Balozi Akutwa Amefariki Dunia Nje ya Hoteli Paris – Global Publishers

Balozi wa Afrika Kusini nchini Ufaransa, Nathi Mthethwa (58) pia aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Polisi pamoja na Waziri wa Sanaa na Utamaduni

Balozi wa Afrika Kusini nchini Ufaransa, Nathi Mthethwa (58), amekutwa akiwa amefariki dunia karibu na Hoteli ya Kifahari ya Hyatt Regency jijini Paris, Ufaransa, maafisa wa Ufaransa wamethibitisha.

Kwa mujibu wa ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Paris, Mthethwa aliripotiwa kupotea Jumatatu jioni na mkewe baada ya kutuma ujumbe uliotajwa kuwa ‘wa kutia wasiwasi’.

Ilibainika kuwa alikuwa amechukua chumba kwenye ghorofa ya 22 ya hoteli hiyo, ambapo dirisha lilionekana limefunguliwa kwa nguvu.

Hadi sasa, mazingira ya kifo chake hayajafahamika, na uchunguzi rasmi umeanzishwa. Mwendesha mashtaka wa zamu alithibitisha kufika eneo la tukio kwa uchunguzi wa awali.

Mthethwa alikuwa mwanasiasa wa muda mrefu ndani ya chama tawala cha African National Congress (ANC), na aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Polisi pamoja na Waziri wa Sanaa na Utamaduni kabla ya kuteuliwa kuwa balozi jijini Paris mnamo Desemba, 2023.

Pia alikuwa mshirika wa karibu wa Rais wa Zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, na alitajwa katika uchunguzi wa ‘state capture’ uliolenga madai ya ufisadi wa juu serikalini wakati wa utawala wa Zuma.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Ronald Lamola, alitoa salamu za rambirambi akimueleza Mthethwa kama ‘mtumishi mashuhuri wa taifa’.

“Hakika kifo chake siyo hasara kwa taifa pekee, bali pia ni pengo kubwa katika jamii ya kidiplomasia ya kimataifa,” alisema Lamola.

Serikali ya Ufaransa imeendelea na uchunguzi, huku taifa la Afrika Kusini likibaki na maswali mengi kuhusu kifo cha ghafla cha mmoja wa wanasiasa wake wenye ushawishi mkubwa.