Utafiti waanika gharama za utapiamlo katika uchumi, wadau washauri

Dar es Salaam. Uchumi wa Tanzania unapotea kila mwaka kwa makadirio ya Sh3.47 trilioni, sawa na Dola za bilioni 1.3 Marekani ikiwa ni asilimia mbili ya Pato la Taifa (GDP) kutokana na athari za utapiamlo kwa watoto, ripoti mpya imebainisha.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti ulioangazia Gharama za Utapiamlo katika Pato la Taifa wa ‘Cost of Hunger in Africa’ (Coha) uliozinduliwa jana Sepetemba 30, 2025  jijini Dar es Salaam Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Hasara hizi zinatokana na ongezeko la gharama za huduma za afya, mzigo kwa mfumo wa elimu na kupungua kwa tija katika nguvu kazi.

Wakati ripoti ikibainisha hayo, Mkutano wa 12 wa Afya, Tanzania Health Summit ulioanza leo Jumatano, Oktoba mosi 2025, umejadili kwa kina umuhimu wa urutubishaji wa chakula ili kupunguza kiwango cha utapiamlo nchini wakiangazia maeneo makuu manne.


Mkutano huo umeeleza kuwa, ili Tanzania iondokane na utapiamlo, inatakiwa kutilia mkazo urutubishaji vyakula (food fortification), ukaguzi sokoni, uwepo wa maabara, kudhibiti mchanganyiko bandia wa lishe, uwepo viwanda na mashine za kusaga zenye uwezo wa kurutubisha vyakula.

Akizungumza wakati wa mdahalo maalumu uliohusu masuala ya lishe, ofisa mtendaji mkuu wa shirika lisilo la kiserikali linalohakikisha chakula kinachofikishwa sokoni kina virutubisho muhimu vya lishe la SANKU, Felix Brooks-Church amesema mkazo zaidi utolewe maeneo ya vijijini hasa maeneo yanayozalisha chakula kwa wingi.

“Mwanamke aliye kijijini yeye hawezi kupata chakula kilichoongezwa virutubishi kwa kuwa, hawezi kufika kwenye masoko kama ‘supermarkets’ hivyo lazima huduma za uongezaji virutubisho, hasa mashine zifike kila mahali,” amesema Felix.

Maoni ya wadau wengi zaidi, ilikuwa kusisitiza mikoa inayozalisha chakula kufungwa mashine na viwanda vya uchakataji mazao ikiwamo mahindi, ngano, chumvi na mafuta ya kula ili kuziwezesha jamii hizo kupata virutubisho muhimu vya lishe.

Akitoa ufafanuzi baada ya mdahalo huo, Ofisa Lishe kutoka Wizara ya Afya, Peter Kaja amesema tayari Tanzania iliazimia tangu Novemba 15, 2024 kupitia Gazeti la Serikali kwamba, lazima kila mzalishaji wa bidhaa hizo za vyakula kuhakikisha anafanya urutubishaji.

“Serikali ilifanya uzinduzi wa kanuni na Wizara ya Viwanda na Biashara ilitoa miezi sita kwa wazalishaji wa bidhaa hizi nne, kuhakikisha wana hizi mashine za kufanya urutubishaji wa vyakula. Ikifika Januari hawataruhusiwa kuuza bidhaa zisizorutubishwa.


“Kama unazalisha na kupaki lazima uwe umefanya ‘fortification’ lazima tuwe na maabara tumeshafanya uwekezaji wa mashine zote, Wizara ya Afya na Viwanda watahusika katika kupima vyakula madukani katika ngazi zote,” amesema Kaja.

Kwa mujibu wa muhtasari wa ripoti hiyo iliyotolewa jana na Shirika la Chakula Duniani (WFP), ingawa kwa kipindi cha miongo mitatu iliyopita, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza kiwango cha watoto wenye udumavu, kutoka asilimia 50 hadi 30, kiwango hicho bado kipo juu ya wastani wa kimataifa wa asilimia 23.

Mwaka 2022, takriban watoto milioni 2.8 walio na umri chini ya miaka mitano walikuwa wamedumaa na zaidi ya milioni 1.1 walikuwa na uzito pungufu wengi wao wakiwa na umri wa kati ya miezi 12 hadi 23.

Utafiti unaonesha kuwa, watoto waliodumaa wana uwezekano zaidi ya mara mbili wa kurudia darasa ikilinganishwa na wenzao waliolishwa vizuri.

“Utafiti wa Coha unathibitisha kile tunachoshuhudia kila siku watoto waliolishwa vizuri hujifunza kwa urahisi, hukua imara na hujenga mustakabali bora. Tunapongeza Serikali ya Tanzania kwa uongozi wao katika kufanikisha utafiti huu,” amesema Ronald Tran Ba Huy, Mkurugenzi mkazi na Mwakilishi wa WFP.

“Kupitia ushirikiano wetu, WFP inaendelea kuunga mkono juhudi za nchi katika kujenga mtaji wake wa rasilimali watu kupitia programu mbalimbali za lishe na mlo shuleni ambako huwasaidia watoto kubaki shuleni, kufanya vizuri na kufikia uwezo wao kamili.”

Tathmini hiyo inakadiria kuwa, Tanzania ingeweza kuokoa hadi Sh4.2 iwapo kiwango cha udumavu wa watoto kingepunguzwa hadi asilimia 15 ifikapo mwaka 2030.

Mwaka 2022 pekee, kurudiwa kwa madarasa kuliko sababishwa na utapiamlo kuliligharimu Taifa Sh125.2 bilioni jambo linaloonesha kuwa utapiamlo hauathiri afya pekee, bali pia elimu na ukuaji wa uchumi wa muda mrefu.

Uzinduzi wa utafiti wa Coha nchini Tanzania unaifanya kuwa nchi ya 26 barani Afrika kujiunga na juhudi za kikanda za kupambana na utapiamlo wa watoto kupitia sera na uwekezaji unaoongozwa na takwimu.

Tafiti za awali za Coha zilizofanyika katika nchi 25 za Afrika zimeonesha upotevu wa kila mwaka katika Pato la Taifa unaokaribia kati ya asilimia 1.9 hadi 16.5 kutokana na athari za muda mrefu za utapiamlo.

“Kueleza umuhimu wa kuzuia na kukabiliana na utapiamlo katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati kunaweza kuwa changamoto katika mijadala ya maendeleo.

“Tathmini ya Coha inaziba pengo hilo kwa kupima athari za utapiamlo kwa kutafsiri madhara yake katika afya, elimu, na tija ya kazi katika thamani ya kifedha,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Dk Germana Leyna.


Akizindua ripoti hiyo kwenye Mkutano Mkuu wa 11 wa wadau wa lishe, Majaliwa aliiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na taasisi za udhibiti ziimarishe ukaguzi na utekelezaji wa sheria ili kuhakikisha uongezaji wa virutubishi na upatikanaji wa vyakula salama.