‘Msiogope kupima saratani ya matiti, tezi dume’

Dar es Salaam. Wananchi wametakiwa wasiogope kujitokeza kupima saratani ya matiti na tezi dume kwa kuwa, unapojua afya  yako, utapata ushauri na kuelewa hatua za kuchukua.

Kauli hiyo imetolea leo Jumatano Oktoba mosi, 2025 na Daktari wa Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani na Elimu kwa Umma kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Kandali Samwel, wakati akizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya Alaf jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa mpango wa siku mbili wa kuwaelimisha wafanyakazi kuhusu afya zao.

Uzinduzi huo ni mojawapo ya kipaumbele cha kampuni hiyo katika kujali afya na ustawi wa wafanyakazi.

“Watu wasiogope kujitokeza kupima matiti na tezi dume kwani unapojua hali yako na kupokea ushauri unaelewa hatua za kuchukua,” amesema Dk Samwel.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa kampuni hiyo, Hawa Bayumi amesema mpango huo ni sehemu ya dhamira ya Alaf ya ustawi wa wafanyakazi na uwajibikaji wa kijamii wa kampuni hiyo.

Amesema upimaji huo ni wa hiari na unazingatia upimaji wa saratani ya matiti, tezi dume, homa ya ini na chanjo.

“Mpango huu unalenga kuelimisha wafanyakazi juu ya umuhimu wa kupima afya ambao ni pamoja kugundua mapema na kuzuia athari zinazoweza kujitokeza ili kila mtu aweze kuishi maisha mazuri na yenye afya bora,” amesema.

Bayuni amesema kuwa, upimaji huo ni bure kwa wafanyakazi wote na kwamba watumishi wote watapata muda wa kutosha wa kuwasiliana na kupata ushauri wa wataalamu wa afya.

Pia, amebainisha kuwa, suala hilo litakuwa endelevu kuhakikisha wafanyakazi wanajenga utamaduni wa kupima afya zao ili waendelee kuwa na afya bora nje na ndani ya kazi.

“Wafanyakazi ni nguvu kazi muhimu kwa ajili ya kampuni yetu ndiyo maana uongozi umeona umuhimu wa kuandaa zoezi hili ili kila mfanyakazi aweze kujua hali yake ya kiafya ndani ya siku hizi mbili, kwani afya nzuri ndiyo itawawezesha kuendelea na kazi vizuri,”amesema.

Amesema wataendelea kuweka kipaumbele katika masuala ya afya na ustawi wa wafanyakazi wake kama sehemu ya juhudi zake zinazolenga kuifanya kampuni iwe na matokeo chanya kwenye mipango yake ya kazi.

Katika uzinduzi huo, madaktari kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Hospitali ya Shree Hindu Mandal walifanya semina kadhaa na wafanyakazi kabla ya upimaji na chanjo.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani wa Hospitali ya Shree Hindu Mandal, Sadiq Dawood, amehimiza kuhusu kupima na kuchoma chanjo ya homa ya ini maana ni moja ya magonjwa yanayoambukiza.