Aliyekuwa Rais wa DRC Joseph Kabila Ahukumiwa Kifo kwa Uasi – Global Publishers


Mahakama ya Kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Septemba 30, 2025, imemhukumu aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Joseph Kabila adhabu ya kifo baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya uhaini, uasi na ushirikiano na magaidi.

Kesi hiyo ilisikilizwa kwa kutokuwepo kwake (in absentia) tangu Julai mwaka huu, baada ya Kabila kutojulikana alipo. Serikali ilimshitaki kwa madai ya kushirikiana na Rwanda pamoja na waasi wa M23 katika kuteka miji kadhaa muhimu ya Mashariki mwa Congo kupitia mashambulizi ya ghafla ambayo bado yanaendelea.

Mwendesha mashtaka aliiomba mahakama itoe hukumu ya kifo, akieleza kuwa Kabila alihusika moja kwa moja katika kupanga na kusaidia harakati za uasi, kula njama na kutoa msaada wa kigaidi.

Aidha, mahakama imeamuru Kabila alipe fidia ya dola bilioni 50 za Marekani kwa serikali na waathirika wa mashambulizi hayo.

Mnamo Mei 2025, Seneti ya Congo ilipitisha uamuzi wa kuondoa kinga ya kisheria aliyokuwa akiifurahia kama Rais mstaafu, jambo ambalo Kabila alililaani vikali akilitaja kuwa “kitendo cha kidikteta.”

Kabla ya hapo, Kabila alikuwa akiishi nje ya nchi kwa hiari yake, lakini aliripotiwa kurejea mjini Goma mwezi Aprili 2025 — miongoni mwa miji inayodhibitiwa na waasi wa M23. Hata hivyo, kwa sasa haijulikani alipo.

Hukumu hii imezua mjadala mkubwa, ikizingatiwa kuwa DRC ilikuwa na moratorium ya muda mrefu dhidi ya utekelezaji wa hukumu ya kifo, kabla ya kuirejesha mwaka 2024 kama njia ya kupambana na ongezeko la uhalifu na ukosefu wa usalama.