ACHANA na ushindi wa kwanza walioupata Tanzania Prisons, kocha mkuu wa timu hiyo, Zedekiah Otieno amesema anahitaji kuona mastraika wa timu hiyo wanaonyesha makali na ametoa muda wa siku saba kwa mastaa hao kabla ya kurudi kambini kujiandaa na mechi zijazo za Ligi Kuu Bara.
Prisons ilianza vibaya Ligi Kuu msimu huu baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Coastal Union na Namungo zote ikipasuka kwa bao 1-0 ugenini kabla ya juzi kuzinduka nyumbani na kuifunga KMC pia kwa bao 1-0, lakini kocha Otieno amelia na washambuliaji.
Huo ulikuwa ushindi wa kwanza kwa kocha huyo raia wa Kenya, ikicheza ligi kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini hapa, matokeo ambayo yalionekana kuwakuna mashabiki, benchi la ufundi na menejimenti.
Ligi inachezwa kesho Jumatano kwa mechi mbili kabla ya Ligi kusimama kupisha kalenda ya michuano ya kimataifa, ambapo Prisons inatarajia kurudi uwanjani Oktoba 21 kuvaana na Mbeya City katika Dabi ya Mbeya itakayopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine.
Akizungumza na Mwanaspoti, Otieno ambaye ni mara ya kwanza kufanya kazi nchini, amesema baada ya mechi hiyo, wachezaji watapumzika hadi Oktoba 5, ikiwa ni kuwapa nafasi kujitafakari na wenye majeraha kukaa sawa.

Amesema wakati wakirejea kambini, anahitaji kuwekeza nguvu zaidi kwenye eneo la ushambuliaji kuhakikisha wanaondoka kwenye idadi ndogo ya mabao na kuongeza makali zaidi, huku akiwapongeza kwa kazi nzuri.
“Kumbuka tulitoka kupoteza mechi mbili mfululizo kwa maana ya kuruhusu mabao, lakini mchezo na KMC, hatukufungwa bao ina maana wachezaji walisahihisha makosa, japokuwa kuna kupungua umakini kwa mastraika kwani tungeweza kufunga zaidi ya bao moja,” amesema Otieno na kuongeza;
“Nimetoa mapumziko hadi Oktoba 5 ambapo tukirejea mazoezini nahitaji kuona mastraika wakifunga sana mabao, badala ya kuishia bao moja licha ya kwamba hesabu zetu ni pointi tatu kila mchezo.”
Kocha huyo aliongeza, wakati akiwasukia mipango kwa mastraika, kazi haitaishia hapo badala yake timu itasukwa pia kujilinda vyema.