Vijana 13 wa Kitanzania, wasomi, wameweza kutengeneza ndege na kuifanya Tanzania iwe nchi ya kwanza Afrika kufanya hivyo. Vijana wazalendo kwa nchi yao, wameandika ubavuni maandishi yanayosomeka waziwazi, “made in Tanzania”, yaani imetengenezwa Tanzania.
Mazimbu, Morogoro, ndiyo kwenye kiwanda cha ndege. Kila kitu kilianza na mawazo ya Mhandisi Paul Ihunya, kisha wenzake 12 wakajiunga naye.
Wote ni wasomi wa fani za uhandisi na anga. Kwa maana hiyo, ndani ya vijana 13, kuna wahandisi na marubani. Yupo pia Lilian Jackson, mdhibiti wa ubora wa ndege. Ni timu ya watu waliochaguana kufanikisha ndoto kubwa.
Vijana hao wameanzisha kampuni ya usafiri wa anga inayoitwa Airplanes Africa Limited (AAL), na ndege zinazozalishwa na AAL ni aina ya Skyleader 500 na 600. Ndege hizo zina uwezo wa kubeba abiria wawili, na zinaweza kusafiri angani kwa saa saba mfululizo, yaani dakika 420.
Kipimo hicho ni kuonesha kuwa Skyleader 500 na Skyleader 600, zinaweza kusafiri kwenda nchi yoyote Afrika bila kuwa na kituo cha kujaza mafuta.
Ndege hizo kwa sasa zina matumizi ya aina tano; shughuli za kilimo, kwa maana ya umwagiliaji, utalii, utafiti wa kisayansi, ulinzi na usalama.
Zinatumia mafuta ya petroli. Mdhibiti wa Ubora wa AAL, Lilian Jachon, anasema kuwa malighafi zote za utengenezaji wa Skyleaders, zilinunuliwa kutoka maeneo yaliyoidhinishwa kwa ajili ya vifaa vya kutengenezea ndege ulimwenguni. Hadi sasa AAL imeshazalisha ndege tisa, tano zikiwa tayari kazini, nne zipo kwenye hatua ya ukamilishwaji.
Ndoto ni kuzalisha ndege nyingi iwezekanavyo. Ihunya, ambaye ndiye mbeba maono, anatuma ujumbe kuwa vijana wa Kitanzania wasihofu, waweke mkazo kwenye ndoto zao, watafanikiwa.
Wewe unatafsiri vipi hatua ya vijana 13 wanaotengeneza ndege Tanzania? Kwa matumizi bora ya elimu waliyoipata na uthubutu wao ambao uliongozwa na ari kwamba wanaweza, si ndiyo?
Unawatafsiri vijana hao kama hazina ya taifa, ambao kama nchi wanapaswa kuenziwa na kutunzwa ili wawe na manufaa makubwa kwa Tanzania na Afrika.
Unawaona vijana hao kama mbegu ambayo imepandwa na kutoa matunda yatakayochagiza uthubutu mkubwa kwa Watanzania wengine, kuona kumbe inawezekana kuota na ndoto yoyote na ikafanikiwa.
Vijana hao siyo tu wamekuwa ingizo jipya la mfano wa kuigwa kwa kizazi kipya cha Watanzania, bali pia wao ni maambukizi ya kijamii kuhusu matumizi bora ya elimu, uthubutu, nidhamu ya maisha, vilevile ufanikishaji wa malengo.
Unawaacha watengeneza ndege, unamtazama Ally Masoud “Kipanya”, mwanahabari, ambaye ni mchora katuni gwiji, lakini ameweza kutengeneza magari kupitia kampuni yake ya KP Motors. Kipanya aliona ombwe la ubunifu na uthubutu Tanzania, akaingia kazini. Leo, Kipanya haishii kuwa mchora katuni mwenye lenzi kali, bali mbunifu wa magari ya umeme, vilevile mmiliki wa kiwanda cha magari ya umeme.
Ni Tanzania ambayo kuna vijana wanachagua kushinda mitandaoni kutukana, kupiga soga zisizo na rutuba kwenye maisha, kulalamika na kulaumu kila kitu.
Ni Tanzania hiyo hiyo kuna vijana wanatengeneza ndege na magari. Wanafanya yale ambayo kila mtu aliamini isingewezekana.
Hapa tafsiri haipaswi kuwa kupanga ni kuchagua, bali bidii inahitajika kukijenga kizazi kione kwamba, “inawezekana”, inatokana na ubongo binafsi, namna unavyochakata mambo. Matokeo yapo kwa wanaoyatafuta.
Vijana 13 wanaotengeneza ndege, Kipanya na wabunifu wengine ambao wamekuwa wakithubutu kila uchwao na kufanikisha ndoto zao, kwa pamoja wanatuma ujumbe ndani ya mipaka na popote ulimwenguni kuwa “Tanzania yote yanawezekana”. Muhimu ni mwota ndoto kutambua anataka nini, na achague mahali pa kusimama. Kuikimbiza ndoto, kuilaumu ndoto au kulalamikia mazingira kwamba yanakwamisha ndoto.
Nyakati ngumu za mapambano ya kudai haki ya mtu mweusi Marekani, shujaa wa wakati wote wa vita ya ubaguzi wa rangi, Dk Benjamin Elijah Mays, aliwaambia Wamarekani Weusi: “Whatever you do, strive to do it so well that no man living and no man dead and no man yet to be born could do it any better.”
Kiswahili: Chochote unachofanya, pambana kufanya kwa ubora wa juu kiasi kwamba asiwepo mtu aliye hai na aliyekufa na ambaye hajazaliwa ambaye angeweza kufanya zaidi.
Mays ambaye ni Rais wa Sita wa chuo cha Wamarekani Weusi cha Morehouse, kilichopo Atlanta, Georgia, alikuwa mwanaharakati hasa ambaye hakutaka mtu mweusi adeke, yeye aliamini kuwa dawa ya kumpandisha hadhi mtu mweusi ni bidii.
Naam, bidii ya kila unachofanya. Kwamba unapofanya chochote jiulize, je, hayupo mwingine anaweza kufanya zaidi kuliko wewe?
Wito na dhamira ya Mtanzania, vinapaswa kuongozwa na falsafa ya Mays. Kuhakikisha unafanya kazi kwa bidii kubwa na kwa ubora wa hali ya juu.
Kwa namna hiyo ndiyo itawezekana kuipeleka Tanzania mbele. Mays aliwaambia Wamarekani Weusi kuwa ukombozi wao ni bidii na ubora wa wanachokifanya kwa sababu wengi wao walikuwa wakilalamika, wakidhani kesho bora watapewa pasipo kuitafuta na kulazimisha kuipata.
Watanzania hasa vijana, wanatakiwa kuelewa kwamba uhuru na utulivu wa kufikiri, mtaji namba moja ni mazingira yenye amani na utulivu.
Taifa lenye mustakabali unaoeleweka, ndilo huzalisha vijana aina ya Ihunya, Kipanya na wengine. Tanzania ni njema kwa kila mwenye kutamani matokeo makubwa. Kila mtu anaruhusiwa kuota ndoto na mazingira ya kufanikisha yapo. Je, unachagua kufuata nyayo za Ihunya na Kipanya kwa kuanza kusaka matokeo yao, au wito wako ni kuwachukia wanaofanikiwa? Tanzania ni moja.