WANAFUNZI SUA WANG’ARA TUZO ZA UMAHIRI WA HABARI ZA SAYANSI TANZANIA

 

Na: Calvin Gwabara – Dar es
salaam

Wanafunzi watatu wa Shahada ya
Uzamili ya Taarifa na Menejimenti ya Maarifa (MIKM) kutoka Idara ya Infomatiki
na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (DIIT) ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) wameng’ara kwenye tuzo kubwa zinazotambua mchango wa wanahabari
kwenye kuandika taarifa za sayansi na bioteknolojia Afrika kwa upande wa Tanzania
(OMAs).

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Taifa ya Sayansi na
Teknolojia (COSTECH) Prof. John Kandolo akikabidhi tuzo kwa washindi wa jumla wa tuzo hizo Bi Rebecca Kachembeho na Bi. Jackline Martine. 


Wanafunzi hao ni Rebecca Kachembeho
na Jackline Martine ambao wameibukwa kwa pamoja washindi wa jumla wa tuzo hizo
(Overall winner) kwa kuandika taarifa nzuri iliyohusu nafasi ya bioteknolojia
kwenye kutatua changamoto za ugonjwa mnyauko wa migomba Mkoani Kagera,
Changamoto za wadudu wa Pamba wanaokwamisha tija pamoja na makala kuhusu Bungua
wa Mahindi na Viwavijeshi vamizi wanavyorudisha maendeleo ya wakulima nchini.

Mwandishi mwingine ambaye pia ni
Mwanafunzi aliyeng’ara kwenye tuzo hizo ni Martinius Sospeter ambaye ameshika
nafasi ya pili kwa upande wa magazeti kwa kuandika Makala nzuri iliyoonesha
mchango wa Sayansi hasa Bioteknolojia katika kutatua changamoto za upungufu wa
chakula zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, wadudu na magonjwa na
nafasi ya Bioteknolojia katika kuboresha afya nchini Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya washindi
na washindi wote kwenye hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es salaam Mshindi wa
jumla Bi. Rebecca Kachembeho amekishukuru Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa
kufundisha kozi ya namna ya kuandika habari za sayansi na kutafsiri matokeo ya
kisayansi kwa lugha rahahisi kwa jamii ili waweze kuelewa na kutumia matunda ya
sayansi.

“Tunakishukuru Chuo Chetu cha
Sokoine cha Kilimo kwa kuona umuhimu wa kutufundisha kozi hii na kutupatia
mbinu nyingi za namna ya kuwasilisha sayansi kwa jamii, hakika imetupatia mbinu
nyingi na maarifa ya kutuwezesha sasa kuitumiakia jamii yetu vizuri kwa
kuwafikishia matokeo ya tafiti kwa lugha rahisi ili wayatumie kutatua changamoto
zinazowakabili na kuongeza ustawi wao katika nyanja mbalimbali.” Alisema Bi. Kachembeho.

Awali akieleza kuhusu tuzo hizo
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amon Nungu
amesema tume imekuwa ikifanya kazi na Waandishi wa habari kwa miaka mingi hasa
kwa kuwajengea uwezo kuhusu Uandishi wa habari za sayansi na nafasi yao katika
kusaidia kufikisha matokeo ya tafiti kwa jamii.

“ COSTECH kupitia Jukwaa la
bioteknolojia za Kilimo Afrika (OFAB Africa) tumekuwa tukifanya kazi kubwa sana
katika kuwajengea uwezo Wanahabari nchini kwa zaidi ya miaka 15 ya jukwaa hili
lakini pia katika kuongeza ari ya kuhamasisha uandishi huo tumekuwa tukitoa
tuzo maalumu kutambua mchango wao kila mwaka hapa Tanzania na baadae washindi huenda
kushindanishwa Afrika na wamekuwa wakifanya vizuri na wengine kunyakua Tuzo
hizo barani afrika kama tulivyosikia Calvin Edward Gwabara kutoka SUAMEDIA
aliyeshinda Tuzo ya Afrika mwaka 2018” alifafanua Dkt. Nungu.

Aidha amewahakikishia Wanahabari
ushirikiano wa kina katika kuwezesha utekelezaji wa majukumu yao lakini pia
kuendelea kuwajengea uwezo zaidi katika kuandika habari za sayansi nchini ili
sayansi iweze kutoa mchango unaostahili kwenye maendeleo ya jamii na Taifa kwa
ujumla.

Nae Mgeni rasmi katika Tuzo hizo
ambaye ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH) Prof. John Kandolo amewapongeza washindi hao wote kwa kuandika habari
na makala nzuri ambazo zimeweza kushawishi majaji kuzipatia ushindi hasa baada
ya kutimiza vigezo vingi vilivyowekwa kuchuja ubora na kuona mchango wake
katika maisha ya watu.

“Niwapongeze wote mlioshinda na
wale wote zaidi ya 50 mlioshiriki kutuma kazi zenu kwenye tuzo hizi, ninaamini
kama hukupata leo basi umefungua mlango wa kujipanga vizuri ili uweze kushinda
kwenye tuzi zijazo, lakini niwapongeze sana kwa kazi nzuri mnayoifanya ya
kuhabarisha jamii kwenye kutumia matokeo ya sayansi kutatua changamoto zao na
kuongeza tija kwao na maendeleo ya Taifa leo” alieleza Prof. Kandalo.

Aidha amesema kuwa maendeleo ya
taifa lolote duniani yanategemea matumizi ya Sayansi na teknolojia na ubunifu
lakini yatatokea endapo matokeo hayo ya tafiti yatafahamika kwa jamii na
kuyatumia kikamilifu kama ambavyo mataifa mengi yaliyoendelea duniani
yanavyofanya.

Awali tuzo zilitanguliwa na
mafunzo kwa waandishi wa habari ambapo Watafiti nguli wa Bioteknolojia na
wabobevu kwenye masuala ya Uandishi wa habari za Sayansi nchni walifundisha
mada mbalimbali na kutoa nafasi ya mjadala mpana wa fursa zilizopo, changamoto
na hatimae kuweka mikakati ya pamoja.

MATUKIO WAKATI WA UTOAJI WA TUZO HIZO.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amon Nungu  akieleza kuhusu tuzo hizo na mchango wa COSTECH kwa wanahabari na sayansi.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Taifa ya Sayansi na
Teknolojia (COSTECH) Prof. John Kandolo akizungumza kabla ya kutoa tuzo hizo. 

Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wakifuatilia mafunzo hayo kabla ya utoaji wa tuzo kuanza.

Bwana Calvin Gwabara akipokea cheti cha ushiriki kutambua mchango wake kwenye tuzo hizo na uandishi wa habari za sayansi.

Mohamed Gojo mmoja wa wanafunzi wa SUA aliyeshiriki kwenye tuzo hizo akipokea cheti chake cha ushiriki.

Mwanafunzi Martinius Sospeter aliyeshika nafasi ya pili kwa upande wa magazeti akipokea cheti chake kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamsheni ya COSTECH.

Washindi wa tuzo hizo kutoka SUA  Bi. Rebecca Kachembeho (wa kwanza kushoto)  Jackline Martine (katikati) na Martinius Sospter (Kulia) wakiwa kwenye piocha ya pamoja mara baada ya kupokea tuzo zao.

Mshindi wa Jumla Bi. Rebecca Kachembeho akiwa ameshika tuzo yake mara bada ya kukabishiwa

Mshindi mwenza Bi. Jacline Martine akiwa kwenye picha na tuzo yake mara baada ya kukabidhiwa kwenye hafla hiyo.