Mfalme akamuona yule mtoto wa maskini akiingia katika jumba lake bila walinzi wake kumuona. Aliingia hadi katika kile chumba cha mwanawe, kisha mfalme huyo akazinduka usingizini.
Asubuhi kulipokucha, mfalme akapewa habari kuwa mwanawe amekutwa amekatwa kichwa chumbani mwake.
Nikahisi kwamba kisa hicho kinalingana kidogo na mkasa ule uliotokea wa kulipa kisasi kwa mtu aliyekufa kwa kuonewa.
Mfalme hakuchukua hatua dhidi ya mwanawe, na afisa magereza hakuchukua hatua dhidi ya wahalifu waliomuua Thomas, nikajiambia.
Nikiwa katika mawazo hayo, Sajin Meja Ibrahim aliingia ofisini kwangu.
Alikuwa ameshika karatasi mkononi. Nikamkodolea macho ya shauku.
“Afande, matokeo yamenishitua,” akaniambia huku akiketi kwenye kiti.
“Umepata matokeo gani?”
“Hizi alama za dole gumba zinalingana. Alama za dole la marehemu na alama zilizopo kwenye zile karatasi ni moja!”
Nikawa namtazama huku nikitoa tabasamu la fadhaa.
Akaendelea kuniambia:
“Yule mtu anaonekana amekufa muda mrefu, sasa inakuwaje alama zake za vidole zilingane kwenye zile karatasi ambazo zilipachikwa kwa wale watu walionyongwa juzi juzi tu?”
Nikabetua mabega yangu huku nikiendelea kutoa lile tabasamu.
“Sijui. Labda nikwambie tu kwamba bado tuko kwenye uchunguzi.”
“Halafu dole gumba moja la marehemu lilikuwa na rangi mbichi ya bluu. Inaonekana ndiyo ile iliyoko kwenye ile alama…”
“Ile rangi tumeiona.”
“Haya mambo yanatisha, Afande.”
“Ukweli ni kuwa yanatisha, lakini mbivu na mbichi zitajulikana tu.”
Akanipa ile karatasi aliyokuwa ameishika. Nikaisoma. Ilikuwa ndiyo ameniandikia matokeo aliyokuwa amenieleza.
“Wewe unadhani nini kimetokea?” nikamuuliza ili nipate mawazo yake.
Sajin Meja Ibrahim akatikisa kichwa.
“Kwa kweli siwezi kujua, lakini ninajua katika kazi hizi za upelelezi wakati mwingine unakutana na matukio ya aina hii. Yanaweza kukukatisha tamaa, lakini polisi ni taasisi kubwa.”
“Una maana gani, Sajin Meja?” nikamuuliza kivivu.
“Nina maana kwamba uchunguzi unaweza kuja kubainisha kila kitu. Nakumbuka kulikuwa na kesi moja ambapo mashahidi wa upande wa mashitaka walikuwa wanauawa. Waliuawa mashahidi watano kwa nyakati tofauti. Kesi hiyo iliyumba sana. Tulikuwa tunamshuku mshitakiwa kwamba alikuwa anawapoteza mashahidi.”
“Na ni lazima itakuwa ni hivyo. Kama si mshitakiwa mwenyewe, basi alikuwa akituma watu. Bila shaka alikuwa mtu mwenye uwezo.”
“Ni kinyume na unavyofikiri. Alikuwa mkulima maskini ambaye hakuwa na uwezo wala mbinu zozote za kuua mashahidi, halafu wakati wote wa kesi yake alikuwa mikononi mwa polisi.”
“Kama si yeye mwenyewe, walikuwa rafiki zake au ndugu zake waliokuwa wanaua.”
“Fikiria mtu wa kijijini. Kilivyo, marafiki zake watakuwa watu wa kijijini. Uwezo wao ni kama yeye tu.”
“Sasa alikuwa ni nani aliyewaua hao mashahidi?”
“Nakumbuka ilikuwa ni Mbeya. Uchunguzi wake ulitukatisha tamaa na kututia hofu. Miongoni mwa mashahidi waliouawa walikuwa polisi. Polisi walikuwa wakiogopa kushughulikia ile kesi. Lakini jitihada za mpelelezi mmoja zilikuja kuzaa matunda.”
