Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amewaahidi wakulima wa viungo visiwani humo kuwawekea bei elekezi ili kuwalinda dhidi ya unyonyaji wa madalali na walanguzi.
Othman amesema hatua hiyo, itawawezesha pia wakulima hao wa viungo mbalimbali ikiwemo karafuu, vanila na pilipili hoho kupata faida kubwa na kuona tija ya kilimo hicho.
Mgombea huyo, ameeleza hayo leo Jumanne Septemba 30, 2025 baada ya kuwatembelea wakulima hao Shehia ya Mtambwe Daya, Mkoa wa Kaskazini Pemba katika mwendelezo wa kampeni za kusaka kura, akitokea Unguja.
Katika maelezo yake, Othman amesema ardhi ya Pemba ina uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao yenye thamani kubwa duniani, lakini waliopewa madaraka wameshindwa kutumia fursa hiyo kwa maendeleo ya watu.
Othman amesema changamoto hizo zinatokana na mifumo mibovu ya Serikali akidai bado haiwajali wakulima wadogo ikiwemo kuwawekea miundombinu bora ya kilimo hicho, jambo litakalokwenda kutekelezwa na ACT Wazalendo, kikishika dola.
“Serikali nitakayoiongoza itatatua na kuondoa changamoto hii ili wakulima wanufaike na rasilimali zao. Tutasimamia uzalishaji, masoko, ubora na usafirishaji wa viungo.
“Hatua hii itasaidia kuwaunganisha wakulima na wanunuzi wa kimataifa kwa mikataba ya moja kwa moja. Serikali itajenga viwanda vidogo vya kusindika viungo Pemba ili kuviongeza thamani ya mazao kabla ya kwenda sokoni,” amesema Othman.
Othman ametolea mfano Madagascar ambayo inaingiza mamilioni ya dola kila mwaka kupitia mauzo ya vanila, akisema Zanzibar inaweza kufanya zaidi kwa kutumia ardhi yake yenye rutuba.
“Tutahakikisha kunakuwepo miundombinu ya umwagiliaji, pembejeo bora na elimu ya kilimo ili kurahisisha uzalishaji na kuongeza tija,” ameeleza Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo.

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud akilitazama zao la vanila baada ya kumtembelea eneo la Mtambwe, Pemba linakolimwa.
Katika mkutano huo, baadhi wakulima wa viungo walimweleza Othman kuwa walishakata tamaa kuhusu bidhaa hizo, kutokana na ukosefu wa masoko na gharama kubwa za uzalishaji.
Bakari Mataka amedai licha ya kulima viungo kwa zaidi ya miaka 15, lakini hajawahi kupata faida inayomwezesha kujikimu na kumudu kuendesha familia yake.
Kwa upande wake, Shabani Ali amesema wana mazao mengi nyumbani lakini hawajui pakuyapeleka ili kupata bei nzuri na kurudisha gharama za uzalishaji wanazozitumia.
Jioni Othman atafanya mkutano wa hadhara wa kunadi sera zake katika uwanja wa mpira Daya Shehia Jimbo la Mtambwe, Pemba.