Arajiga, Mkono kuchezesha Cape Verde v Eswatini

Marefa wanne wa Tanzania wamepangwa kuchezesha mechi inayoweza kuwa ya uamuzi katika mashindano ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 baina ya Cape Verde na Eswatini.

Waamuzi hao ni Ahmed Arajiga, Mohamed Mkono, Hamdani Saidi na Nasir Siyah.

Katika mchezo huo, Arajiga atakuwa refa wa kati huku Mohamed Mkono akiwa mwamuzi msaidizi namba moja na Hamdani Said atakuwa msaidizi namba mbili huku Siyah akiwa refa wa akiba.

Mchezo huo umepangwa kuchezwa Oktoba 13, 2025 katika Uwanja wa Taifa wa Cape Verde kuanzia saa 12 jioni kwa Muda wa Afrika Mashariki.

ARAJI 01


Ahmed Arajiga

Kama Cape Verde haitoibuka na ushindi katika mechi yake dhidi ya Libya, Oktoba 8, 2025, mechi hiyo dhidi ya Eswatini inaweza kuwa ya uamuzi kwao kama watafuzu Kombe la Dunia au la.

Ikiwa itashinda dhidi ya Libya ugenini, Cape Verde itafuzu moja kwa moja kwani itafikisha pointi 22 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu nyingine yoyote kwenye kundi hilo.

ARAJI 04


Hamdani Saidi

Ikitokea imetoka sare au kupoteza dhidi ya Libya, Cape Verde itahitajika kupata ushindi dhidi ya Eswatini ili iende katika Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico mwaka 2026.

ARAJI 02


Nasir Siyah

Ikumbukwe Septemba 16, mwaka huu, Arajiga na Mkono walichezesha mechi ya Watani wa Jadi, Yanga na Simba ambayo ilikuwa ni ya Ngao ya Jamii.

Katika mchezo huo, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Pacome Zouzoua.

ARAJI 03


Mohamed Mkono

Katika msimu wa 2023/2024, Arajiga alishinda tuzo ya Refa Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Mohamed Mkono alishinda tuzo ya Refa Bora Msaidizi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.