Fiston Mayele ameanza pale alipoishia msimu uliopita katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuiongoza Pyramids FC kupata ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya APR ya Rwanda akifunga mabao yote hayo ya timu yake.
Msimu uliopita, mshambuliaji huyo wa timu ya Taifa ya DR Congo alifumania nyavu mara sita kwenye mashindano hayo na kuibuka Mfungaji Bora.
Katika mchezo wa leo Oktoba Mosi uliofanyika katika Uwanja wa Pele, Kigali Rwanda, Mayele alifunga mabao yake katika dakika ya 49 na dakika ya 86.
Mayele amefunga bao la kwanza la Pyramids FC akimalizia pasi ya Abdelrahman Magdi na bao la pili la nyota huyo wa zamani wa Yanga alipachika akimalizia pasi ya mwisho ya Magdi tena.
Ushindi huo wa mabao 2-0 ambao Pyramids FC imeupata ugenini leo, unaiweka katika nafasi nzuri timu hiyo ya Misri kutinga raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Pyramids FC inahitaji matokeo ya ushindi au sare ya aina yoyote katika mechi ya marudiano itakayochezwa Oktoba 5, 2025 huko Cairo, Misri ili isonge mbele.
Katika raundi ya pili ya mashindano hayo, mshindi wa jumla baina ya Pyramids FC na APR atakutana na Ethiopian Insurance ya Ethiopia ambayo katika raundi ya kwanza imeitoa Mlandege ya Zanzibar.
Ethiopian Insurance imeitoa Mlandege kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3 ambapo katika mchezo wa kwanza Ethiopia ilishinda mabao 2-0 na ziliporudiana Visiwani Zanzibar ikafungwa mabao 3-2.
Ikukbukwe wiki iliyopita, Mayele aliiongoza Pyramids FC kutwaa ubingwa wa Kombe la Mabara la Klabu baada ya kuichapa Al Ahli ya Saudi Arabia ambapo alifunga mabao yote matatu.