Dorcas wa Chaumma anavyosaka kura kaya kwa kaya

Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Dorcas Francis jana Jumanne Septemba 30, 2025 ameendeleza na kampeni zake kwa mtindo wa ziara za kaya kwa kaya na kutembelea maeneo yenye mikusanyiko ya wananchi, akiahidi aina mpya ya uongozi utakaowashirikisha wakazi wa jimbo hilo moja kwa moja katika uamuzi wa maendeleo.

Katika ziara yake iliyoishia kwa mkutano sokoni Bunju B, Dorcas ametangaza kuwa kauli mbiu yake ya kampeni ni uwakilishi shirikishi, akieleza kuwa lengo lake ni kubadili mtazamo wa siasa za kibunge kutoka ule wa kiutawala kwenda kwenye mtazamo wa ushirikiano na uwajibikaji wa moja kwa moja kwa wananchi.

“Nitakuwa mwakilishi wenu, siyo mtawala. Nitahakikisha kauli mbiu yangu ya uwakilishi shirikishi inatekelezwa kwa vitendo kwa kuunda kamati za kisekta zitakazowahusisha moja kwa moja, nanyi mtakuwa sehemu ya uongozi, si watazamaji,” amesema.

Dorcas amesisitiza kuwa mpango wake utagusa sekta nyeti zinazogusa maisha ya kila siku ya wakazi wa Kawe, ikiwamo uvuvi, biashara ndogondogo, afya, elimu na miundombinu.

Ameweka bayana kuwa matatizo ya wananchi hayatabaki kwenye makaratasi, bali yatapewa majibu ya kweli kwa ushirikiano wa karibu kati ya jamii na viongozi wao.

Akijikita zaidi katika masuala ya uchumi, Dorcas ameahidi kuweka mkazo kwenye elimu ya ujasiriamali kwa vijana na wanawake kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali, akieleza kuwa lengo lake ni kuhakikisha wakazi wa Kawe wanajengewa uwezo wa kumiliki na kuendesha uchumi wao wenyewe.

“Tutatoa elimu ya ujasiriamali na fursa za mikopo midogo kupitia taasisi zinazoshirikiana nasi, ili vijana na akinamama wawe na uwezo wa kujitegemea kiuchumi. Kawe inahitaji wananchi wake wawe wamiliki wa uchumi, si watazamaji wa ukuaji wake,” amesema.

Dorcas hakusita kuwataka wakazi wa Kawe kuepuka kupewa matumaini hewa ya kisiasa, akisisitiza kuwa yeye na chama chake wanatoa ahadi zenye mashiko na zinazoweza kutekelezeka.

“Situmii ahadi hewa za majukwaani, ninasimama na ahadi za mambo yanayotekelezeka jimboni hapa. Nipeni mimi Dorcas na mchague madiwani wa Chaumma pamoja na rais wa Chaumma, ili tuwaletee mageuzi makubwa kwa vitendo,” amesema.

Ziara hiyo pia ilimpa nafasi mgombea udiwani wa kata ya Bunju kupitia chama hicho, anayejulikana kwa jina maarufu la Ajuwaye, kuwasilisha sera zake na kuomba kura kutoka kwa wananchi.

Ajuwaye alitumia jukwaa hilo kueleza namna alivyo mzaliwa na mkazi wa Bunju, akisisitiza kuwa anaelewa vyema changamoto za eneo hilo.

“Mimi ni mtoto wa Bunju hii, nimekulia hapa, nimesoma hapa na ninaifahamu Bunju vyema. Nipeni udiwani nikafanye kazi ya kweli kwa ajili yenu,” amesema Ajuwaye.

Ajuwaye ambaye amewahi kujishughulisha na kazi ya bodaboda katika eneo hilo kwa miaka mingi, ameelezea uzoefu wake kwamba ndiyo unaompatia nafasi ya kipekee ya kuelewa changamoto zinazowakabili vijana wa bodaboda na mama lishe.

“Nimekuwa mwendesha bodaboda hapa kwa muda mrefu, najua changamoto za bodaboda na mama lishe. Nipeni kura zenu nikazitatue kwa vitendo,” amesema.

Kampeni za Dorcas na timu yake zimeonekana kuchukua mwelekeo tofauti na ule wa kisiasa wa kawaida, ambao mikutano mikubwa ya hadhara ndiyo imekuwa nguzo ya uhamasishaji. Badala yake, mgombea huyo wa Chaumma ameweka mkazo kwenye mikakati ya kuonana uso kwa uso na wananchi kwenye kaya zao akiwagawia vipeperushi vinavyofafanua sera zake na kuzungumza nao kwa ukaribu.