Dar es Salaam. Tanzania kupitia jumuiya za kikanda inaliomba Bunge la Marekani kuongeza muda wa mkataba maalumu wa kibiashara wa Sheria ya Ukuaji na Fursa Afrika (Agoa), unaozipa nchi za Afrika upatikanaji wa soko la Marekani bila kulipia maelfu ya bidhaa.
Ripoti zinaonesha kuwa, mkataba wa Agoa unafikia tamati leo Septemba 30, 2025 na kupitia hilo nchi za Afrika zitapoteza ufikiaji maalumu wa bure wa soko hilo lililosaidia utengenezaji wa nafasi za kazi, kuboreshwa kwa minyororo ya ugavi na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Marekani na Afrika.
Agoa haijasaidia tu wauzaji bidhaa wa Kiafrika, bali imenufaisha kampuni za Marekani kwa kutoa upatikanaji wa malighafi ya bei nafuu na kuhimiza uwekezaji wa Marekani barani Afrika.
Akizungumzia suala hilo leo Jumanne Septemba 30, 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah amesema Serikali kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inasema iwapo mpango huo hautahuishwa, viwanda na wafanyabiashara wengi wa ndani wanaweza kukumbwa na changamoto.
“Tuna kampuni ambazo tayari zinanufaika na Agoa. Iwapo mpango hautauishwa, wanaweza kupoteza soko la Marekani na kukabiliana na changamoto kubwa za kibiashara,” amesema.
Aidha, tayari Tanzania ilishatoa ombi la kurefushwa kwa mkataba huo miaka miwili iliyopita kwa kuwa, wakati wa ziara ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris Machi 30, 2023 Rais Samia (Suluhu Hassan) alitumia ujio wa Kamala kuomba Marekani kuuongezea muda mkataba wa Agoa ili kutoa fursa za ukuaji wa kibiashara kwa nchi za Afrika.
“Nchi za Afrika ikiwamo Tanzania zinaomba kurefushwa kwa mkataba huu kwa miaka 10 ili wawekezaji wanaofanya biashara zao wawe na uhakika wa kuwa endelevu hapa nchini,”amesema Rais samia.
Agoa ni mpango wa biashara ulioanzishwa na Marekani mwaka 2000 ili kusaidia uchumi wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara unaoruhusu zaidi ya bidhaa 1,800 zikiwamo za nguo, kilimo na madini kuingia katika soko la Marekani bila kutozwa ushuru.
Hivi sasa, nchi 32 za Afrika zinanufaika na mpango huo huku baadhi kama Lesotho na Madagaskar, wanaitegemea zaidi kwa kusafirisha bidhaa kama vile nguo huku mnamo 2023, uagizaji wa bidhaa za Amerika chini ya Agoa ulikuwa na thamani ya karibu Dola 10 bilioni za Marekani.
Mtaalamu wa uchumi na biashara, Oscar Mkude amesema mustakabali wa AGOA hauelewekei, ingawa mazungumzo yalikuwa yameanza hapo awali, sera za ushuru zilizowekwa na Rais wa Marekani Donald Trump zilivuruga maendeleo na bado hakuna mfumo wazi wa kufanya upya.
“Inawezekana, lakini hakuna uwezekano mkubwa. Tunaweza kuendelea kufanya biashara na Marekani kupitia hali ya kawaida ya soko, ambayo ni pamoja na ushuru wa juu,” amesema Mkude.
Pia, amesema mauzo muhimu ya Tanzania chini ya Agoa ya mwaka 2023 ni pamoja na dhahabu ilikuwa na thamani ya Dola 51.1 milioni , mazao ya kilimo Dola 28 milioni za Marekani na nguo zenye thamani ya Dola za 11 milioni Marekani.
“Bado, jumla ya mauzo ya nje kwenda Marekani ni asilimia 1.86 tu ya mauzo ya nje ya Tanzania takribani Dola milioni 210 kati ya Dola bilioni 11.3 kwa dunia nzima,” amesema.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE), Dk Abel Kinyondo amesisitiza umuhimu wa kuelewa kile ambacho nchi inazalisha ili kukuza uchumi endelevu.
Amesema kuongeza uwezo wa nchi wa kuongeza thamani ni muhimu.
“Kutia saini mikataba mingi ya biashara, ikiwa ni pamoja na Sheria ya Ukuaji na Fursa Afrika, haina umuhimu kama hatuna bidhaa shindani au huduma za kutoa kwa kubadilishana,” amesema Dk Kinyondo.
Amesema bila kuimarisha uzalishaji wa ndani na kuboresha uongezaji thamani, mikataba hiyo haiwezi kunufaisha kikamilifu uchumi wa nchi.
“Ipo haja ya kuwa na uwekezaji wa kimkakati katika viwanda vya ndani na ubunifu ili kukuza uwezo wa Tanzania kuuza nje na kuhakikisha ushiriki wa maana katika masoko ya kimataifa,” amesema.
Hili linakwenda kushuhudiwa wakati ambao nchi za Afrika zinafanya kazi ya kuimarisha biashara ya kikanda kupitia Eneo Huru la Biashara Bara la Afrika (AfCFTA) licha ya jambo hili kuhitaji muda ili kuanza kuzaa matunda yanayokusudiwa.