CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kutoka Shirika la Global Health Labs (GHL) la nchini Marekani Vifaa tiba vinavyotumia Akili Unde (AI) vyenye thamani ya Dola za Marekani 16,000 sawa na Sh milioni 40.
Vifaa hivyo ambavyo ni kompyuta tatu zenye uwezo mkubwa wa kutumia akili unde, vimepokelewa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kutoka Shirika la Global Health Labs (GHL) la nchini Marekani linaloshirikiana na Shirika la Bill and Melinda Gates.
Akizungumza leo Septemba30,2025 Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema MUHAS ina kompyuta tisa ambazo zina uwezo mdogo na zimewezesha kugundua magonjwa ya saratani ya matiti, shingo ya kizazi na magonjwa ya moyo hivyo kuongezewa kwa vifaa hivyo, kutaongeza ubora wa huduma.
Amesema vifaa hivyo vinatarajiwa kuongeza ubora katika uchunguzi wa magonjwa, ugunduzi wa mapema na kuwapunguzia wagonjwa gharama za kusafiri kufuata tiba kwenye hospitali kubwa.
Amesema kupitia watafiti na wagunduzi wao, waliandika andiko na kulituma kwa wadau mbalimbali duniani wakiomba kompyuta moja itakayowawezesha kugundua magonjwa hayo kwa haraka ili kuwapunguzia adha wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali nchini ambao wamekuwa wakichelewa kupata tiba ya saratani.
“GHL walipenda andiko letu na kutuletea kompyuta tatu badala ya moja tuliyoomba, vifaa hivi vina vyenye uwezo mkubwa kuliko tulivyokuwa navyo, hii itasaidia kuongeza uchukuaji wa sampuli za saratani na magonjwa ya moyo,” amesema Profesa Kamuhabwa.
Ameongeza wanatumia akili unde kutafuta taarifa, kuchakata na kueleza namna bora ya kutibu na kwamba chuo hicho hakiwezi kukwepa matumizi ya teknolojia hiyo kwa kuwa wanatafiti, wanafundisha na kutoa huduma za afya.
“Vifaa hivi vitaboresha mazingira ya kufundishia, kutafiti na kuboresha maisha ya Watanzania kwani tunakusanya taarifa za wagonjwa kutoka vituo mbalimbali vya afya na badala ya daktari kuchakata mwenyewe kujua ugonjwa husika, sampli zitaingizwa kwenye mashine na kugundua aina ya tatizo na matibabu yake,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Vifaa tiba MUHAS, Deogratius Mzurikwao amesema kompyuta hizo zitawasaidia kutengeneza mifumo ya akili unde itakayowasaidia kugundua magonjwa na kwamba mpaka sasa wana teknolojia ya utambuzi wa saratani ya matiti na ugonjwa wa moyo.
Mzurikwao amesema teknolojia hizo zitawasaidia wagonjwa waliopo vijijini kutambuliwa mapema kama wana saratani au magonjwa ya moyo hivyo kupatiwa tiba mapema na kupona.
Pia amesema vifaa hivyo vitaisaidia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kubaini vifaa vinavyoletwa kutoka nje ya nchi kama vinafaa kwa matumizi ama la hivyo kuchukua hatua za kiudhibiti.
Amesisitiza wanatarajia kusimika mifumo ya mtandao kuwezesha madaktari ambao wanashindwa kupata mtandao kupandisha sampuli za magonjwa hayo kwenye mifumo watakayoitengeneza.
Kwa upande wake, mgunduzi wa akili unde kubaini ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi, Dk Sangundi Sangundi amesema kupitia kompyuta zilizopo kwenye chuo hicho waliweza kukusanya sampuli 5,000 kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Saratani Ocean Road kubaini saratani ya shingo ya kizazi.
Amesema walitumia muda wa wiki mbili kuufunza mfumo wao kubaini magonjwa na kwamba kutokana na Vifaa hivyo watatumia muda mfupi hivyo kumuwezesha mwananchi aliyepo vijijini kufanyiwa uchunguzi kwa haraka na kupatiwa majibu mapema.
“Wanawake wengi wanagundulika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi wakiwa katika hatua za mwisho hivyo kusababisha kuchelewa kupata matibabu,” amesema.
Amefafanua daktari aliyepo katika vituo vya afya wanaweza kutuma picha ya sehemu ya nyama inayodhaniwa kuwa na saratani na kuituma kwenye mfumo na kwamba utarudisha majibu ndani ya muda mfupi.