Morogoro .Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimewataka wananchi wa Morogoro kujiandaa kunufaika na neema ya sera ya viwanda, kikiahidi kurejesha hadhi ya mkoa huo kuwa kitovu cha viwanda kama ilivyokuwa enzi za Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mlimba, Leo Jumanne Septemba 30, 2025, Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chaumma, Salum Mwalimu amesema tayari mipango ya viwanda imeandikwa katika ilani ya chama na kinachosubiriwa ni wananchi kuwachagua Oktoba 29, 2025 ili iunde Serikali itakayotekeleza ahadi hizo.
“Morogoro ni mkoa wa kimkakati kwa ajili ya viwanda kwa sababu upo katikati ya Bandari ya Dar es Salaam na Tanga, jambo linalorahisisha usafirishaji wa bidhaa,” amesema Mwalimu.
Amesema viwanda vilivyowahi kujengwa mkoani humo vilikufa, lakini Chaumma imelenga kufufua taswira ya Morogoro kuwa mkoa wa viwanda.
Amebainisha kuwa, moja ya viwanda vya kipaumbele ni vya uzalishaji wa sukari ili kupunguza gharama kwa wananchi, hususan wa Mlimba, ambako sukari huuzwa hadi Sh4,000 kwa kilo moja licha ya kuwepo kwa mazingira mazuri ya kilimo cha miwa.
“Haiingii akilini Mlimba mnunue sukari kwa bei hiyo wakati mna uwezo wa kuzalisha wenyewe. Tupeni Chaumma, tutaleta mabadiliko,” amesema Mwalimu.
Katika mkutano huo, ameeleza pia dhamira ya chama kujenga barabara ya lami kuanzia Ifakara kupitia Mlimba hadi mkoani Njombe, wakilenga kurahisisha usafirishaji wa mazao na kuongeza tija kwa wakulima.
“Chaumma tunataka mkulima asafirishe mahindi au mpunga wake bila matatizo, barabara nzuri italeta bei nzuri sokoni na kuwawezesha wananchi kujenga nyumba bora,” amesema mgombea urais huyo.
Pia, amesema sera ya miundombinu ya Chaumma inaweka kipaumbele katika maeneo ya uzalishaji kama ya Mlimba.
Hata hivyo, amekosoa mtazamo wa Serikali wa kujenga barabara akidai hazina mchango wa moja kwa moja katika maendeleo ya wananchi.
“Hatukubali ujenzi wa barabara za kwenda saluni kabla ya zile za maeneo yanayozalisha mazao. Hii si haki kwa wakulima wetu,” amesisitiza Mwalimu.
Akizungumza katika mkutano huo, mgombea ubunge wa Mlimba kupitia Chaumma, Suzan Kiwanga ameibua hoja kuhusu changamoto ya miundombinu, hususan barabara ya kutoka Mlimba hadi Njombe.
Amesema barabara hiyo ya mkoa ilishatengewa fedha tangu mwaka 2020, lakini hadi sasa haijajengwa licha ya kuwa katika mipango ya Serikali.
“Nichagueni niende nikazitafute zilipo, maana wakati natoka bungeni 2020, fedha zilishatengwa lakini hadi sasa, hii barabara haijajengwa,” amesema Kiwanga kwa msisitizo, huku akieleza kuwa fedha hizo zilitolewa na benki kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Kiwanga ameahidi kushughulikia suala hilo atakapopewa ridhaa na wananchi huku akisema ujenzi wa barabara hiyo utawezesha usafirishaji rahisi wa mazao kutoka vijijini kwenda sokoni, jambo litakalopunguza gharama za maisha kwa wananchi wa Mlimba.
Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chaumma, John Mrema amewaomba wananchi wa Mlimba kumpigia kura Kiwanga, akimtaja kwamba ni ‘mama wa shoka’ mwenye rekodi ya kuwawakilisha wananchi kwa ujasiri na ufanisi bungeni.
“Kiwanga ni sauti ya wananchi, ni jasiri na ana uchungu na maendeleo ya watu wa Mlimba. Tumchague arudi bungeni akamilishe kazi aliyoianza,”amesema Mrema.