Mwanza. Watu wawili wamefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa silaha za jadi na wananchi wenye hasira, baada ya kuwatuhumu kuvunja milango na madirisha na kuiba mali za wakazi wa mtaa wa Igelegele, Kata ya Mahina, jijini Mwanza.
Waliouawa ni Omary Shaban (24) na Said Bundala (35) waliokuwa wakiishi chumba kimoja cha kupanga katika mtaa huo.
Akizungumza leo Jumanne, Septemba 30, 2025, katika mkutano wake na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea Septemba 26, 2025, saa mbili usiku, baada ya wananchi kuwakamata vijana hao kwa tuhuma za wizi wa pikipiki na uvunjaji nyumba kwa nyakati tofauti.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa akizungumza leo katika mkutano na Waandishi wa habari, jijini Mwanza. Picha na Damian Masyenene
Mutafungwa amesema wananchi wa mtaa wa Igelegele, wakiwa pamoja na mtendaji na mwenyekiti wa mtaa huo, waliwakamata watu hao kwa ajili ya kuwafanyia mahojiano kuhusiana na tuhuma hizo.
Walipohojiwa walidaiwa kuwa watuhumiwa hao walikubali kufanya matukio hayo ikiwemo kuiba pikipiki ya mkazi wa mtaa huo, Hamis Nuhu, iliyoibwa Septemba 18, 2025, baada ya kuvunja nyumba ya mkazi huyo.
“Baada ya kuhojiwa na kukiri kuiba vitu hivyo, waliwaongoza wananchi hao kwenda kwenye chumba walichokuwa wanaishi ambapo, baada ya kufika, walikutwa na vitu mbalimbali vya wizi,” amesema Mutafungwa.
Ameeleza kuwa katika chumba hicho zilipatikana runinga nne (flat screen), vifaa vya kuvunjia ikiwemo nyundo na msumeno, funguo malaya mbili, funguo nyingine 70, kifaa maalumu cha umeme kinachotumika kuvunjia milango na madirisha, makufuli nane na mtalimbo.
Amesema baada ya kupatikana na vitu hivyo, wananchi wenye hasira kali na silaha mbalimbali za jadi walianza kuwashambulia vijana hao, licha ya mtendaji na mwenyekiti kuwazuia.
Baada ya ghasia hizo, viongozi wa Serikali ya mtaa huo walipiga simu kwa Jeshi la Polisi ambalo lilifika eneo la tukio na kutawanya kundi la watu na kuwachukua watuhumiwa hao waliokuwa tayari wamejeruhiwa vibaya.

Baadhi ya mali na vitu mbalimbali vilivyokutwa kwenye chumba walichokuwa wakiishi marehemu hao. Picha na Damian Masyenene
“Kutokana na majeraha hayo, vijana hao walipelekwa Hospitali ya Bugando kwa matibabu, lakini siku hiyo usiku tulipokea taarifa kwamba vijana hao wawili wamefariki dunia wakati wakiendelea kupatiwa matibabu,” amesema Kamanda huyo.
Amesema tayari ndugu wa vijana hao wameshaitambua miili yao na taratibu za kuwakabidhi kwa ajili ya maziko zinaendelea, huku msako ukiendelea kuwanasa wananchi waliojichukulia sheria mkononi kwa kuwashambulia vijana hao.