Samia aahidi kukamilisha miradi iliyoombwa na Msuya Kilimanjaro

Kilimanjaro. Mgombe urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amewasili mkoani Kilimanjaro akiahidi kukamilisha miradi mikubwa miwili wilayani Mwanga aliyoombwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya.

Miradi hiyo ni wa maji Same-Mwanga Korogwe wenye thamani ya Sh304.4 bilioni ulioweza kupandisha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 75 hadi asilimia 85 na ule wa barabara ya mzunguko ya Msuya.

Kilimanjaro unakuwa mkoa wa 18 kwa mgombea huyo tangu kuzinduliwa kwa kampeni hizo Agosti 28,2025 jijini Dar es Salaam kisha kuzunguka kwenye mikoa mbalimbali akipita na kunadi ilani ya CCM huku akiomba ridhaa ya wananchi kuongoza nchi kwa miaka mitano ijayo.

Kabla ya Kilimanjaro, mgombea huyo ameshafanya kampeni zake katika mikoa ya Tanga, Pwani, Mtwara, Lindi, Ruvuma, Kusini Pemba, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kigoma,Tabora, Singida, Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe, Dodoma na Morogoro.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhra uliofanyika Mwanga na Samia leo Jumanne Septemba 30, 2025, amesema ni faraja kwake kuona ametekeleza miradi yote miwili aliyoomba Msuya na aliiona kabla hajafariki dunia.

“Mradi huu wa maji ulikuwa wa kufa na kupona wa Msuya, Alinifuata na kuniomba miradi  miwili ambayo ameiona kabla Mungu hajamchukua. Kama nilivyomuahidi, nawahakikishia wana Mwanga huu mradi unakwenda kukamilika,” amesema Samia.

Sambamba na uendelezaji wa mradi huo, mgombea huyo ameahidi kumaliza changamo ya ulanguzi wa mazao ya wakulima kwa kuanzisha masoko mawili ya kisasa wilayani Mwanga.

“Mwanga kuna wakulima wazuri wa mahindi, mpunga, maharage na vitunguu changamto iliyopo ni ukosefu wa masoko. Nimeambiwa hapa mjini hakuna soko sasa tutajenga soko la kisasa. Pia, katika kukomesha walanguzi kwenda mashambani kule kata ya Kileo tutajenga soko,” amesema.

Kuhusu changamoto ya magugu maji katika ziwa Jipe inayotajwa kuathiri shughuli za uvuvi na vyanzo vya maji, mgombea huyo amesema tayari Sh1.9 bilioni zimeshatengwa kwa ajili ya kununua mitambo ya kuondoa magugu maji hayo kwa haraka.

“Wana Mwanga niwaombe mtupe kazi tukajenge utu wa mtu, mkatupe ushindi wa kishindo itakapofika Oktoba 29,” amesema.

Akihutubia mkutano wilayani Same yenye majimbo mawili ya uchaguzi ya Same Magharibi na Same Mashariki, Samia amesema endapo Serikali yake itapata ridhaa ya kurejea madarakani, itajenga barabara za milimani kwa kiwango cha lami na zege ili kurahisiha usafirishaji wa zao la tangawizi.

“Nafahamu barabara ni ajenda yenu kubwa  wana Same, mkitupa ridhaa tutakwenda kujenga barabara za milimani ili wakulima watangawizi wasafirishe mazao yao.

“Tumeshaanza ujenzi wa Barabara ya Mkomazi-Same tutaikamilisha kwa sababu tunafahamu barabara hii nayo ni muhimu kwa usafirishaji wa mazao,” amesema Samia.

Kwenye sekta ya kilimo, ameahidi ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika Bonde la Ruvu sambamba na ujenzi wa bwala la Mkomazi ili kusaidia kilimo cha umwagiliaji Korogwe na Same.

“Ni imani yetu kuwa maeneo haya yatazalisha mazao ya kutosha na kukuza ajenda ya kilimo biashara. Niwaambia wana Same yajayo yanafurashisha hivyo kapigieni kura CCM ili tunawirishe utu wa Mtanzania,” amesema.

Mbali na hatua hizo, Samia amesema Serikali yake itaongeza bajeti ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) ili kuongeza barabara za vijijini.

Kwenye nishati ya umeme, amesema mpango uliopo ni kumaliza adha kwa kuhakikisha ndani ya miezi 18 akiingia madarakani, vitongoji vyote vilivyosalia vitakuwa vimeunganishwa na huduma hiyo.

Kuhusu huduma za afya, amesema ahadi ya chama chake ni kuendelea kuhakikisha Watanzania wanapata huduma hizo kwa uhakika kwa kujenga miundombinu na kuajiri watoa huduma.

