Biashara ya Mitumba Yadorora Dar es Salaam

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

Baadhi ya wafanyabiashara wa nguo za mitumba jijini Dar es Salaam wamesema biashara hiyo imekuwa ngumu zaidi katika kipindi cha hivi karibuni, hali inayosababisha kushuka kwa mauzo na kuathiri kipato cha familia nyingi zinazotegemea sekta hiyo.

Wakizungumza na Michuzi Blog, wafanyabiashara hao wamesema changamoto kubwa inayowakabili ni kupungua kwa mizigo mipya inayoingia sokoni na hivyo bidhaa wanazopata kushindwa kukidhi mahitaji ya wateja.

Aidha, uchakavu wa miundombinu ya masoko umeendelea kuongeza ugumu wa kufanya biashara hiyo.

Katika Soko la Karume, linalotambulika kama kitovu cha biashara ya mitumba jijini, wafanyabiashara wanasema idadi ya wateja imepungua tofauti na ilivyokuwa miezi iliyopita.

“Tulizoea kuona wateja kutoka maeneo mbalimbali ya jiji wakifika kwa wingi, lakini sasa hali siyo ile tuliyoizoea. Biashara imepungua na inakuwa ngumu kuendesha familia,” amesema Debora Jailos ambaye ni mmoja wa wafanyabiasha wa soko la Karume.

Hali kama hiyo imeripotiwa pia katika Soko la Mbezi Mwisho, ambako wafanyabiashara wamesema upungufu wa mizigo mipya. Wamesisitiza kuwa serikali inapaswa kutazama kwa makini mazingira ya biashara hiyo kwa kuwa inagusa maisha ya wananchi wa kipato cha chini wanaotegemea nguo za bei nafuu.

Kwa upande wa Soko la Big Brother Urafiki, wafanyabiashara wamesema changamoto kubwa ni miundombinu chakavu ya masoko ikiwemo ukosefu wa maeneo bora ya kuhifadhi bidhaa, jambo linalosababisha nguo nyingi kuharibika kabla ya kufika kwa wateja.

Wafanyabiashara wote kwa pamoja wameiomba serikali kusimamia kwa karibu zaidi uingizaji wa nguo za mitumba nchini, kuboresha miundombinu ya masoko na pia kuangalia kodi na ushuru unaotozwa ili kuondoa vikwazo vinavyowafanya washindwe kushindana sokoni.

Ikumbukwe kuwa biashara ya nguo za mitumba nchini Tanzania imeendelea kukua kwa kasi kwa miaka ya hivi karibuni, kutokana na mahitaji makubwa ya nguo za bei nafuu na upatikanaji wake kutoka nje ya nchi. Hata hivyo, changamoto zinazojitokeza sasa zinatishia ustawi wa sekta hiyo ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa ajira.