Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amesema wanaohangaika wakidhani kanisa hilo linataka kushindana, kulumbana au kushikana mieleka na Serikali, watambue halina mpango huo.
Amesema hayo leo Oktoba mosi, 2025, wakati wa maadhimisho ya misa takatifu ya jubilei ya mapadri wa jimbo hilo iliyofanyika Msimbazi Centre, Dar es Salaam. Kwa tamko hilo, amesema liwasaidie wawe na uelewa sahihi na watafute msimamo sahihi.
Kupitia mitandao ya kijamii kumesambazwa matangazo ya Dominika ya 25 ya Mwaka (C) wa Kanisa Septemba 21, 2025 ambayo hayaonyeshi ni ya parokia gani. Tangazo mojawapo lilihusu warsha ya waamini wote.
“Uongozi wa kamati tendaji ya Jimbo Kuu Katoliki la Dar-es Salaam unapenda kuwaalika waamini wote kwenye warsha ya waamini wote itakayofanyika siku ya tarehe 29/10/2025 katika viwanja vya Kristo Mfalme Tabata. Adhimisho la misa takatifu litaanza saa 2:00 asubuhi,” linaeleza tangazo hilo na kuongeza:
“Mada mbalimbali zitatolewa ikiwemo uchaguzi na uongozi katika kanisa. Burudani ya muziki mtakatifu na michezo itakuwepo. Ada kwa kila mshiriki ni Shilingi 5,000. Wote tunaalikwa kushiriki. Pia viongozi wa kanda mnaombwa kufika ofisini kwa katibu kwa ajili ya kuchukua kadi za michango kwa ajili ya kuzigawa kwenye jumuiya.”
Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema: “Naomba kutamka wale mnaotumia vilongalonga, wale mnaopitapita kwenye mitandao mtafahamu kwamba kuna jambo ambalo kwa siku hizi limekuwa likisambaa kwenye mitandao.”
“Nitangazo lililotolewa kuhusu semina ya walei, naomba nitamke awali ya yote kwamba, tangazo hilo halikutolewa na ofisi yangu,” amesema.
Amesema: “Kwa hiyo, siyo tangazo linalobeba saini yangu au lililotangazwa kupitia kwa Chancellor au katibu mkuu, hilo liwafanye kwamba siyo tangazo rasmi.”
Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema jambo la pili ni kuwa, jambo lililotangazwa kwamba litafanyika Oktoba 29, 2025 katika kalenda ya jimbo limepangwa kufanyika Novemba 29, 2025.
Oktoba 29, 2025 imetangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwa siku ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani nchini.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema: “Kwa hiyo, wale wanaohangaika wakidhani kwamba Kanisa Katoliki linataka kushindana, kulumbana au kushikana mieleka na Serikali watambue kwamba, sisi hatuna mpango huo. Kwa hiyo, tamko hili langu liwasaidie muwe na uwelewa sahihi na mfuate msimamo sahihi.”
Amewaeleza wanapoona matangazo yametolewa kwenye vyombo vya habari, wayachunguze vizuri kabla hawajaanza kuhaha.
“Maana yake siku hizi kumekuwa na kuhaha kwingi na huko ni kutokana na kutokuwa makini kutokana na kutochambua na kubainisha uhalisia wa jambo linalotangazwa,” amesema.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi kujilinda na taarifa potofu, uzushi, uhalifu na ulaghai mtandaoni kupitia kampeni ya kufuta kabisa taarifa hizo ijulikanayo “Futa Delete Kabisa”.
Kampeni hiyo inalenga kutoa elimu kwa umma kuhusu usalama wa taarifa na umuhimu wa kuhakiki taarifa zinazopokewa kabla ya kusambaza.
Jeshi la Polisi mara kadhaa limekuwa likionya na kuchukua hatua kuhusu habari za uongo na upotoshaji zinazochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.