Dar es Salaam. Bei za mafuta ya petroli na dizeli zitakazotumika Oktoba mwaka huu nchini zimeendelea kupungua kwa kiwango tofauti ikilinganishwa na zilizokuwepo mwezi uliotangulia, huku upande wa mafuta ya taa ukiendelea kusalia vilevile.
Bei hizi zinapungua nchini wakati ambao kumekuwa na ongezeko katika soko la dunia kwa asilimia 2.80 kwa mafuta ya petroli, asilimia 3.65 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 3.57 kwa mafuta ya taa.
Pia taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) inaonyesha kuwa licha ya bei kikomo kupanda katika soko la dunia, gharama za kuagiza mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam zimepungua kwa wastani wa asilimia 1.95 kwa mafuta ya petroli.
Kwa upande wa dizeli zimeongezeka kwa asilimia 2.39 na hakuna mabadiliko kwa mafuta ya taa. Katika Bandari ya Tanga zimeongezeka kwa asilimia 6.38 kwa mafuta ya petroli na dizeli na katika Bandari ya Mtwara zimeongezeka kwa asilimia 0.49 kwa mafuta ya petroli na hakuna mabadiliko kwa mafuta ya dizeli.
Hali hiyo inafanya bei ya jumla sasa lita moja ya mafuta inayopitia katika bandari ya Dar es Salaam kuuzwa kwa Sh2,720 kutoka Sh2,807 iliyotumika Septemba mwaka huu, dizeli itanunuliwa kwa Sh2,704 kutoka Sh2,754 iliyokuwapo Septemba mwaka huu
Hata hivyo, kwa watumiaji wa mafuta ya taa yanayopitia katika bandari hiyo watalazimika kuendelea kutumia bei ya Sh2,774 iliyokuwapo Septemba mwaka huu.
Kwa wanunuaji wa rejareja kwa mafuta yanayopita Bandari ya Tanga sasa watanunua petroli lita moja kwa Sh2,813 kutoka Sh2,868 iliyokuwapo Septemba mwaka huu, dizeli Sh2,766 kutoka Sh2,816 huku mafuta ya taa yakisalia na bei ya Sh2,835 iliyokuwapo mwezi uliotangulia.
Kwa Bandari ya Mtwara, petroli sasa itanunuliwa Sh2,844 kutoka Sh2,899, dizeli Sh2,797 kutoka Sh2,847 na mafuta ya taa yakisalia kuwa Sh2,866 iliyotumika Septemba mwaka huu.
Taarifa hii iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Ewura, Dk James Mwainyekule imeeleza kuwa gharama za kubadilisha fedha za kigeni zimepungua kwa asilimia 5.10.
Kufuatia hilo, Ewura imeendelea kuvielekeza vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionyesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.
“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja,” imeeleza taarifa hiyo.
Kadhalika mamlaka hiyo imewataka wauzaji wa mafuta, bidhaa za mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP), na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.