Zanzibar, kwa sasa, imekuwa kinara wa maendeleo katika sekta ya elimu, ikiongoza kwa kiwango cha kusoma na kuandika (KKK), matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), na ujuzi wa lugha. Hali hii, inayoweka visiwa hivyo mbele ya baadhi ya maeneo ya bara la Afrika, inatokana na juhudi za makusudi za Serikali na wadau mbalimbali katika kuboresha miundombinu ya elimu na kutoa mazingira bora kwa wanafunzi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Uchambuzi wa Elimu na Kiwango cha Kusoma na Kuandika iliyotolewa Mei, 2025 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Zanzibar inaongoza kwa kiwango cha kusoma na kuandika, ambapo takriban asilimia 96.6 ya wakazi wanajua kusoma na kuandika, huku Tanzania Bara ikiwa na asilimia 83.
Huu ni ushahidi tosha kwamba visiwa vya Zanzibar vimefanikiwa kuwa na kiwango cha elimu kinachokaribia viwango vya juu zaidi barani Afrika.
Hii ni tofauti kubwa na hali ya Tanzania Bara, ambako idadi kubwa ya watu na changamoto za miundombinu zimekuwa kikwazo katika kufikia malengo ya elimu bora.
Zanzibar imekuwa na mafanikio makubwa si tu katika sekta ya kusoma na kuandika, bali pia katika matumizi ya lugha. Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 700,000 Zanzibar (karibu asilimia 36.2) wanajua Kiswahili na Kiingereza kwa pamoja, huku Tanzania Bara ikiwa na asilimia 20.5 tu ya watu walio na ujuzi wa lugha hizi mbili.
Huu ni ushahidi mwingine kwamba Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kutumia lugha kama chombo cha mawasiliano na maendeleo.
Pamoja na mafanikio ya kielimu, Zanzibar imekuwa kielelezo cha matumizi ya Tehama katika elimu. Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya asilimia 88.8 ya watu wa Zanzibar wanamiliki simu za mkononi, ikilinganishwa na asilimia 82.3 ya watu wa Tanzania Bara.
Aidha, matumizi ya Tehama katika elimu yameendelea kuongezeka, ambapo zaidi ya 320,000 (asilimia 16.1) ya watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea wanatumia Tehama kwa ajili ya kujifunza.
Hii ni tofauti kubwa na Tanzania Bara, ambapo asilimia 9.8 ya watu wanatumia Tehama katika kujifunza.
Profesa Ngogo Mang’enyi, mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) Mwanza, anaeleza kuwa tofauti hii inatokana na ukubwa wa idadi ya watu kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.
Anasema kwamba Zanzibar, ikiwa na wakazi milioni 2 pekee, imeweza kuwekeza kwa urahisi zaidi katika miundombinu ya elimu na Tehama, jambo ambalo limekuwa vigumu zaidi kwa Tanzania Bara yenye wakazi zaidi ya milioni 60.
Dk Zubeda Mussa kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) anasema kuwa idadi ndogo ya wakazi wa Zanzibar, imeirahisishia Serikali kushughulikia changamoto za elimu kwa ufanisi zaidi. “Ni rahisi kujenga shule, vyuo, na kuweka miundombinu ya Tehama kwa idadi ndogo ya watu kuliko kwa mamilioni ya watu Bara,” anasema.
Mageuzi ya Elimu Zanzibar
Kwa miaka mingi, Zanzibar ilihesabiwa nyuma katika sekta ya elimu, lakini hali hiyo imebadilika kwa haraka. Katika miaka ya karibuni, Zanzibar imefanikiwa kuboresha miundombinu ya elimu kwa kiwango kikubwa.
Kwa mfano, kuanzia mwaka 2020 hadi 2024, Serikali ya Zanzibar imejenga madarasa 4,810, ikiwa ni pamoja na shule 36 za ghorofa, na kugawa zaidi ya kompyuta 3,000 mpya kwa shule za Serikali.
