Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameziagiza wizara saba kuhakikisha kila mojawapo inakamilisha majukumu yake katika kushughulikia afua za lishe ili kuondokana na changamoto zilizopo eneo hilo.
Majaliwa ametoa maagizo hayo baada ya kuzindua ripoti ya utafiti uliofanyika nchini ukiangazia ‘Gharama za Utapiamlo Katika Pato la Taifa’.
Ripoti hiyo imeangazia gharama za utapiamlo katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Katika maagizo yake ameiagiza Wizara ya Fedha kuboresha ufuatiliaji wa rasilimali za lishe ili kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya afua za lishe zinafanya kazi iliyokusudiwa.
Amesema hayo leo Jumanne, Septemba 30, 2025 kwenye Mkutano Mkuu wa 11 wa wadau wa lishe jukwaa lililojadili hatua zilizofikiwa, changamoto zilizopo na namna bora ya kuimarisha jitihada za pamoja katika kupambana na utapiamlo na kukuza afya za Watanzania.
Pia, ameiagiza Tamisemi kusambaza maofisa lishe kote nchini ili kuzifikia kaya zote.
“Hakikisheni watendaji wanaofanya kazi hii waweze kuwa na usafiri wa kufika pembezoni na kuifikia jamii yote mpaka vijijini, pia hakikisheni wanapata chakula na mahitaji muhimu wawapo kazini,” amesema.
Majaliwa amezitaka wizara zinazosimania uongezwaji wa virurubishi katika chakula zihakikishe zinasimamia hilo na kuzitaka taasisi za utafiti na vyuo vya elimu kuendeleza tafiti na kuhakikisha majibu ya ripoti yanatumika kwa jamii ili kutatua changamoto zilizopo.

“Wizara zinazohusika zitenge rasilimali za kutosha katika afya za lishe. Tamisemi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Mendeleo ya Jamii endelezeni programu za lishe shuleni, Wizara ya Afya endeleeni kutilia mkazo mkazo lishe bora na salama katika jamii.
“Imarisheni mifumo ya kidijitali ya ukusanyaji na ufuatiliaji wa taarifa za lishe ili mifumo iwe rahisi kwa wadau wote, kuna gharama kubwa za utapiamlo katika pato la Taifa,” amesema.
Ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na taasisi za udhibiti ziimarishe ukaguzi na utekelezaji wa sheria ili kuhakikisha uongezaji wa virutubishi na upatikanaji wa vyakula salama.
Majaliwa amewataka wadau kushirikiana na Serikali katika kuimarisha hali ya lishe nchini ili kupunguza kasi ya magonjwa yasiyoambukiza.
Amesema licha ya juhudi kubwa zilizopigwa bado nchi inakabiliana na utapiamlo, udumavu pamoja na tatizo la unene uliopitiliza alilolitaja kukithiri kwa watu wazima.
Amesema watu wazima wengi hawafanyi mazoezi, wengi wanakula chakula kingi hawafanyi mazoezi, kila mahali anakwenda kwa gari, unakunywa supu nzito unarudi kukaa;
“Tusipuuze changamoto zilizosalia bali tupambane. Lishe ni sekta mtambuka inayotakiwa kusimamiwa na wadau wote utaratibu huu unatufundisha kuwa tukishirikiana kwa dhati tutaweza kusonga mbele.
“Uwekezaji katika lishe hakuna mipango utakayotimia bila uwekezaji katika rasilimali, kila wizara iwekeze kwenye bajeti ya kila mwaka,” ameagiza.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete amesema mwaka huu wamekamilisha utafiti na kutoa ripoti ya Gharama za Utapiamlo Katika Pato la Taifa.
“Tumefanikisha zoezi la kukamilisha utafiti wa Ripoti ya gharama za utapiamlo katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, utafiti huu utatumika katika kuona maeneo yapi Yana changamoto na namna tunavyoweza kuyafanyia kazi,” amesema.
Amesema Serikali inaendelea kuhakikisha wadau wa sekta zote wanashiriki na Wizara zote zinaingiza mipango ya lishe katika bajeti zao kila mwaka.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk Jim Yonazi amesema wadau na wataalamu 320 kutoka sekta ya umma na binafsi pamoja na wadau wa lishe Kimataifa wamekutana katika dhima tatu za lishe katika nyanja kuu za ubunifu na upatikanaji wa fedha, kitita muhimu cha lishe na mifumo ya uwajibikaji.
Ametaja baadhi ya maazimio waliyofikiwa katika kikao cha siku mbili kuwa ni pamoja na Serikali kwa kushirikiana na wadau kukusanya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe, kujenga uelewa wa lishe kwa sekta binafsi ili kuimarisha mnyororo wa chakula na vinywaji nchini.
Pia, amesema wamekubaliana kuhamasisha ushiriki wa jamii na familia katika kuhakikisha lishe inazingatiwa na kupambana na utapiamlo.
Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan amesema Ireland imekuwa ikisaidiana na Tanzania kwa kipindi kirefu katika sekta ya lishe, njaa na utapiamlo kwa watoto na kwamba nchi hiyo itaendelea kushiriki katika mapambano hayo.
“Tanzania imefanikiwa kufikia hatua nzuri katika mapambano ya utapiamlo, hivyo nasisitiza kuwekeza katika lishe katika eneo lolote ni mwanzo mzuri wa nchi husika kuondoka katika umasikini, na kuwa na Taifa lenye nguvu, kuokoa maisha, na kuondokana na udumavu kwa watoto,” amesema
Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Elke Wisch amesema suala la lishe si kazi ya sekta moja bali inaingia katika sekta nyingi na tunatakiwa kushirikiana ili kufikia malengo kwani kila mtoto ana haki ya kukua na kuwa na afya njema.
Amesema watoto walioathirika na udumavu pia wanaathirika katika ukuaji wao wa uelewa, kielimu na kuchanganua mambo hivyo ni muhimu kwa mtu mmoja mmoja, jamii, sekta zote kushirikiana kufikia malengo.

“Tumekuwa tukifanya kazi bega kwa bega na Serikali pamoja na wadau wote kuhakikisha kila mtoto anaweza kukua na kuwa mwanajamii atakayechangia maendeleo ya nchi na dunia,” amesema.
Awali akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Warda Obathan amesema lishe ni jambo la muhimu bila kuwa na lishe bora jamii haiwezi kuwa na afya na tija katika ujenzi wa Taifa.