Doyo aibua kero tano Geita, aahidi kuzitatua ndani ya mwaka mmoja

Dar es Salaam. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, ameibua mambo matano aliyoyataja kuwa kero katika Mkoa wa Geita, ambayo ameahidi kuyashughulia endapo Watanzania watampatia ridhaa kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Katika muendelezo wa kampeni zake mikoa ya Kanda ya Ziwa, leo Septemba 30, 2025, zilizofanyika katika Jimbo la Sengerema, eneo la Stendi ya Zamani na Kata ya Buseresere, Mkoa wa Geita, Doyo amesema kero kubwa katika maeneo hayo ni ubovu wa barabara na gharama kubwa za usafiri.

Ametaja kero nyingine ni ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya, upungufu wa maji safi na salama, na wakulima kushindwa kupata masoko yenye tija kwa mazao yao.

Amesema endapo wananchi wataridhia mikakati iliyomo kwenye ilani ya chama chao na wakamchagua kuongoza nchi, kipaumbele chake ni kuzikomesha changamoto hizo katika mwaka wake wa kwanza madarakani.

Doyo amewaomba wananchi wa Kanda ya Ziwa kutafakari kwa kina juu ya sababu zinazowafanya kuendelea kukosa maendeleo, akigusia namna wakulima wanavyolazimika kuuza mazao yao katika masoko yanayowanyonya.

“Mkinipa ridhaa nitahakikisha wakulima wanapata fursa ya kuuza mazao yao katika masoko yenye tija na faida. Hivi sasa wengi wanalazimishwa kuuza katika masoko yanayowanyonya na kuendeleza umaskini.

“Wananchi, mkiniamini na kunipigia kura Oktoba 29, nitasimamia na kuhakikisha wakulima wanapata bei nzuri na zenye motisha kwenye mazao yenu yote,” amesema Doyo.

Mgombea huyo wa urais amesema haiwezekani wananchi watumie gharama kubwa katika kilimo, halafu Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inawapangia bei. Amesema kuwa hizo ni mbinu za chama hicho kutaka kuendeleza umaskini kwa wananchi, ili waendelee kutawaliwa.

Katika kampeni hizo, Doyo amegusia pia changamoto za miundombinu na huduma za kijamii wilayani Sengerema, akibainisha kuwa licha ya taifa kuwa na rasilimali nyingi kama dhahabu, almasi na Tanzanite, bado wananchi wanaendelea kuishi maisha ya umaskini.

“Nchi hii ina madini ya kila aina, lakini bado wananchi wake hawana maji safi, huduma bora za afya na miundombinu ya barabara. Hili ni jambo la aibu kubwa,” amesema Doyo.

Mgombea huyo pia amezungumzia sekta ya usafirishaji, akieleza kuwa madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji wanalalamikia gharama kubwa za uendeshaji kutokana na ubovu wa barabara.

“Hali hii inasababisha biashara zao kushindwa kuleta faida huku wakidaiwa kodi kubwa bila kuhakikisha uwekezaji kwenye barabara unafanyika ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato.

“Changamoto hizi zimeshindwa kutatuliwa kwa miongo kadhaa, na sasa wanarudi tena kwa wananchi kuomba kura kwa hoja zile zile ambazo hawajawahi kuzitekeleza. Watanzania, ichagueni NLD kwa maendeleo,” amesema.

Awali, akimnadi mgombea urais huyo, Kampeni Meneja wa NLD, Pogora Ibrahim Pogora, amesema Watanzania wanapaswa kumchagua mgombeawa chama hicho kwa kuwa amejipambanua kuwa kiongozi atakayewatetea maslahi yao.

“Ni wakati wa wananchi kumchagua Doyo, kiongozi atakayekwenda kutatua changamoto zenu ambazo kabla ya kuomba ridhaa yenu amezifanyia utafiti,” amesema Pogora.

Amesema ilani ya NLD imezingatia mambo matatu ambayo ni uzalendo, haki na maendeleo, ambavyo mzalendo wa kweli Doyo atavisimamia na kuvitekeleza ipasavyo Watanzania wakimpa ridhaa kwenye uchaguzi.