Kiungo Fountain Gate afichua kinachowaangusha Ligi Kuu

KIUNGO mkabaji wa Fountain Gate, Abdallah Kulandana amesema licha ya kuanza vibaya msimu wakifungwa mechi zote tatu anaamini wana timu bora ila kinachowaangusha ni uchache wa wachezaji.

Fountain Gate ambayo imeanza msimu na wachezaji 14 imecheza mechi tatu na kuambulia vipigo zote ikianza na Mbeya City ikachapwa bao 1-0, Simba ikalala 3-0 na Mtibwa Sugar ilifungwa mabao 2-0.

Akizungumza na tovuti ya Mwanaspoti, Kulandana amesema ni kweli hawapo vizuri kwa mujibu wa matokeo wanayoyapata lakini wanaamini wao ni bora na watakuwa bora zaidi kwa mechi zijazo huku akiweka wazi kuwa wanaangushwa na idadi ndogo ya wachezaji.

“Tuna kikosi bora na cha ushindani lakini namba za wachezaji tuliopo ndio shida kubwa ambayo inatuangusha lakini tukikamilika tutakuwa na timu bora sana msimu huu tukitoa ushindani kwa wapinzani,” amesema na kuongeza:

“Unajua tumeanza msimu tukiwa pungufu lakini kwa ujumla tumeweza kuendana na ushindani japo tumefungwa, timu inacheza na wachezaji 11 ndani wawili benchi hatuwezi kucheza kwa nguvu kuepuka kuchoka tulikuwa tunacheza kwa akili.

“Kupoteza mechi tatu za mwanzo sio mwisho wa sisi kukubali kuwa hakuna kitu tunaweza kukifanya msimu huu tutafanya vizuri na tutakuwa miongoni mwa timu bora shindani.”

Mchezaji huyo alisema wanaamini uongozi wa timu wanapambana kuhakikisha wanakamilisha asajili zilizobaki hasa nyota ambao tayari wanafanya nao mazoezi pamoja ili kuweza kuisaidia timu hiyo kuwa na uwiano sawa na timu wanazoshindana nazo.

“Kuna wachezaji tunafanya nao mazoezi wapo vizuri na unaona watakuwa na mchango mkubwa kwa timu. Naamini hao pia wakiingizwa kwenye mfumo, basi uwiano wa ushindani ndani ya kikosi na kwa wapinzani utakuwa sawa.”

Msimu uliopita Fountain Gate ilimaliza nafasi ya 14 ikacheza mtoano kubaki Ligi Kuu.