UCHAMBUZI WA SALIMU: Kumekucha, uchaguzi na mtihani wa amani

Kumekucha Tanzania. Baada ya kuhesabu miaka, miezi na sasa siku, taifa lipo katika hatua za mwisho kuelekea uchaguzi mkuu wa nane tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Katika safari hii, Zanzibar imetajwa mara nyingi kama eneo nyeti linalohitaji tahadhari kubwa ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na usalama.

Kwa zaidi ya miezi sita iliyopita, wito wa kulinda amani umekuwa ukitolewa kila kona ya visiwa hivi. Kauli hizo zimesikika kwenye majukwaa ya kisiasa, vyombo vya habari, nyumba za ibada, hafla za kijamii, sherehe za maulidi, harusi na hata kwenye mazishi. Kila mmoja amesisitiza haja ya kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani, huru na wa haki. Hata hivyo, pamoja na maneno yote ya kutia moyo, hofu bado imetanda miongoni mwa wananchi. Wengi wanaona uchaguzi Zanzibar umegeuka kuwa mtihani mkubwa, mara nyingine ukihusishwa na vitisho, watu kupigwa na wengine kuuawa.

Kwa baadhi ya familia, uchaguzi umekuwa kama msimu wa maafa unaosababisha wajane, mayatima na hata watu kuhama makazi yao ili kuanza maisha mapya kwingineko.

Viongozi wa Serikali na vyombo vya ulinzi wameendelea kutoa hakikisho kwamba hatua madhubuti zimechukuliwa ili mara hii Zanzibar iwe na uchaguzi wa amani.

Lakini wananchi wanakumbuka kuwa kauli kama hizo ziliwahi kusikika katika chaguzi zilizopita, huku matokeo yake yakiwa kinyume kabisa, vitisho, dhuluma na vifo vilitokea.

Ni wazi kuwa amani haiwezi kujengwa kwa maneno matupu. Inahitaji mazingira halisi yanayoruhusu haki, usawa na imani miongoni mwa pande zote. Hali ya sasa kuelekea uchaguzi unaotarajiwa haijatofautiana sana na ya miaka iliyopita. Malalamiko ya kunyimwa haki ya kupiga kura, mipangilio isiyo rafiki kwa uchaguzi huru na kura ya mapema, vimeendelea kuzua hofu na mashaka.

Kura ya mapema ndiyo imekuwa chanzo kikuu cha mgogoro. Wakati ilipoanzishwa, ililenga kurahisisha upigaji kura, lakini wapinzani wanasema imekuwa kichocheo cha vurugu na vifo. Tukio kubwa linalokumbukwa ni lile la kuuawa kwa watu 21 na wengine wengi kujeruhiwa baada ya kura ya mapema kuibua utata.

Mpaka sasa kura ya mapema bado ipo. Ingawa idadi ya watakaopiga kura siku hiyo haijulikani bayana, hofu ni kubwa kuhusu uhalali wake. Katiba ya Zanzibar haijafanyiwa marekebisho kuhalalisha mfumo huu, jambo linalowafanya wapinzani kudai kuwa ni kinyume cha katiba na kuiita siku ya kura ya wizi.

Kwa maoni yangu, hili lingetatuliwa mapema kupitia mazungumzo na makubaliano baina ya pande zote. Badala yake, watu wanakaribia kupiga kura wakiwa bado na sintofahamu kuhusu mustakabali wa kura ya mapema.

Hatari iko pale ambapo kura hiyo haitafanyika kwa uwazi na uadilifu, jambo linaloweza kuleta kutoelewana.

Ni lazima si tu itazamwe kwa tochi, bali hata kwa darubini ili kugundua dalili zote za vurugu mapema.

Jambo jingine linalozua hofu ni kuibuka tena kwa makundi ya vijana wanaofanya mazoezi kwenye viwanja na hata barabarani. Makundi haya yamekuwa yakipewa majina mbalimbali yenye kutisha kama wauaji, mazombi na janjaweed.

Katika chaguzi zilizopita, makundi kama haya yalihusishwa na vitisho, uporaji na hata mauaji. Cha kushangaza, licha ya uhalifu mkubwa uliofanyika miaka iliyopita, hakuna mtu hata mmoja aliyepelekwa mahakamani kwa mashtaka.

Hii ni fedheha kubwa kwa taifa linalojigamba kuwa na misingi ya utawala bora na kuheshimu sheria.

Kwa sasa, makundi hayo yameonekana tena, yakisababisha hofu na hata usumbufu kwa watumiaji wa barabara kutokana na misongamano.

Nyimbo wanazoimba vijana hawa, baadhi wakiwa wamefunika nyuso zao zinabeba ujumbe wa vitisho badala ya amani. Swali linalojitokeza ni kwa nini hali kama hii inaruhusiwa kujitokeza tena?

Kwa mtazamo wa jumla, hali bado ni shwari ukilinganisha na chaguzi zilizopita. Miaka iliyopita, wakati kama huu tayari wananchi walikuwa katika hofu kuu, wakisikia mara kwa mara taarifa za uvamizi wa nyumba, vipigo na hata mauaji.

Lakini uzoefu unatufundisha kuwa kutokuonekana kwa wingu hakumaanishi kutokuwapo kwa mvua. Ni lazima kila dalili ya vurugu ichukuliwe kwa uzito.

Mamlaka husika, hasa Jeshi la Polisi, lina wajibu mkubwa wa kuhakikisha sheria inasimamiwa kikamilifu. Yeyote anayeonyesha dalili za kutaka kuharibu amani ya nchi anapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria bila upendeleo.

Amani ni urithi wa kila Mzanzibari na kila Mtanzania. Wanaochezea amani kwa kisingizio cha uchaguzi, au kudhani kuwa visiwa hivi ni mali yao binafsi na wapo juu ya sheria, wanapaswa kuelekezwa wazi kwamba wanakosea. Wachezee mpira iwe kandanda, pete au netiboli, lakini wasichezee amani ya Zanzibar.