Dar es Salaam. Licha ya Mahakama ya Kijeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kutoa hukumu ya kifo dhidi ya Rais wa zamani, Joseph Kabila, bado utekelezaji wake umeonekana kuwa mgumu kwa kuwa hadi sasa haijafahamika alipo au anaishi wapi.
Kabila, aliyeongoza DRC kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, tangu afunguliwe kesi hiyo Julai 25, 2025 kwenye Mahakama ya Kijeshi, hakuwahi kuhudhuria kesi hiyo wala kuwakilishwa hadi ilipotolewa hukumu juzi, Jumanne ya Septemba 29, 2025.
Pia, mahakama iliamuru Kabila kulipa fidia ya Dola bilioni 29 kwa Serikali ya DRC, Dola bilioni mbili kwa jimbo la Kivu Kaskazini na nyingine Dola bilioni mbili kwa jimbo la Kivu Kusini, kama fidia kwa madhara ya kijamii, kiuchumi na kimazingira yaliyosababishwa na machafuko.
Hukumu hiyo haijampa nafasi Kabila ya kuipinga na zaidi anachoweza kufanya ni kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani ya Juu kwa misingi ya madai ya dosari za kisheria pekee, na si kwa ajili ya kupitia upya hoja za msingi za kesi yenyewe.
Ugumu wa utekelezaji wa hukumu hiyo, ikiwamo kulipa fidia, ni kutokana na kutojulikana Kabila anaishi nchi gani kwa sasa.
Taarifa za hivi karibuni zilionesha kuwa Kabila aliishi kwa kipindi kirefu nchini Afrika Kusini tangu mwaka 2023, lakini Mei 2025 alionekana hadharani katika Jiji la Goma, linalodhibitiwa na waasi wa M23 mashariki mwa DRC, ambako alielekea kwa lengo la kuhimiza amani kupitia mkutano na viongozi wa dini.
Licha ya Mahakama ya Kijeshi ya DRC kutoa amri ya kukamatwa Kabila, bado mahakama hiyo haijaelekeza nani wa kuitekeleza amri hiyo, tofauti na ilivyo kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ambayo inaziomba nchi wanachama kumkamata muhusika, japokuwa hazilazimiki.
Ugumu wa utekelezaji wa amri ya ICC
Machi 17, 2023, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa hati za kukamatwa kwa Rais wa Russia, Vladimir Putin, kufuatia uchunguzi wa uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari.
Hata hivyo, utekelezaji wa amri hiyo umeshindikana mpaka sasa kwa kuwa kukamatwa kwa Putin kunategemea utashi wa nchi atakayotembelea, na hivi karibuni alikuwa Marekani na hakukamatwa.
Pia, ni hati ya kwanza kutolewa dhidi ya kiongozi wa nchi mwanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Novemba 21, 2024, ICC pia ilitoa hati ya kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu wa kivita wa kutumia njaa kama mbinu ya kivita, pamoja na uhalifu dhidi ya binadamu wa mauaji, mateso ya kisiasa na vitendo vingine visivyo vya kibinadamu wakati wa vita vya Gaza.
Pamoja na kwamba ni hati ya kwanza kutolewa dhidi ya kiongozi wa nchi ya kidemokrasia inayoungwa mkono na mataifa ya Magharibi kwa tuhuma za uhalifu wa kivita, utekelezaji wake bado umekuwa mgumu.
ICC pia ilitoa hati ya kukamatwa aliyekuwa Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, lakini kiongozi huyo alifanya ziara katika baadhi ya nchi ikiwamo Jordan na hakukamatwa na hati hiyo haijatekelezwa mpaka sasa.
Kabila alikutwa na hatia ya makosa mbalimbali, yakiwemo uhaini, uhalifu dhidi ya ubinadamu, mauaji, unyanyasaji wa kingono, mateso na uasi.
“Kwa kutumia Kifungu cha 7 cha Kanuni ya Adhabu ya Kijeshi, Mahakama imeamua kutoa adhabu moja tu, ambayo ni kali zaidi, nayo ni adhabu ya kifo,” alisema Luteni Jenerali Katalayi wakati akisoma hukumu hiyo.
Pia, Kabila alituhumiwa kushirikiana na kikundi cha waasi cha M23, linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, ambalo liliteka maeneo kadhaa ya mashariki mwa Congo mwanzoni mwa mwaka 2025.
Hata hivyo, Rwanda ilikanusha kutoa msaada wa kijeshi kwa M23, lakini wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema jeshi la Rwanda lilikuwa na mchango “mkubwa” katika mashambulizi ya kundi hilo.
Hukumu hiyo imetolewa baada ya Seneti ya DRC kupiga kura Mei kufuta kinga ya Kabila dhidi ya mashtaka, hatua ambayo Rais huyo wa zamani aliilaani kama ya kidikteta.
Nchi hiyo pia mwaka jana iliondoa marufuku ya muda mrefu dhidi ya adhabu ya kifo, ingawa hakuna hukumu yoyote ya kifo iliyotekelezwa hadi sasa.
Mwendesha mashtaka wa kijeshi, Jenerali Lucien Rene Likulia, alitoa hoja mahakamani ya kutaka Kabila ahukumiwe kifo.
Likulia alimshutumu kiongozi huyo wa zamani kwa kupanga njama ya kumpindua Rais Felix Tshisekedi, huku mashtaka mengine dhidi yake yakiwemo mauaji, mateso na ubakaji, yakihusishwa na kundi la M23.
Joseph Kabila, aliyechukua madaraka nchini Congo akiwa na umri wa miaka 29 baada ya baba yake, Laurent Kabila, kuuawa na mlinzi wake binafsi, aliongoza nchi hiyo kwa miaka 18 akiwa kiongozi wa pili kukaa madarakani muda mrefu.
Kabla ya kuchukua madaraka ya nchi, alikuwa kiongozi ndani ya jeshi la waasi la muungano wa waasi wa ADFL (Alliance of Democratic Forces for the Liberation of Congo-Zaire), akitambulika kwa jina la Kadogo kwa maana ya askari mdogo kiumri.
Baadaye alipata mafunzo zaidi ya kijeshi nje ya nchi kabla ya kuchukua nafasi ya juu katika Jeshi la Taifa la Congo (FARDC).
Kabila, ambaye ni pacha waliozaliwa Juni 4, 1971 akiwa na mwenzake ambaye ni dada yake Jaynet Kabila, baada ya kuchukua madaraka aliongoza DRC kwa mafanikio, ikiwamo Serikali yake kushirikisha wapinzani.
Alipigana kama sehemu ya majeshi ya waasi yaliyosaidia baba yake kumuondoa madarakani Rais Mobutu Sese Seko wa Zaire mwaka 1997. Laurent alichukua urais na akarejesha jina la zamani la nchi hiyo kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na alipelekwa China kwa mafunzo zaidi ya kijeshi.
Aliporejea, alikabidhiwa uongozi wa majeshi ya nchi akiwa na cheo cha Meja Jenerali.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.