Dar es Salaam. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Viwanda na Biashara, zimewasisitiza wakulima kufuata kanuni sahihi za kilimo zilipozungumzia kuhusu taarifa za uwepo wa nyanya sokoni zenye mabaki ya viuatilifu.
Septemba 29, 2025 Mwananchi liliripoti uwapo wa nyanya zenye mabaki ya viuatilifu sokoni, huku wakulima na wafanyabishara wakisema uwepo wake husaidia isipondeke, kuharibika na kukaa kwa muda mrefu.
Kwa upande wao, wataalamu wa afya walieleza mabaki hayo ni hatari kwa afya ya binadamu.
Kwa nyakati tofauti Septemba 29 na 30, viongozi wa wizara hizo na watumishi wa taasisi na mamlaka zingine za udhibiti wa ubora wamezungumzia suala hilo na kutoa ufafanuzi.
Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah, amewahakikishia Watanzania kuwa katika soko la Tanzania hakuna bidhaa yenye madhara kwa matumizi ya binadamu na kwamba, vyombo vya ubora vinazingatia kila kitu.
“Soko la Tanzania ni salama kwa matumizi. Kwa wakulima kuna matumizi ya dawa ambayo yana maelekezo baada ya kuwekwa kuna siku za kuhesabu ni lini dawa inawekwa kwenye mmea na mpaka inafika sokoni inafuatiliwa,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk Ashura Katunzi, amesema shirika hilo lina jukumu la kufanya ufuatiliaji wa bidhaa za chakula ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya ubora na usalama.
“TBS hufanya ufuatiliaji wa mabaki ya viuatilifu kama njia mojawapo ya kuhakikisha usalama na ubora wa bidhaa husika. Ufuatiliaji wa mwisho katika soko ulifanyika mwaka 2023/2024 ambao ulionyesha hakuna mabaki ya viuatilifu ambayo yapo juu ya kiasi vumilivu (kwa mujibu wa viwango vya WHO/FAO, Maximum Tolerable limits),” amesema.
Wataalamu wa kilimo wamesema changamoto hiyo wamekuwa wakikumbana nayo na nyakati zote hutoa elimu kwa wakulima kuhusu madhara ya kuchuma nyanya kabla muda wa uangalizi haujaisha baada ya kuwekwa dawa.
Gungu Mibavu, Mkurugenzi wa masoko na usalama wa chakula, Wizara ya Kilimo, amesema ufuatiliaji umekuwa ukifanyika kwa mnyororo kuanzia shambani mpaka sokoni.
Amesema nyanya inapokuwa shambani wizara ina taasisi ya Mamlaka ya Afya ya Mimea ambayo hufuatilia iwapo kuna mabaki ya viuatilifu kwenye mimea, wakishathibitisha hutoa cheti cha kupeleka bidhaa nje ya nchi.
“Tumekuwa tukitoa elimu kwa wakulima kupitia maadhimisho ya Nanenane, tunawaambia madhara ya viuatilifu hata kwa wao wenyewe, ukipuliza upepo ukakurudia unaipata athari, elimu inatolewa na kwa maofisa ugani pia,” amesema na kuongeza:
“Inawezekana hilo likawa limetokea shambani, baada ya kuvunwa ama wakati wa kuisafirisha au sokoni kwenyewe. Taasisi ya TBS iliyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara pia tunashirikiana nao kuchunguza bidhaa ikishafika sokoni.”
Amesema lazima taasisi hizo mbili na wizara zione namna ya kushughulikia changamoto hiyo.
“Tunafuatilia kila siku si kwamba tumesikia leo, tumekuwa tukichukua hatua mara kwa mara na huwa tunazimwaga na kuziteketeza. Tunalipokea (taarifa) na kulifanyia kazi kujua kitu gani kimetokea na namna gani tutalishughulikia,” amesema.
Mtembei Kamwesige, Mkurugenzi wa operesheni na udhibiti ubora wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), amesema suala hilo wamekuwa wakilishughulikia na kuchukua hatua.
Amesema changamoto iliyopo si kwa viuatilifu pekee, hata mbolea zina muda kulingana na mazao.
Mtembei amesema kwenye nyanya dawa mbalimbali zina muda wake wa kupulizwa, hasa mwishoni ili kuharakisha nyanya kuiva. Ameeleza homoni hazina athari kwa mlaji na hazina sumu kwa kuwa si dawa za kuua wadudu bali huharakisha uivaji.
“Tunalifahamu hili na huwa tunawakagua kabla hawajavuna,” amesema.
Ameeleza wengine wana dawa za kuhakikisha wanaharakisha mifumo ya kibaolojia itokee haraka, nyanya iwahi kuiva na kukaa muda mrefu sokoni.
“Kwa dawa hii nyanya haibunguliwi au kutobolewa, lakini kumekuwa na matumizi yasiyofaa, tumekuwa tunafuatilia sokoni, kama nyanya bado ina dawa na imefika tunachukua hatua,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kilimo Tanzania (TARI), Dk Thomas Bwana, amesema changamoto hiyo imekuwa inaonekana na huwashauri wakulima.
“Kinachotokea wote tunawashauri iwe wakulima wa mbogamboga au wengine, tunawaambia ukipiga mchicha wako dawa, ukipiga mbogamboga yoyote usiuze mpaka siku saba au zaidi lakini changamoto wengine si waaminifu,” amesema.
Bwana amesema nyakati zingine wamekuwa wakikuta sampuli katika mazao na wamekuwa wakichukua hatua.
“Tunawaambia jamani kufanya hivi unahatarisha afya ya mtu mwingine, unaweza kufika sokoni unaona kuna dalili za kopa na dawa zingine,” amesema na kuongeza:
“Wengine unakuta ile kopa imekaa muda wake umepita lakini haina madhara ila haiwezi kutoka pale bila kuoshwa au kama wanavyofanya wengine kuvuna kabla, inatakiwa ukivuna nyanya uoshe ndipo uipeleke sokoni sasa sisi unasema ukiosha itaoza, tukitoa tunajaza kwenye matenga, zipelekwe sokoni iko hivyo,” amesema.
Amesema walichobaini baadhi ya wakulima hupiga dawa, nyanya ikiwa tayari lakini mteja hajafika akiona itaharibika anapiga tena. Wakati muda haujaisha mteja anafika anamuuzia vivyo hivyo.
“Tunawashauri wawe wamepiga dawa na wakae mpaka iishe ndipo inakuwa haina madhara kwa binadamu, mara nyingi wanapiga dawa za ukungu, kopa na nyinginezo. Katika hizo siku saba mpaka nane ukiosha inatoka, kinachotokea ni presha ya wanunuzi,” amesema.
Bwana amesema nyanya zenye madoa madoa wamekua wakiziona sokoni na wakiuliza zaidi huambiwa zilivunwa kabla ya muda wake.
Hata hivyo, amesisitiza kwamba katika mnyororo wa ugavi mkulima hana mawasiliano ya moja kwa moja na mfanyabiashara bali huwasiliana na wachuuzi na madalali.