Dk Mwinyi: Ahadi tulizotoa tumezitimiza, tunaomba ridhaa tena

Unguja. Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi amesema ahadi walizotoa wamezitimiza lakini wamerudi kuomba kura ili wafanye makubwa zaidi.

Amewasihi vijana wajipange kadri iwezekanavyo kupata ajira za kudumu na kumaliza changamoto hiyo.

Ametoa kauli hiyo leo Oktoba mosi, katika viwanja vya Nyarugusu Pangawe wakati Akizungumza na makundi ya wajasiriamali na wananchi wa Jimbo hilo ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zake za kusaka kura kuingia madarakani kwa kipindi cha pili.

“Ndugu zangu aahadi tulizozitoa wakati tunaomba kura mwaka 2020, tumezitumiza, kwahiyo tumekuja kuomba kura tena ili tufanye makubwa zaidi,” amesema.

Dk Mwinyi ametaja maeneo ambayo wametekeleza miradi mikubwa ni katika sekta za afya kwa ujenzi wa hospitali za kisasa, elimu kwa ujenzi wa Shule za ghorofa na miundombinu ya barabara na viwanja vya Michezo.

Amewahakikishia wananchi wa Jimbo hilo kuwa licha ya kuwapo changamoto kadhaa za afya, barabara na Shule akiwaahidi kuwajengea shule ya ghorofa na barabara ambapo tayari mipango hiyo inaendelea.

“Hivi karibuni tumesaini mktaba wa kujenga shule 29 za ghorofa, tutaangalia kujenga hapa shule moja, na kuna kituo cha afya Kwarara kinajengwa,” amesema.

Kuhusu ajira, Dk Mwinyi amesema katika awamu ijayo ya uongozi wamejipanga kutoa ajira kwa vijana ambapo watatoa ajira hizo serikalini, viwandani na kuwawezesha kiuchumi ili wajiajiri.

“Vijana tujipange kadri iwezekanavyo tuwape ajira za kudumu, mipango tunayo na tayari imeshaanza, kwahiyo tunaomba turejeshwe madarakani tuweze kuzitekeleza mipango hiyo,” amesema Dk Mwinyi.

Ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi siku ikifika kupiga kura kwake na Chama Cha Mapinduzi.

“Hamasa pekee haitoshi kushinda uchaguzi, hivyo tunatakiwa kujitokeza kwa wingi siku ya Oktoba 29 kuchagua chama chetu ili tushinde kwa kishindo na kuwakosesha wapinzani kisingizio cha kuibiwa kura,” amesema.

Awali Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa amesema chama hicho ndio kimeleta wagombea wenye sifa, na kuwataka wananchi wasifanye kosa siku ya kupiga kura.

“Ukichagua Dk Mwinyi umechagua maendeleo, kwahiyo siku ikifika tusifanye makosa tumchague ili kupata Maendeleo,” amesema.