Tuwafunde watoto moyo wa kuchakarika kimaisha

Dar es Salaam. Katika mitaa mingi ya miji yetu na vijiji vyetu, simulizi za maisha ya vijana wasio na mwelekeo zimekuwa jambo la kawaida. 

Unakutana na kijana wa miaka 25, ana afya njema, nguvu za mwili bado zimemiminika, lakini hana kazi, hana mpango, na hata hana ndoto ya nini afanye. 

Ukimuuliza kesho atakuwa wapi, anakutazama kwa macho yaliyokosa nuru ya matumaini. Ni hali inayotia uchungu, kwa sababu taifa letu linapoteza hazina kubwa ya nguvu kazi.

Ukweli mchungu ni kwamba tunakosa moyo wa kuchakarika. Tunakosa ule msukumo wa kupambana na mazingira ili tupate riziki, ili tujitengenezee nafasi ya kuishi maisha yenye heshima.

 Wazee wetu walikuwa wachakarikaji, walilima mashamba makubwa bila trekta, walivua samaki baharini bila mitambo ya kisasa, walichonga mashua, walitengeneza zana, na walipambana na vikwazo vingi. Lakini sisi, kizazi cha sasa, mara nyingi tunataka kila kitu kiwe rahisi.

Mfumo wa ujamaa uliotuweka pamoja baada ya Uhuru ulikuwa na nia njema. Ulitufundisha mshikamano na mshikikano. 

Lakini, kwa namna fulani, ulitulevya. Tuliishi tukiamini chakula na msaada vitapatikana bila kuchakarika sana. Ulipokosa nyumbani kwako, ulikimbilia kwa mjomba au shangazi aliye jirani, na hukulala njaa.

Utamaduni huu wa utegemezi uliota mizizi mioyoni mwetu. Hadi leo hii, wengi wetu hatuoni uchungu wa kukosa kazi, kwa sababu tunaamini daima kutakuwa na mtu wa kutusaidia.

Tunapaswa kuandaa watoto wetu mapema, kuanzia shuleni na hata nyumbani, wawe wachakarikaji kimaisha.

Shule zetu mara nyingi zimejikita katika nadharia pekee,  hesabu, fizikia, historia, lugha. Bila shaka masomo haya ni muhimu, lakini ni lazima tuulize: je, shule inamwandaa mtoto kuwa mchakarikaji? Je, inamfundisha namna ya kutumia mikono yake na ubunifu wake? Je, inamfundisha kutengeneza kitu kinachoweza kuuzwa sokoni, au kujitegemea akitoka darasani? Mara nyingi jibu ni hapana.

Ulimwengu wa leo unahitaji watoto wanaojua kupambana, wanaojua kubuni, na wanaoweza kuanza mradi mdogo bila kusubiri ajira ya ofisini. 

Tunapaswa kuwa niliitalo somo la “maisha halisi” shuleni,   linalofundisha mtoto namna ya kupanda mboga nyuma ya nyumba, namna ya kushona sketi au suruali, namna ya kutengeneza kikombe cha udongo, namna ya kuuza bidhaa sokoni, na namna ya kuandika bajeti ya pesa ndogo.

Tukiwa wazazi, walimu, na viongozi wa jamii, lazima tubadili mwelekeo huu. Tuwafundishe watoto kuwa wachakarikaji tangu wadogo. 

Wazazi wa mjini wanaweza kuanza kwa kumpa mtoto jukumu dogo la kuuza maji baridi mlangoni, au kumfundisha namna ya kutunza bustani ndogo ya mboga. Vijijini, mtoto anaweza kufundishwa kufuga kuku au kutengeneza kitu cha mikono. Kila hatua ndogo itamjenga mtoto kuwa na moyo wa kujitegemea.

Kizazi tunachokilea leo ndicho kitakachounda taifa la kesho. Tukiwalea watoto wenye moyo wa kuchakarika, tutakuwa na taifa lenye watu wabunifu, waliyo tayari kutafuta fursa kila kona. Tukiwalea watoto wa kutegemea, tutakuwa na taifa linaloishi kwa kulalamika.

Tunapaswa kukubali kuwa kuchakarika siyo suala la mtu binafsi pekee, bali ni suala la taifa. Taifa lenye wachakarikaji linaweza kufikia maendeleo kwa haraka zaidi, kwa sababu kila mmoja anasukuma gurudumu mbele. 

Lakini taifa lenye watu wasio na mpango, waliokaa wakisubiri msaada, litasalia nyuma.

Ni jukumu letu kuondoa ulevi huu wa utegemezi. Shule zetu zisibaki tu mahali pa kusoma vitabu, bali ziwe warsha za maisha. 

Wazazi wasibaki tu walezi wa chakula na nguo, bali wawe walimu wa moyo wa kuchakarika. Vijana wasisubiri neema kutoka serikalini, bali wajifunze kupiga hatua kwa nguvu zao wenyewe.

Kwa hakika, tunaweza kulibadili taifa letu. Tukiamua kuandaa watoto kuwa wachakarikaji kimaisha, kesho tutashangaa kuona kizazi kipya cha Watanzania wenye ndoto, wenye mipango, na wenye mikono isiyochoka. Hapo ndipo tutaacha historia ya utegemezi na kuandika historia ya mapambano na mafanikio.