“Zilizaa matunda gani?”
“Kumbe wale mashahidi walikuwa wanauawa kwa kemikali ya sumu waliyoishika na kuivuta kwa njia ya hewa wakati polisi walipomkamata mtuhumiwa, ambaye alikutwa na kemikali hizo ambazo mwenyewe alidai hajui zilikuwa za nini wakati zilikutwa nyumbani kwake.”
“Waliuawa kwa kemikali za sumu? Kivipi?”
“Polisi walipomkamata waliita mashahidi, mwenyekiti wa kijiji na baadhi ya watu. Wakati polisi wakifungua zile chupa za kemikali ya sumu, walikuwa wanavuta hewa na pia walizishika zile chupa kwa mikono mitupu. Uchunguzi wa madaktari ndiyo uliokuja kugundua hilo baada ya polisi kusumbuka sana.”
“Waligundua kwamba hao watu waliuawa kwa sumu?”
“Ndiyo. Ile sumu ilikuwa ikiwaathiri kidogo kidogo bila wenyewe kujua. Baada ya muda tu wakaanza kufa mmoja baada ya mwingine.”
“Loh! Sasa ikawaje kwa yule mshitakiwa?”
“Yule aliachiwa na mahakama baada ya mashahidi wote kufa. Hakukuwa na ushahidi wa kumtia hatiani.”
“Ni kweli tatizo kama hilo linaweza kutokea na kusumbua watu, lakini kama ulivyosema hatimaye ilifahamika kwamba mashahidi hao waliuawa na sumu.”
“Ndiyo hivyo. Katika kazi zetu hizi matukio ya aina hiyo ni ya kawaida. Kinachohitajika ni umakini na moyo wa kujituma. Unapokata tamaa haraka, utakuwa umeshindwa.”
“Ni kweli, Sajin Meja. Nakubaliana na ushauri wako. Asante sana.”
Mara tu Sajin Meja Ibrahim alipotoka ofisini kwangu, nilimpigia simu afisa upelelezi ili nimjulishe matokeo ya uchunguzi wa alama za dole la Thomas.
“Hello Inspekta Fadhil, kuna tatizo lolote huko?” sauti ya afisa upelelezi ikasikika kwenye simu.
“Nilikuwa nataka kukufahamisha kuhusu uchunguzi wa alama za dole la marehemu Thomas.”
“Nifahamishe.”
“Uchunguzi umeonesha kuwa alama za dole la Thomas ndizo zilizoko katika zile karatasi.”
Afisa upelelezi akagutuka.
“Unasema kweli?”
“Ni kweli tupu, Afande. Nimeshangaa sana.”
“Maana yake ni kwamba marehemu ndiye aliyeweka dole lake kwenye zile karatasi?”
“Ndivyo inavyoonekana.”
“Na kwa maana hiyo ndiye aliyewanyonga wale wafungwa?”
Afisa upelelezi alikuwa amenitega.
“Si hivyo, lakini ndivyo ambavyo uchunguzi wa alama za dole ulivyoonesha.”
“Tutakuja kulizungumzia hilo. Kwa sasa mimi niko Gereza la Maweni pamoja na maafisa wangu wawili. Tunataka kuchunguza kuhusu nyendo za yule afisa mstaafu.”
“Unadhani unaweza kugundua kitu kingine zaidi?”
“Tunataka kujua kama kulikuwa na wafungwa wengine aliowaachia kama wale na mambo mengine. Hili ni agizo limetoka makao makuu. Pia nataka kukufahamisha kuwa yule askari mstaafu tuliyezungumza naye katika hospitali ya Muheza ameshafariki.”
“Oh, alifariki lini?”
“Nimeambiwa alifariki jana usiku.”
“Sawa. Tutaonana utakapotoka huko.”
“Okey.”
Nikakata simu na kuiachia akili yangu kutafakari zaidi kuhusu uchunguzi uliokuwa mbele yangu.
Baada ya muda kidogo nikapata wazo la kuendelea kulipekua jalada la uchunguzi wa kuuawa kwa Thomas Christopher.
