DKT. KIMAMBO KUIONGOZA MUHIMBILI KATIKA MABADILIKO MAKUBWA, AAHIDI KUYAFANYA YAWANUFAISHE WANANCHI

:::::::

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Delilah Kimambo, ameeleza kuwa ameingia katika kuongoza hospitali hiyo katika wakati muafaka, kwani amekabidhiwa majukumu yake katika kipindi cha mabadiliko makubwa yanayoendelea nchini, ambayo yamelenga kuboresha hospitali ya MNH pamoja na sekta ya afya kwa ujumla.

Akizungumza katika mahojiano maalum na UTV leo, Septemba 30, 2025, amebainisha kuwa uongozi wake  utaweka mkazo katika maboresho ya huduma, uwekezaji katika mafunzo endelevu ya wataalamu wa afya, upanuzi wa miundombinu, pamoja na kuimarisha mahusiano kati ya wagonjwa na wahudumu wa afya.

 “Nimekabidhiwa jukumu hili katika kipindi cha mabadiliko makubwa, na dhamira yangu ni kuhakikisha mabadiliko haya hayabaki kwenye makaratasi pekee bali yanazaa matokeo chanya. Tunataka kila mwananchi anapofika Muhimbili ajisikie yupo sehemu salama, anahudumiwa kwa heshima na kupata matibabu yenye viwango vya juu.” ameeleza Dkt. Kimambo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kimambo ametumia nafasi hiyo kuishukuru serikali kumuamini kuiongoza MNH na kueleza kuwa uteuzi wake ni sehemu ya muendelezo wa jitihada za kuboresha sekta ya afya nchini.