JANA Jumanne Septemba 30, 2025, Yanga ilibanwa mbavu na Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya n kuifanya timu hiyo kudondosha pointi mbili za kwanza kwa msimu huu.
Baada ya mechi hiyo, kelele zimeendelea kuwa nyingi kwa kocha mkuu wa Yanga, Romain Folz kuwa hawamuelewi aina ya ufundishaji, hujku wakidai anatumia mbinu ngumu licha ya timu kutopoteza mechi yoyote msimu huu kati ya tano za kimashindano ilizocheza. Pia timu hiyo haijaruhusu nyavu zao kuguswa na yenyewe kufunga mabao tisa.
Awali kelele hizo zilikuwa mitandaoni na vijiwe vya kahawa, lakini jana mashabiki waliokuwepo Uwanja wa Sokoine walipaza sauti zao wakisema: “Hatumtaki! Hatumtaki! Hatumtaki! Aondoke.”
Sasa basi kutokana na kelele hizo kuwa nyingi, kocha mkongwe na mkufunzi wa makocha wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Sunday Kayuni, amesema akiitazama Yanga huko nyuma ilikuwa na falsafa ambayo wangekuwepo wachezaji aina ya Khalid Aucho aliyejiunga na Singida Black Stars na Stephane Aziz KI anayeichezea Wydad, hali isingekuwa hivi ilivyo sasa.

“Mfano Barcelona ina falsafa yake katika makaratasi, lazima kocha anayekwenda kuifundisha awe na vinasaba vya timu hiyo, ama awe aliwahi kuichezea timu hiyo iwe timu ya vijana ama kubwa na akaenda kusomea ukocha, hivyo huwezi kuona wanachukua makocha kiholela,” amesema Kayuni aliyewahi kuandika rekodi ya kuipa AFC Leopard ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya mwaka 1998.
“Kuna mawili, huenda Folz anaweza akaendana na falsafa ya timu, lakini wachezaji alionao hawaendani nayo, hivyo kwa sasa anatengeneza namna ambavyo timu lazima ipate matokeo huku mambo mengine ya kiufundi yakiendelea.
“Nimezitazama mechi za Yanga kila inapocheza inakuwa na mabadiliko ya wachezaji, hilo linatokana na kocha kukosa muda mrefu wa kukaa nao, kwa sababu lazima umjue kila mmoja ubora na udhaifu wake.

“Pia inawezekana wachezaji wapya siyo wa falsafa ya Yanga, hivyo kocha anatumia falsafa yake ndiyo maana mashabiki wanakuwa hawaelewi, nimemsikia akihojiwa akiwa Mbeya, naona kuna kitu anakitengeza kinachohitaji muda ambacho kitakuwa na faida mbele.”
Jambo lingine la msingi alilolisisitiza Kayuni ni klabu za Simba na Yanga zihakikishe zinakuwa na mabenchi ya ufundi imara, ili kocha akiondoka inakuwa ni rahisi kumpendekeza anayeendana na falsafa zao.
“Benchi la ufundi ni pana, kocha akiondoka wapo wale ambao tayari wanakuwa wameshafanya skauti ya kuona kocha fulani anaendana na falsafa yao, pia lazima wasajili wachezaji wanaoendana na falsafa zao, hilo linawasaidia kufanya vizuri na timu kuwa katika muendelezo wa kiwango kizuri,” amesema Kayuni.

Kayuni ni kocha wa zamani wa Taifa Stars, Yanga, AFC Leopards ya Kenya, Kagera Stars na Mtibwa Sugar ambaye pia amewahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakati wa utawala wa Rais Leodgar Tenga.
Mwaka 2023, alipata shahada ya juu ya ukocha PRO-LICENSE kutoka Shirikisho la Soka Amerika Kusini (CONMEBOL).
Leseni hiyo ameipata baada ya kusomea masomo ya ukocha kupitia Chama cha Soka Argentina (Argentina Football Association) kwa miaka 4.
Wakati Kayuni akiyasema hayo, kocha mkongwe mwenye rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyefunga hat trick katika Dabi ya Kariakoo akifanya hivyo mwaka 1977, Abdallah Kibadeni amesema: “Sina hakika kama kocha amekaa na timu muda mrefu katika maandalizi ili kuwajua vyema wachezaji, angalau zichezwe zaidi ya mechi tano ndipo mfumo wake utakapoonekana, ila kwa sasa ngumu kumuelezea, kwani mifumo inakuja baada ya kuwajua vizuri wachezaji.”