“Nikiwa kwenye kampeni mwaka 2020 kama mgombea mwenza, nilikuja Hedaru nikakuta zahanati mbovu, mbaya zaidi ilikuwa inatoa huduma za kujifungua sikufurahishwa hata kidogo na hali ile hivyo nikajiweka nia ya kubadilisha hali ile Tanzania nzima na kwa hakika nimeweza.

“Kufa kupo lakini kujifungua au kuleta maisha mapya isiwe sababu tutaendelea kuboresha huduma za afya kwa kujenga vituo, kuweka vifaa tiba na watoa huduma,” amesema.

Kuhusu uvamizi wa wanyamapori waharibifu amesema tayari kimejengwa kituo cha udhibiti na endapo atapata ridhaa Serikali yake itaongeza jitihada za udhibiti kwa kuweka ndege nyuki za kuwafuatilia na kuwafukuza wanyama.

Sumaye atia neno kaskazini

Akizungumza kwenye mkutano huo, waziri mkuu mstaafu na mratibu kampeni za CCM kanda ya kaskazini, Frederick Sumaye amesema kanda hiyo imepanga kufuta historia ya mbaya kwa chama hicho huku akiahidi imejipanga kuongoza kwenye wingi wa kura.

“Kaskazini imejiandaa kukufurahisha na kukifurahisha Chama cha Mapinduzi safari hii, kanda hii sehemu zake zingine kwa kawaida hazikuwa vizuri lakini wanataka kufuta historia hiyo.

“Watafuta historia hiyo kwa kukupa kura za heshima, watakupa kura kwa sababu kuna alama nyingi umeweka katika majimbo, kata na vijiji vyote vya kanda ya kaskazini,” amesema Sumaye.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Patric Boisafi amesema mkoa huo umeshaamua kuwa Oktoba 29, wananchi wote watajitokeza kupiga kura na kuwachagua viongozi wa chama hivyo.

“Kilimanjaro tuko salama, tunapambana kuhakikisha Oktoba 29 mgombea wetu unapata kura unazostahili, wananchi tupo tayari kukupa kura kwa sababu tunajua utaendelea kufanya kazi ya kutuletea maendeleo,” amesema Boisafi.

Akizungumza kwenye mkutano huo mgombea ubunge wa jimbo la Same Mashariki, Anna Malecela amesema katika kipindi cha miaka minne maendeleo makubwa yamepatikana kwenye jimbo hilo.

“Tulikuwa na kituo cha afya kimoja sasa tumepata vinne, miaka yote tulikuwa tunaomba barabara ya Mkomazi Kisiwani-Same ijengwe hatimaye tumepata kilomita 100

za lami zinajengwa kwa sababu hii na nyingine nyingi ya kuchagua CCM,” amesema Anna.

Mgombea ubunge wa jimbo la Same Magharibi David Mathayo amesema vijiji vyote katika jimbo hilo vimepata huduma ya umeme huku akiomba vitongoji 110 vilivyosalia kwenye jimbo hilo kuunganishwa na nishati ya umeme.

Hata hivyo Mathayo ameomba barabara ya kilomita 48 kuwezesha wananchi wake kutoka maeneo ya milimani kupata huduma za usafiri katika kipindi chote cha mwaka.

Mkazi wa Same Rehema Ally wa amesema miaka yote wamekuwa wakisikia ahadi zinazovutia lakini utekelezaji wake ni mdogo.

 “Kila uchaguzi tunasikia ahadi za maji, barabara na hospitali. Tunataka safari hii tusisikie maneno, bali tuone utekelezaji wa kweli baada ya uchaguzi.”

Kwa upande wake Hassan Mkude amepongeza jinsi mikutano ya kampeni inavyoendeshwa kwa utulivu na kusisitiza hali hiyo kudumishwa katika kipindi chote hadi siku ya kupiga kura. 

“Hali ya amani katika mikutano inatupa matumaini makubwa hadi sasa hatujasikia popote zilipotokea vurugu. Tunataka hali iendelee hivi hadi Oktoba 29 tuweze kupiga kura kwa utulivu.Tusishawishike kufanya mambo yasiyofaa pakiharibika hapa hakuna pa kukimbilia,” amesema Mkude.

Grace Lyatuu mkazi wa Mwanga amesema bado kuna changamoto ya usawa katika majukwaa ya kampeni kwa vyombo vya habari kutotoa nafasi kwa usawa kwa wagombea.

“Kuna wakati mgombea mmoja anapata nafasi kubwa zaidi ya kujitangaza kuliko wengine.Tunataka vyombo vya habari viwape nafasi sawa wagombea wote ili wananchi wafanye uamuzi sahihi,” amesema Grace.