Tabora. Mgombea urais kupitia tiketi ya chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassani Doyo, ameahidi endapo atachaguliwa kuongoza serikali, mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu bila riba, itaongezwa hadi kufikia asilimia 40 ili ichochee ukuaji wa uchumi kwa wananchi.
Akihutubia leo Jumatano, Oktoba Mosi 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Soko la Kachoma, Kata ya Chem Chem Manispaa ya Tabora, Doyo amesema sera hiyo inalenga kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na kupunguza utegemezi kwa serikali.
“Nichagueni mpate maendeleo makubwa hasa katika uchumi wa mtu mmoja mmoja. Kila mtu akiwa na fedha za kutosha, mzigo wa serikali kugharamia mahitaji mengi utapungua, hivyo itaweza kuelekeza nguvu kwenye miradi mikubwa ya kitaifa,” amesema.
Doyo amebainisha kuwa changamoto kubwa inayokwamisha makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ni ukosefu wa mitaji ya kutosha licha ya wao kuwa nguvu kazi na nguzo muhimu za maendeleo.
“Maendeleo yataongezeka haraka ikiwa makundi haya yatashirikiana katika shughuli za biashara. Hata wale wanaofanya biashara ndogo ndogo wana nafasi kubwa ya kukuza uchumi endapo watapewa mtaji wa kutosha,” ameongeza.
Mbali na suala la mikopo, Doyo ameahidi pia kwamba serikali yake itahakikisha huduma za afya, ikiwemo uzazi, zinatolewa bure kwa wanawake wakati wa ujauzito na kujifungua, pamoja na huduma nyingine za afya.
“Mimi nikiingia madarakani nahakikisha huduma zote za afya ni bure. Nchi hii ina rasilimali nyingi zinazoweza kugharamia mahitaji yote ya wananchi bila mzigo wa ziada,” amesema Doyo.
Aisha Kasala, mkazi wa Kata ya Chem Chem, amesema sera za mgombea huyo ni nzuri na akipewa ridhaa ya kuongoza nchi, anatamani azitekeleze kwa vitendo.
“Sisi tunahitaji huduma bora za kijamii ikiwemo afya na elimu bora kwa watoto wetu. Ingependeza sana kama wanawake wasingelipa fedha wakati wa kujifungua,” amesema Aisha.
Naye Haji Suleimani, mkazi wa Manispaa ya Tabora, amesema ongezeko la mikopo kutoka asilimia 10 hadi asilimia 40 litakuwa ni hatua kubwa kwa wajasiriamali.
“Tunahitaji mitaji ili tufanye biashara kwa ufanisi na kuongeza mzunguko wa fedha. Tabora sasa inakua kwa kasi, na kwa mujibu wa sensa ya 2022, tuna zaidi ya watu milioni tatu. Hii si idadi ndogo, na ikitumika vyema inaweza kuleta mageuzi ya kiuchumi,” amesema.