Dodoma. Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umetangaza kuanza ujenzi wa minara mingine 280 katika awamu ya 10 ili kuifungua Tanzania katika mawasiliano hasa maeneo ambayo yalikosa huduma hiyo.
Kabla ya kuanza kwa ujenzi wa minara hiyo, tayari UCSAF imejenga minara 758 ambayo utekelezaji wake upo kwa asilimia 97, hivyo ujenzi wa minara mipya utafikisha jumla ya minara 1,038 iliyojengwa katika kipindi kifupi.
Katika taarifa iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Peter Mwasalyanda kwa wananchi wa Morogoro amesema baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa minara 758, tayari wameanza mpango wa kujenga kwa haraka minara mingine 280 ambayo hatua zote zimeshakamilika.
Amesema wanajenga minara katika maeneo yenye changamoto za kijiografia, jambo alilodai limekuwa kikwazo katika kufikia kasi ya ujenzi inayotakiwa hasa wakati wa upelekeaji wa malighafi.
“Hata hivyo, UCSAF imeweka mikakati thabiti kuhakikisha kila awamu inakamilika kwa wakati ili huduma zipatikane kwa idadi kubwa ya wananchi na tumekuwa tukifuatilia hatua kwa hatua kwa wasimamizi wa ujenzi huo ili wasipoteze muda kwani wananchi wanasubiri kwa hamu kubwa mawasiliano hayo,” amesema Mwasalyanda.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu huyo, ujenzi mwingine wa minara awamu ya 11 utaanza mara baada ya kukamilisha ujenzi wa minara 280 ambapo awamu hiyo pia itakwenda kujengwa minara 280 na kwamba miradi yote hiyo ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano kwa wananchi.
Walengwa zaidi ni wananchi walioko vijijini na pembezoni ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa na kuwa na mawasiliano na ndugu na jamaa zao kwani upatikanaji wa huduma za mawasiliano ni haki ya kila mwananchi bila kujali anaishi kwenye mazingira yapi.
UCSAF, pia, imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano, wananchi na wadau mbalimbali ili kuhakikisha utekelezaji wenye tija na endelevu ikiwemo kuwasaidia kushiriki kikamilifu katika shughuli za kila siku na kuchangia ukuaji wa Taifa.
Mchungaji wa Kanisa la EAGT, Mvomelo Ainea Lazaro anasema mpango wa UCSAF umesaidia kwa kiasi kikubwa kuyafungua maeneo ambayo yalionekana kuwa yametengwa na ambayo yalikuwa yakilalamikiwa zaidi kuwa hayana mawasiliano.
“Mimi nafanya mawasiliano na watu wengi kwa kazi ya uinjilishaji, huu ujenzi wa minara japo haujafikia maeneo mengi lakini kwa kiasi umesaidia sana maana kwenye kazi zetu kuzunguka vijijini wakati mwingine tulikuwa tunatengwa kabisa na familia zetu au hadi usimame juu ya mti uwasiliane na nyumbani, leo mambo ni mazuri,” amesema Mchungaji Lazaro kutoka jamii ya wafugaji.
Diwani aliyemaliza muda wake katika kata ya Pemba, Coster Reuben amekiri hali ilikuwa ngumu kwenye masuala ya mawasiliano kabla ya kuanza kwa ujenzi wa minara na mara nyingi hata usalama wa wananchi ulikuwa mdogo kwani hawakuwa wakitoa taarifa kwa wakati pindi yanapotokea matukio, jambo lililosababisha vyombo vya ulinzi kutofika kwa wakati.