Yona Amos ajihami mapema Ligi Kuu Bara

KIPA wa Pamba Jiji, Yona Amos aliyemaliza Ligi Kuu Bara msimu uliopita akiwa na ‘clean sheet’ 11, amesema kuna mambo mengi ameyafanyia marekebisho na kuongeza ujuzi wa namna ya kuimarisha ulinzi golini.

Amesema alipata muda wa kuzitazama mechi za msimu uliyopita, zilizomsaidia kuona baadhi ya mapungufu aliyoyafanyia kazi, kuhakikisha huduma yake inakuwa bora kwa timu.

“Kila msimu unakuwa na mabadiliko ya kiuchezaji, ushindani kama kipa siwezi kujibweteka lazima nitaendelea kujifunza kila wakati, kutoka kwa makocha na kuangalia kinachofanywa na wengine.

“Mfano naweza nikaangalia ni mabao ya aina gani niliyofungwa zaidi msimu uliypita ili nikifanya mazoezi yaendane na kile ambacho nahitaji kukirekebisha, kwa sababu hata washambuliaji wanakuwa wameishawasoma makipa udhaifu wao,” amesema.

Amesema anatambua msimu huu washambuliaji watakuja kivingine, lakini tayari amejipanga kuhakikisha anafanya kazi nzuri kadri awezavyo kufanyika msaada kwa timu hiyo.

“Kila mtu aonyeshe ubora wake katika nafasi yake, lakini jambo la msingi zaidi ni kucheza kitimu na kutanguliza malengo ya timu ndipo tutakapofanikiwa kwa ukubwa,” amesema.