Katika mechi tano alizoongoza Folz, kikosi chake kimekuwa na mabadiliko makubwa kila siku huku wachezaji ambao hawajacheza hata dakika moja ni makipa Aboutwalib Mshery, Abubakar Khomeny, mabeki Abubakar Nizar ‘Ninju’, Frank Assinki na viungo Farid Mussa, Abdulnasir Mohammed ‘Casemiro’, Salum Abubakar ‘Sure boy’ na Denis Nkane. Mchezaji pekee aliyecheza dakika zote ni kipa Djigui Diarra.
Hata hivyo, Yanga imekuwa na wakati mgumu inapokwenda kucheza Uwanja wa Sokoine dhidi ya Mbeya City.
Rekodi zinaonyesha katika mechi tano za mwisho uwanjani hapo, timu hizo hakuna iliyoondoka na ushindi. Mara ya mwisho Yanga kushinda Sokoine dhidi ya Mbeya City ilikuwa Desemba 29, 2018 iliposhinda 2-1. Mabao yote yalifungwa na Heritier Makambo ambaye sasa yupo Namungo. Lile la Mbeya City mfungaji alikuwa Idd Nado anayecheza Azam kwa sasa.
Akizungumza baada ya mechi ya jana dhidi ya Mbeya City, Folz amekubali kukutana na ugumu akieleza kuwa ni sehemu ya matokeo akiahidi anaenda kusahihisha makosa yaliyojitokeza.
Amesema kwa kuwa ligi inasimama, anaenda kuboresha maeneo yote kuhakikisha timu inafanya vizuri haswa mechi za kimataifa zinazoikabili Yanga akiwatuliza mashabiki akiwaambia wawe wavumilivu.
“Hatukutarajia kupata matokeo haya ila tunakubali yapo makosa ambayo yalionekana upande wa ushambuliaji kushindwa kutumia nafasi tulizopata, tutatumia mapumziko haya kusahihisha,” amesema Folz.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema wamesikia kelele za mashabiki, lakini uongozi unaendelea kufanya tathimini na muda ukifika utaamua iwapo itahitajika la kufanya.
Amewaomba mashabiki kuwa watulivu akieleza timu yao ni bora na Uwanja wa Sokoine umeendelea kuwa mgumu kwao kupata matokeo mazuri.
“Uongozi unaendelea na tathimini kwa hiki kilichosikika kwa mashabiki, tukubali Sokoine kwa historia umeendelea kuwa mgumu kwetu na mambo mengine yatafanyiwa kazi,” amesema Kamwe.
Katika mechi 11 baina ya timu hiyo uwanjani hapo tangu mwaka 2013, Yanga imeshinda mara tatu tu, huku ikipoteza moja na zilizosalia ni sare.
Baada ya mechi ya jana kumalizika, Yanga iliweka matokeo kwenye akaunti yake ya Instagram ambapo chapisho hilo limepata wachangiaji zaidi ya 8,000.
Katika wachangiaji hao, wapo wanaomtetea kocha na wengine wakiendelea kuponda kiwango cha timu kinavyocheza. Haya hapa maoni yao.
Akili500 ameandika: “Wana yanga mnalalamika nini? Mbeya miaka yote inakuaga ngumu kwetu.”
Sophy_canavaro23: “Kocha tumejitahid kumlemba kwenye mitandao ila harembeki😢.”
Sportsextra_tz: “KOCHA akifika Nyerere day, basi Hadi X-MASS mnakula nae.! -🗣️ (Mzee Saidi Simba🔴).”
Djferuuh: “SINA SHIDA NA KOCHA HAIKUWA BAHATI PLUS UWANJA MBOVU ILA TEAM YANGU IMEUPIGA MWINGI INSHAALLAH YANGA BINGWA 🔥🔥🔥.”
Stevensiggo: “Fukuza kocha.”
_.dremo: “Usajili Tuliopigwa msimu huu, 1. Balla Conte, 2. Ecua, 3. Edmund – Very medium player, 4. Kocha😂😂😂😂.”
Yangawhatsapp_makaomakuu: “🔥🔥🔥mechi ilikuwa nzuri sana pande zote mbili”