Hali hii imeongeza ubora wa elimu na kuboresha mazingira ya kujifunza, hasa kwa kutumia mifumo ya madarasa janja katika baadhi ya shule.
Abdalla Khamis Juma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, anasema kuwa Serikali imefanikiwa kutoa vifaa vya kisasa vya kujifunzia na kuboresha miundombinu ya shule, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu. “Tumeboresha miundombinu, tumewajiri walimu, na kuweka mazingira bora. Kwa sasa Zanzibar inaoongoza hata katika matumizi ya Tehama kwa shule za serikali, ukilinganisha na nchi nyingi za Afrika,” anasema.
Katika mwaka 2024, kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha sita Zanzibar kilifikia asilimia 96.8, kiwango ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya visiwa hivyo. Mabadiliko haya yanaonyeshwa pia kwa ongezeko la wanafunzi wanaofaulu na kujiunga na vyuo vikuu na vya kati, huku baadhi ya shule zikiongeza michepuo ya darasa la saba kutoka asilimia 5.5 hadi asilimia 15.
Aidha, mifumo ya madarasa janja au “smart room” imesaidia sana katika kuboresha ufundishaji na kujifunza Zanzibar.
Mohamed Ali Mohamed, mwalimu katika Sekondari ya Mtakuja, anasema kwamba kwa sasa hakuna haja ya kutoa nakala nyingi za masomo, kwani kila mwanafunzi anapata taarifa za masomo kwa njia ya kidigitali.
“Somo linaingizwa kwenye mfumo na kila mwanafunzi analipata, jambo hili limerahisisha ufundishaji na kuongeza ufaulu Zanzibar,” anaeleza.
Wanafunzi pia wameshuhudia mabadiliko makubwa katika mfumo huu. Suleisa Iddi Ali, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, anasema kuwa mfumo huu umewasaidia kuelewa kwa haraka kile wanachojifunza, badala ya kutumia makaratasi pekee.
“Tunashukuru Serikali kwa kutujengea mazingira bora ya kujifunza, na tunahakikisha kuwa tutaleta matokeo bora zaidi,” anasema.
Serikali ya Zanzibar inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Kwa sasa, kuna mpango wa kujenga shule 100 mpya na kuziunganisha na mkongo wa taifa wa intaneti.
Aidha, Serikali imeongeza bajeti ya wizara ya elimu kutoka Sh265 bilioni hadi Sh860 bilioni, huku ikiajiri walimu 5,265 na kutoa posho za nauli kwa walimu.
Pia, mashirika yasiyo ya kiserikali kama Room to Read na Karemjee Foundation, yameungana na serikali kutoa msaada wa vifaa vya kujifunzia, vitabu na kuboresha maktaba shuleni.
Joan Minja, Mkurugenzi wa Shirika la Room to Read, anasema kuwa ushirikiano wao na serikali umeongeza kasi ya kuboresha matokeo ya elimu kwa kutoa vifaa vya kujifunzia na kuboresha mazingira ya ujifunzaji. Naye, Caren Rowland, Mkurugenzi wa Taasisi ya Karemjee, anasema kuwa wao wamekuwa wakisaidia kukuza mapenzi ya wanafunzi kwa kusoma na kuongeza ujasiri wao.
Zanzibar, kwa sasa, imeonyesha kuwa ni kielelezo cha mafanikio katika sekta ya elimu, matumizi ya Tehama na kukuza ujuzi wa lugha.
Ingawa idadi ya watu ni ndogo, serikali ya Zanzibar imeweza kuweka mazingira bora ya kujifunza na kuwekeza katika miundombinu ya kisasa.
Hii inadhihirisha kuwa hata katika hali ya changamoto, juhudi za makusudi na mipango bora ya serikali zinaweza kuleta mabadiliko makubwa na kuleta maendeleo endelevu.
Zanzibar inaonekana kuwa mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine za Afrika, katika kuboresha elimu na matumizi ya teknolojia katika sekta hiyo.