::::::::::::::
Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya huduma za kifedha kwa njia ya simu, MIXX, imeingia makubaliano ya ushirikiano na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) pamoja na kampuni ya Yas Business, kwa lengo la kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Makubaliano hayo yanalenga kuwaunganisha wafanyabiashara, wakulima, wanawake na vijana katika mfumo wa uchumi wa kisasa unaotegemea teknolojia, ili kurahisisha malipo na kukuza ushiriki wa watu wengi zaidi katika uchumi wa kidijitali.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa MIXX, Bi. Angelica Pesha alisema kuwa ushirikiano huo utasaidia kufanikisha dira ya maendeleo ya Taifa ifikapo mwaka 2050 kwa kutoa huduma za kifedha zinazopatikana kwa urahisi, salama na kwa uwazi zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA, Bw. Oscar Kissanga alieleza kuwa makubaliano haya ni fursa kwa wanachama wa chemba hiyo, hasa walioko vijijini na maeneo ya pembezoni, kupata huduma bora za kifedha na mawasiliano ya uhakika.
Ushirikiano huo umejikita kwenye maeneo matatu makuu: kuimarisha mifumo ya malipo ya kidijitali, kutoa huduma bora za mawasiliano kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, pamoja na kutoa elimu ya kifedha kwa vijana na wanawake nchini.
Kupitia kampuni ya Yas Business, wanachama wa TCCIA wanatarajiwa kunufaika na huduma za kisasa za intaneti, zitakazowezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati na kuongeza ufanisi wa biashara zao.
Zaidi ya hapo, ushirikiano huu unalenga kuwajengea uwezo vijana na wanawake kupitia elimu ya kidijitali na masuala ya kifedha, ili waweze kushiriki kikamilifu katika fursa zinazotolewa na uchumi wa kisasa.
MIXX na washirika wake wamesema kuwa hii ni hatua ya kujenga misingi ya uchumi jumuishi, unaotoa nafasi sawa kwa makundi yote ya jamii kushiriki katika maendeleo ya Taifa.
PICHA NA JAMES SALVATORY – TORCH MEDIA
Mwisho.