De Ruck, Chamou waiweka Simba kileleni baada ya siku 244

MABEKI wa kati wa Simba, Rushine De Ruck na Karabou Chamou wameibeba timu hiyo hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kupita takribani siku 244 kufuatia kupachika mabao dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Mara ya mwisho Simba kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ilikuwa Februari 5, 2025, siku ambayo ilishushwa na Yanga kufuatia mabingwa hao watetezi kuichapa KenGold mabao 6-1. Zimepita takribani siku 244 kurejea tena nafasi hiyo.

Tangu hapo, Yanga imeendelea kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi hadi kubeba ubingwa msimu uliopita 2024-2025.

Mabao ya Chamou na De Reuk sambamba na Seleman Mwalimu, yamechangia kuifanya Simba kuibuka na ushindi wa pili mfululizo, baada ya mechi ya kwanza Wekundu wa Msimbazi kuitandika Fountain Gate ya mabao 3-0 kama ilivyokuwa leo Oktoba 1, 2025 uwanjani hapo dhidi ya Namungo. 

Katika mechi hiyo iliyoanza saa 2:15 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, Simba ilipata bao la kwanza dakika ya 42 baada ya Chamou kumalizia kwa kichwa kona iliyochongwa na Joshua Mutale. 

Ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, Simba ilionekana kuendelea kuwa na changamoto katika kujenga mshambulizi yake kutokea nyuma kama ilivyokuwa katika mechi ya kwanza ya msimu kwenye ligi. 

Licha ya kuanza kwa Steven Mukwala kama mshambuliaji kinara badala ya Jonathan Sowah, Simba haikuonekana kuwa na utulivu eneo hilo. 

Wakati kipindi cha pili kinataka kuanza, kocha msaidizi wa Simba ambaye ndiye anaiongoza timu hiyo kwa sasa baada ya kuondoka Fadlu Davids, Seleman Matola alifanya mabadiliko kwa kumtoa Ellie Mpanzu ambaye hakuonekana kuwa na makali katika kipindi cha kwanza na kuingia Neo Maema ambaye dakika sita baadaye alichangia upatikanaji wa bao la pili. 

Maema alichonga faulo ambayo ilimaliziwa na De Ruck ambaye alifunga katika mechi yake ya pili mfululizo katika ligi, ikumbukwe kuwa beki huyo ndiye alifunga bao la kwanza la msimu kwa Wekundu wa Msimbazi katika mechi iliyopita dhidi ya Fountain Gate. 

Kuwa mbele kwa mabao hayo, kulimfanya Matola kufanya mabadiliko zaidi katika kipindi hicho cha pili ikiwamo kuwatoa, Morice Abraham, Mukwala na Mutale huku nafasi zao wakiingia, Seleman Mwalimu, Jean Charles Ahoua na Kibu Denis.

Mabadiliko hayo yaliifanya Simba kuendelea kumiliki mechi huku ikitengeneza nafasi mfululizo kabla ya Mwalimu kufunga bao lake la kwanza kwenye ligi kufuatia kumlamba chenga beki wa Namungo, Hussein Kazi na kuachia mkwaju ambao ulimshinda kipa Jonathan Nahimana. 

Kwa upande wa Namungo, licha ya kuwatoa Hassan Kabunda na Abdallah Mfuko aliyekuwa na kadi ya njano na kuingia Herbert Lukindo na Pius Buswita, mabadiliko hayo hayakutosha kuwanusuru na kipigo hicho. 

Matokeo hayo, yameifanya Simba kuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi sita pamoja na mabao sita, huo ni ushindi wa sita kati ya mechi saba kwa Simba ikiwa nyumbani dhidi ya Namungo katika ligi, mechi moja waliwahi kutoa sare.

Kikosi cha Simba: Yakoub Suleiman, Shomari Kapombe, Anthony Mlingo, Rushine De Ruck, Karabou Chamou, Kante Alasana, Yusuph Kagoma, Joshua Mutale, Elie Mpanzu, Steven Mukwala na Morice Abraham. 

Wachezaji wa akiba walikuwa Jonathan Sowah, Jean Ahoua, Naby Camara, Charles Semfuko, David Kameta, Kibu Denis (38), Hussen Abel, Wilson Nagu, Neo Maema na Seleman Mwalimu.

Kikosi cha Namungo: Jonathan Nahimana, Jacob Masawe, Ali Ahmed, Daniel Amoah, Abdallah Mfuko, Faria Ondongo, Hassan Kabunda, Heritier Makambo, Geofrey Julius, Abdulkarim Kiswanya, na Bakari Hussein. 

Wachezaji wa akiba Pius Buswita, Rodgers Gabriel, Ayoub Semtawa, Herbert Lukindo, Abubakar Mfaume, Abdallah Denis, Fabrice Ngoy, Azizi Saidi, Mussa Mussa na Frank Methew.