Kinshasa. Mahakama ya kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imemuhukumu adhabu ya kifo aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila, bila ya yeye kuwepo mahakamani.
Hukumu hiyo imetolewa jana Jumanne na Mahakama ya Kijeshi ya DRC kutokana na mashitaka yaliyofunguliwa dhidi ya Kabila kwenye mahakama hiyo Julai 25, 2025.
Kiongozi wa jopo la majaji sita waliosikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Kijeshi, Luteni Jenerali Joseph Mutombo Katalayi, amesema Kabila alikutwa na hatia ya makosa mbalimbali yakiwemo uhaini, uhalifu dhidi ya ubinadamu, mauaji, unyanyasaji wa kingono, mateso na uasi.
“Kwa kutumia Kifungu cha 7 cha Kanuni ya Adhabu ya Kijeshi, mahakama imeamua kutoa adhabu moja tu, ambayo ni kali zaidi, nayo ni adhabu ya kifo,” alisema Luteni Jenerali Katalayi wakati akisoma hukumu hiyo.
Pia, Kabila alituhumiwa kushirikiana na kikundi cha waasi cha M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, ambalo liliteka maeneo kadhaa ya mashariki mwa Congo mwanzoni mwa mwaka huu.
Hata hivyo, Rwanda ilikanusha kutoa msaada wa kijeshi kwa M23, lakini wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema jeshi la Rwanda lilikuwa na mchango mkubwa katika mashambulizi ya kundi hilo.
Kabila, ambaye aliongoza DRC kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, aliondoka DRC mwaka 2023, hivi karibuni alitembelea mji wa Goma ulioko mashariki mwa nchi hiyo, eneo linalodhibitiwa na waasi wa M23.
Hata hivyo, hakuna taarifa rasmi kuhusu mahali alipo Kabila baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo na mahakama ya kijeshi.
Rais huyo wa zamani hakuwahi kuhudhuria kesi hiyo na hakuwa na wakili yeyote wa kumwakilisha tangu kesi hiyo ilipofunguliwa mahakamani hapo Julai 25, 2025.
Awali, Kabila alilaani kesi dhidi yake, akiziita mahakama kuwa chombo cha ukandamizaji.
Hata hivyo, rufaa dhidi ya hukumu hiyo ya Mahakama ya Juu ya Kijeshi bado inawezekana kukatwa katika Mahakama ya Rufani ya Kikatiba (Court of Cassation), ingawa ni kwa misingi ya madai ya ukiukaji wa taratibu, si kwa kuchunguza hoja za msingi za kesi hiyo.
Waangalizi wanasema hukumu hiyo inalenga kuondoa uwezekano wa Kabila kuunganisha upinzani nchini humo, licha ya kutojulikana kwake mahali alipo.
Hata hivyo, wengi wamehoji iwapo uamuzi huo unaweza kuchochea machafuko zaidi.
Hukumu hiyo imetolewa baada ya Seneti ya DRC kupiga kura Mei kufuta kinga ya Kabila dhidi ya mashtaka, hatua ambayo rais huyo wa zamani aliilaani kama ya kidikteta.
Nchi hiyo pia iliondoa marufuku ya muda mrefu dhidi ya adhabu ya kifo mwaka jana, ingawa hakuna hukumu yoyote ya kifo iliyotekelezwa hadi sasa.
Mwendesha mashtaka wa kijeshi, Jenerali Lucien Rene Likulia, alitoa hoja mahakamani ya kutaka Kabila ahukumiwe kifo.
Likulia alimshutumu kiongozi huyo wa zamani kwa kupanga njama ya kumpindua Rais Felix Tshisekedi, huku mashtaka mengine dhidi yake ikiwemo mauaji, mateso na ubakaji yakihusishwa na kundi la M23.
Makubaliano ya amani kati ya serikali za Congo na Rwanda yalisainiwa Juni huko Washington nchini Marekani. Tamko la makubaliano ya kusitisha mapigano ya kudumu pia lilisainiwa na kundi la M23 nchini Qatar Julai mwaka huu.
Hata hivyo, ghasia bado zinaendelea na mashirika ya kiraia yamelalamikia ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya raia, ikiwemo mauaji holela, ubakaji wa halaiki na utekaji nyara.
Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa uliofanyika mapema Septemba ulibaini kuwa pande zote zinazohusika katika mgogoro huo huenda zimehusika na uhalifu wa kivita na dhidi ya ubinadamu.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.