Ishu ya kocha Simba ipo hivi

KATIKA benchi la ufundi la Simba, hakuna kocha mkuu, hiyo ni baada ya kuondoka kwa Fadlu Davids ambaye tayari ametambulishwa kuinoa Raja Casablanca ya Morocco.

Wakati Fadlu akiondoka huku akiiacha Simba ikipambana kumsaka mbadala wake, timu hiyo tayari imecheza mechi mbili, moja ya Ligi Kuu Bara iliyoongozwa na Kocha Msaidizi, Seleman Matola ambapo imeshinda mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate, kisha sare ya 1-1 dhidi ya Gaborone United kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kufuzu hatua ya pili.

Baada ya Simba kutinga raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 2-1 dhidi ya Gaborone United, lakini hiyo haina maana kama mabosi wa klabu hiyo wameridhika na ishu ya kocha, kwani mchakato unaendelea kwa kasi na sasa imevamia jeshini.

Timu hiyo imecheza mechi ya marudiano dhidi ya Gaborone ikiwa chini ya kocha wa muda, Hemed Suleiman ‘Morocco’ aliyemaliza kazi hiyo na sasa mabosi wa Simba wametuma maombi ya kumuhitaji kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally ili kuongeza nguvu benchi la timu hiyo kama kocha msaidizi.

Simba ilifikia makubaliano ya kuachana na Fadlu Davids aliyekuwa kocha mkuu aliyetimkia Raja Casablanca ya Morocco, kisha kumkaimisha Morocco ili aiongoze katika mechi hiyo ya CAF ambapo ilishuhudiwa ikiisha kwa sare ya 1-1, lakini ushindi wa 1-0 ugenini wiki iliyopita uliwabeba.

KOCH 01


Hata hivyo, licha ya kumpa kazi Morocco, lakini mabosi wa klabu hiyo walikuwa bado wapo katika harakati za kutafuta kocha mkuu mpya na chanzo cha kuaminika kutoka Msimbazi kinasema tayari wamepiga hodi JKT kutaka kumchomoa Ahmad ili akaongeze nguvu katika benchi la ufundi la timu hiyo.

Ahmad aliyewahi kuiongoza timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars na kuinoa Tanzania Prisons, msimu uliopita aliiwezesha JKT kumaliza nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, huku akiifanya timu hiyo kuwa ngumu kufungika uwanja wa nyumbani ambapo ilipoteza mechi mbili pekee kati ya 15, ikishinda tano na sare tatu. Kwa jumla, timu hiyo ilipoteza mechi 10, ikishinda nane, sare zikiwa 12.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeiambia Mwanaspoti, klabu hiyo imefanya mazungumzo na kocha Ahmad ili kumuongeza katika benchi la ufundi kama kocha msaidizi kusaidiana na Seleman Matola aliyepo kwa sasa.

KOCH 02


“Simba tayari imempa ofa rasmi kocha huyo na mchakato unaendelea, mambo yakienda kama walivyopanga, atajiunga na timu haraka na kukaa benchi katika mechi ya ligi dhidi ya Namungo.

“Kuhusu suala la kocha mkuu mpya pia ni suala la muda tu, tunaendelea kupambana kutafuta na kuna maombi mengi tumeyapokea kutoka kwa makocha wenye CV kubwa muda ukifika wanasimba watamfahamu kocha,” kimesema chanzo hicho.

Mtoa taarifa huyo amesema mchakato wa kumtafuta Ahmad umekuja baada ya makubaliano na kocha Morocco kukamilika na wanaamini mpango ukienda sawa kocha huyo atakuwa sehemu ya benchi lao msimu huu.

Mwanaspoti imefanya jitihada za kumtafuta Mtendaji Mkuu wa JKT Tanzania, Meja Stan Chale, ambapo alipoulizwa juu ya kufuatwa na Simba, amesema hata wao wameziona taarifa hizo lakini hakuna maombi yoyote waliyoyapokea kutoka Simba, hivyo bado Ahmad ni kocha wa timu hiyo.

KOCH 03


“Hakuna taarifa yoyote tuliyoipokea kutoka Simba au kwa kocha kama kuna ofa kutoka Simba na sisi tunazisikia na kuziona taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii.

“Hivyo hizo ni taarifa za mitandaoni tu Ahmed ni kocha wa JKT Tanzania na anaendelea na maandalizi kwa ajili ya kuiandaa timu ili iweze kufikia malengo tuliyo yakusudia msimu huu,” amesema Meja Chale.

Msimu uliopita chini ya Fadlu, Simba ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza kwa jumla ya mabao 3-1 mbele ya RS Berkane ya Morocco. Pia kocha huyo akaiwezesha Simba kumaliza nafasi ya pili ya Ligi Kuu Bara.

Jumatano Oktoba Mosi, 2025, Simba itashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuikaribisha Namungo, ikiwa ni mechi ya pili ya Ligi Kuu Bara msimu huu kwa timu hiyo baada ya awali kuinyoosha Fountain Gate kwa mabao 3-0.