Siku tatu zamtosha Mgunda kuikabili Simba

KOCHA Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, amesema kikosi chake kipo tayari kukabiliana na Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kesho Oktoba 1, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, saa 2:15 usiku.

Mgunda amesema siku tatu walizokuwa jijini Dar es Salaam wamefanya maandalizi kuhakikisha wanapata matokeo mazuri licha ya kukutana na timu yenye kikosi kilichosheheni wachezaji wazuri.

“Tuna siku tatu hapa mjini, tumejiandaa vizuri kuja kukutana na timu nzuri, yenye wachezaji wazuri, maandalizi yote tumeyafanya ili tufanye vizuri, tuhaiheshimu Simba, tumekuja kushindana nao,” amesema Mgunda.

Namungo inakwenda kukutana na Simba ikiwa tayari imeshuka dimbani mara mbili kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu ikianza na sare ya 1-1 dhidi ya Pamba Jiji, kisha ikaichapa Tanzania Prisons bao 1-0, mechi zote zikichezwa Uwanja wa Majaliwa uliopo Lindi.

Mgunda ambaye amewahi kuinoa Simba, msimu uliopita akiwa na Namungo alishuhudia kikosi chake kikipokea vichapo mara mbili vya mabao 3-0 mbele ya Wekundu wa Msimbazi.

Mbali na hivyo, Namungo kesho itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kutoshinda mechi yoyote ya mashindano dhidi ya Simba kwani timu hizo zimekutana mara 13, Simba imeshinda mechi nane na sare tano.

Katika mechi hizo 13, moja ni ya Kombe la FA iliyochezwa Januari 1, 2021 ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.