ZEC yaweka wazi watakaopiga kura Zanzibar, 8,325 wakosa sifa

Unguja. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetangaza kuwa jumla ya wapiga kura 717,557 ndiyo walioidhinishwa kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, baada ya kukamilika kwa mchakato wa uhakiki wa daftari la kudumu la wapigakura.

Akizungumza katika mkutano na wadau wa uchaguzi uliofanyika leo Jumanne, Septemba 30, 2025, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina, amesema jumla ya wapiga kura 8,325 wameondolewa katika daftari kutokana na kukosa sifa.

Kwa mujibu wa Faina, kati ya wapigakura walioidhinishwa, wanawake ni 378,334, sawa na asilimia 53, huku wanaume wakiwa 339,223, sawa na asilimia 47. Kati ya idadi hiyo, vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 ni 326,304 (asilimia 45), wenye umri wa miaka 36 hadi 59 ni 300,986 (asilimia 42), na walio na umri wa miaka 59 na kuendelea ni 90,267 (asilimia 13).

“Hii ndiyo nguvu ya kisiasa iliyo mbele yenu. Ni wajibu wenu wanasiasa kufahamu namna ya kuwafikia wapigakura hawa ili kuwashawishi katika kampeni,” amesema Faina.

Pia, amebainisha kuwa ZEC imeidhinisha maeneo 50 ya kupiga kura ya mapema, ambapo Unguja kutakuwa na vituo 32 na Pemba vituo 18.

“Kwa ujumla, vituo vya kupiga kura vitakuwa 1,752, kati ya hivyo, Unguja 1,294 na Pemba 458. Vilevile, kutakuwa na vituo 407 kwa ajili ya shehia 388 na shehia za ziada,” amesema.

Hata hivyo, Faina amesema tayari ZEC imepokea maombi ya waangalizi wa kimataifa kutoka nchi 10 na taasisi tatu za kimataifa, huku mchakato wa mapokezi ukiendelea kabla ya kutangazwa rasmi idadi kamili ya waangalizi watakaoshiriki.

Akizungumzia kura ya mapema, Faina amesema:“Kura ya mapema siyo kwa ajili ya wizi, bali ni suluhu iliyopatikana kutokana na ripoti za uangalizi wa mwaka 2010. Ni haki ya kikatiba inayolenga kumsaidia mpigakura mwenye dharura siku ya uchaguzi. Hata hivyo, siyo lazima kila mtu aipige kura hiyo.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi, amewataka wagombea na vyama vya siasa kutumia majukwaa ya kampeni kueleza sera na mipango ya maendeleo, badala ya lugha zenye viashiria vya uvunjifu wa amani.

Amesisitiza umuhimu wa kuamini mawakala wa vyama katika kusimamia mchakato wa uchaguzi na kukemea tabia ya kuhamasisha wananchi kulinda kura, akisema kitendo hicho ni kinyume cha sheria inayowataka wapigakura kukaa umbali wa mita 200 baada ya kupiga kura.

“Tusipotoshe wananchi kwa kuwatia kwenye majukumu yasiyo yao. Vyombo vya ulinzi vipo na mawakala wenu mliowateua wapo kuhakikisha kura zenu zipo salama. Historia inatufundisha, tusirudi nyuma,” amesema Jaji Kazi.

Pamoja na hayo, amewataka wanasiasa kuviachia vyombo husika na taasisi zenye vibali vya kutoa elimu ya mpigakura jukumu hilo, kwa kuwa wao wana uelewa mpana kuliko wanasiasa ambao mara nyingi huzingatia maslahi ya vyama.

Katika mjadala huo, baadhi ya wadau wametoa maoni yaom, akiwemo Iddi Ali Iddi aliyesisitiza kuwa watu watakaovuruga amani wachukuliwe hatua bila upendeleo.

Naye Donald Naveta kutoka Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, ameiomba ZEC kuendeleza utamaduni wa kuwapatia vitambulisho maalumu mapema, ili kurahisisha ushiriki wao katika uchaguzi.

Naye Makia Juma Ali, mwangalizi wa uchaguzi, amesema kuna umuhimu wa kutoa elimu zaidi kwa askari polisi na vikosi vya SMZ ili watambue ipasavyo vitambulisho vinavyotolewa na ZEC.

Akijibu hoja hiyo, Faina amesema mafunzo kwa vyombo vya ulinzi na usalama yataendelea kutolewa, ili kuhakikisha wanatambua majukumu yao na kusimamia mchakato wa uchaguzi kwa ufanisi na uadilifu.