Mayele atupia mbili Pyramids ikiiadhibu APR kwao

CHAMA la mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele, Pyramids FC limeanza na ushindi wa mabao 0-2 ugenini dhidi ya APR ya Rwanda yaliyofungwa na nyota huyo katika mechi ya kwanza ya raundi ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nyota huyo raia wa DR Congo, amefunga mabao yote mawili kipindi cha pili, akiisaidia timu hiyo kuanza vyema harakati za kutetea ubingwa wa michuano hiyo.

Timu hiyo ilikuwa ugenini jijini Kigali nchini Rwanda, ikiwa tayari ina mtaji wa mabao mawili. Kama itafuzu raundi ya pili itakutana na Insurance ya Ethiopia, iliyoitoa Mlandege ya Zanzibar.

Mayele alionyesha uwezo binafsi akiukokota mpira upande wa kulia; juhudi za mabeki wa APR kumkaba zilishindikana kwani aliachia shuti kali lililompita golikipa Pierre Ishimwe na kuandika bao la kwanza.

Hata hivyo, baada ya kufunga bao hilo, Mayele aliendelea kuonyesha kiwango bora na kufunga bao la pili dakika ya 86 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Abdelrahman Magdi, na kuifanya mechi kumalizika Pyramid ikiibuka kidedea.

Nyota huyo amekuwa na muendelezo mzuri kwenye michuano hiyo kwani msimu wa 2022-2023 akiwa na Yanga, alimaliza kama mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufunga mabao saba, na msimu uliopita akaisaidia Pyramids kuwa mabingwa, akifunga mabao sita na kuibuka tena mfungaji bora.

Timu hizo zitarudiana jijini Cairo nchini Mjmisri Jumapili wiki hii huku Pyramids ikipewa nafasi kubwa ya kuvuka hatua hiyo kutokana na kile ilichokifanya ugenini.