Nililipekua kutafuta watu ambao walitajwa kama mashahidi waliotoa maelezo polisi kuhusiana na kuuawa kwa Thomas Christopher.
Nikapata jina la mtu mmoja aliyeitwa Mustafa Abuu. Kwa mujibu wa jalada hilo, Mustafa alikuwa dereva wa kina Thomas. Nikahisi kwamba endapo nitampata yeye, ninaweza kupata picha halisi ya Thomas Christopher.
Anuani yake ilikuwa imeandikwa, ingawa namba ya simu yake haikuwepo. Wakati akitoa maelezo yake polisi, alikuwa mkazi wa Makorora, nyumba namba 222 karibu na soko la Makorora.
Baada ya kuipata anuani ile, nililiweka jalada hilo juu ya meza yangu na nikatoka ofisini. Nilijipakia kwenye gari na kuelekea Makorora.
Nilipofika katika soko la Makorora, nikaanza kusoma namba za nyumba. Nikaugundua mtaa uliokuwa na nyumba namba 222.
Ulikuwa nyuma ya soko. Ilikuwa nyumba ya kizamani iliyojengwa kwa miti na udongo, lakini baadhi ya kuta zilikuwa zimeanza kujengwa kwa matofali.
Niliegesha gari mbele ya nyumba hiyo, nikashuka na kwenda kwenye mlango wa nyumba hiyo.
Baada ya kubisha hodi, alitoka mama mmoja ambaye nilimsalimia na kumuuliza kama Mustafa Abuu alikuwa akiishi pale.
“Ndiyo, anaishi hapa,” akaniambia.
“Ninaomba kuonana naye.”
Yule mama akanitazama usoni mara moja, kisha akaniambia:
“Karibu, pita ndani.”
Alitangulia kurudi ndani na mimi nikamfuata. Aliingia katika chumba kimoja, nikamsikia akizungumza na mtu, kisha akatoka katika chumba hicho na kuniambia:
“Pita.”
Nikaingia katika kile chumba. Mwanga uliokuwemo ulikuwa hafifu sana kwa sababu chumba chenyewe hakikuwa na dirisha. Ukuta wake wa upande wa nje ulijengwa kwa matofali na sehemu ya dirisha ilizibwa kwa kukandikwa udongo.
Niliona mtu mmoja aliyekuwa amekaa kwenye kitanda. Alikuwa mzee. Kichwa chake kilikuwa na mvi tupu. Alikuwa amevaa shuka aliyojifunga kiunoni. Kifua chake kilikuwa wazi.
“Karibu,” akaniambia kwa sauti ya kutetemeka huku akinitazama kwa macho ya shauku na udadisi.
“Shikamoo mzee,” nikamwamkia.
“Marahaba. Habari yako?”
“Nzuri.”
“Karibu kiti.”
Kulikuwa na kiti cha marimba kilichokuwa kando ya kitanda.
Nikakaa.
“Nilikuwa namhitaji Mustafa Abuu,” nikamwambia.
“Ndiye mimi,” akaniambia.
Kidogo niligutuka kwani nilitarajia kukutana na kijana mwenzangu au mtu aliyenizidi kidogo, lakini yule alikuwa kama babu yangu.
“Unatoka wapi?” akaniuliza.
“Mimi ni askari wa upelelezi. Natokea kituo cha polisi cha Chumbageni.”
Sikuona hata haja ya kumuonesha kitambulisho changu kwani sikuwa na uhakika kama macho yake yangeweza kukisoma.
Mzee alishituka kidogo.
“Ulikuwa na tatizo gani?” akaniuliza.
“Ni tatizo kwa upande wangu, si kwa upande wako. Ninahitaji msaada kutoka kwako. Unamfahamu Thomas Christopher?”
Mzee akanitazama huku akipepesa macho yake.
“Huyo mtu ninayemuuliza alishafariki. Nilitaka kujua kama unamfahamu,” nikamwambia.
“Wewe unazungumzia yule kijana aliyeuawa kwa Unyeke, sijui mwaka jana au mwaka juzi. Sina kumbukumbu nzuri…”
Niliposikia lile jina Unyeke nikamwambia:
“Nadhani ni huyo huyo.”