MECHI tatu ilizocheza Coastal Union, ikifungwa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma, ikipoteza kwa mabao 2-1 dhidi JKT Tanzania na kushinda bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons, straika wa timu hiyo Adam Salamba hajaonekana uwanjani.
Salamba amesema sababu ya kutocheza mechi hizo ni kutokana na kutopata kibali cha uhamisho wa kimataifa (ITC) kilichoiomba Coastal katika klabu ya Branes aliyoichezea mwaka 2024.
“Kibali kikitumwa basi ninaweza kuanza majukumu yangu, maana tayari uongozi umeishakiomba, wanasubiri majibu kutoka klabu ya Branes niliyoichezea mwaka 2024.
“Lakini naendelea na mazoezi na timu kuhakikisha ninauweka mwili wangu tayari kwa ajili ya kazi, ili ITC ikifika niendelee na majukumu yangu kama kawaida,” amesema Salamba.

Salamba baada ya kucheza kwa muda mrefu nje akizitumikia klabu mbalimbali kama Libyan, El Mahalla, Js Saoura na Al-Jahra, amesema amerejea nyumbani kujipanga upya, ikitokea kapata ofa nje basi ataondoka.
“Kurejea nyumbani kujipanga siyo kitu kibaya, kikubwa najua kitu gani nakihitaji katika mpira wa miguu, nilikuwa nafuatilia Ligi Kuu Bara najua ina ushindani na ngumu, nipo tayari kwa ajili ya kukabiliana na hilo,” amesema Salamba aliyewahi kuzitumikia Stand United, Lipuli, Simba na Namungo FC.