Matola afichua ugumu wa kuikabili Namungo

LICHA ya Simba kutopoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara mbele ya Namungo, lakini Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema hawatarajii kuwa na mechi nyepesi kutokana na aina ya timu wanayokwenda kukutana nayo ikiwa na kocha Juma Mgunda anayeifahamu Simba.

Matola ambaye amekabidhiwa jukumu la kukiongoza kikosi cha Simba baada ya kuondoka kwa Fadlu Davids, amesema Namungo imekuwa ikiwapa wakati mgumu kwenye mechi za hivi karibuni licha ya kwamba mbili za mwisho walishinda.

“Tunatarajia kuwa na mechi ngumu, kama mkiangalia rekodi, Namungo wamekuwa wakitusumbua licha ya kuwafunga mechi mbili za mwisho,” amesema Matola.

Kuhusu kukutana na Namungo inayofundishwa na Juma Mgunda aliyewahi kuinoa Simba huku Matola akiwa msaidizi wake, amesema: “Wana kocha mzuri anayeijua Simba, tutaingia na tahadhari kubwa.”

Simba itakuwa mwenyeji wa Namungo katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kesho Oktoba 1, 2025 saa 2:30 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Rekodi zinaonyesha Simba katika mechi 12 za Ligi Kuu Bara ilizocheza dhidi ya Namungo, imeshinda saba na sare tano, haijapoteza, lakini hilo haliipi uhakika Simba kushinda hapo kesho.

Wasiwasi unakuja kufuatia Simba kuwa na uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi lakini inashindwa kuzitumia ipasavyo ingawa Matola amesema wamelifanyia kazi.

“Tunalijua hilo kwani tumekuwa tukitengeneza nafasi nyingi shida imekuwa kuzimalizia, tumelifanyia kazi kwa kiwango kikubwa,” amesema Matola.

Kabla ya mechi mbili za mwisho msimu uliopita Simba kuichapa Namungo nyumbani na ugenini tena bila ya kuruhusu bao, timu hizo zilitoka sare tatu mfululizo.

Msimu huu, Simba imeanza ligi na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate ambapo Matola ndiye aliiongoza timu hiyo, huku Namungo ikiwa tayari imeshuka dimbani mara mbili, ikitoka sare 1-1 dhidi ya Pamba Jiji na kushinda 1-0 mbele ya Tanzania Prisons.