitoa majibu yasiyo na mantiki na wakili wake aliomba lishughulikiwe kwa mujibu wa kifungu cha 237 cha CPA.

“Kwa nguvu ya ushahidi wa upande wa mashtaka na hakuna utetezi wa kuupinga, nimeona mshitakiwa ana hatia na ninamtia hatiani kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu,” amesema Jaji.

Kuhusu adhabu, amesema baada ya kuzingatia hali ya mshtakiwa kuchanganyikiwa wakati wote wa kesi, majibu yake yasiyo na mantiki katika utetezi wake na shahidi wa tatu kueleza kuwa alikuwa na matatizo ya akili.