Unguja. Tatizo la zima, washa na umeme mdogo Zanzibar sasa limepata mwarobaini baada ya kuzinduliwa mradi wa uimarishaji wa upotevu wa umeme katika miundombinu ambao unatajwa kudhibiti changamoto hiyo.
Zanzibar inapokea umeme kupitia gridi ya Taifa kutoka Tanzania bara kwa msongo wa kilovoti 132 (Unguja) na kilovoti 33 (Pemba), hata hivyo zilikuwa hazipokewi kwa kiwango kinachotolewa na kusababisha upotevu wa umeme kufika mahali husika mdogo, hatua iliyoibua changamoto kwa wananchi.
Kutokana na hali hiyo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) waliingia mkataba na Kampuni ya Novavis International kwa gharama ya Dola za Marekani 8.4 milioni kuweka miundombinu itakayoweza kudhibiti upotevu huo wa umeme.
Akizungumza leo Oktoba mosi, 2025 wakati wa kuzindua mradi huo, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema hiyo ni ishara njema ya Serikali kuhakikisha inaboresha miundombinu yake ya umeme kukuza uchumi wa nchi na jamii kwa ujumla.
“Mifumo yetu ya umeme ilikuwa inakabiliwa na changamoto kubwa, ilikuwa imechakaa na kuzidiwa na idadi kubwa ya watu, kwa hiyo tulichukua jitihada za makusudi kuhakikisha hali hiyo inabadilika, hii ni ishara njema kwa Serikali kuboresha miundombinu yake,” amesema Dk Mwinyi.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akikata utepe kuashiria uzinduzi mfumo wa uimarishaji umeme Zanzibar
Dk Mwinyi amesema kutokana na hali hiyo imepunguza gharama za uendeshaji ambazo walikuwa wakikumbana nazo wawekezaji hususani wa hoteli na kuokoa shughuli za kiuchumi za wananchi mmojammoja, kwani zilikuwa zikisimama kutokana na umeme mdogo na maeneo mengine kukosa kabisa,” amesema Dk Mwinyi.
Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha umeme unapatikana katika maeneo yote ya Zanzibar mjini na vijijini.
Ametaja baadhi ya hatua zinazochukuliwa mbali na mradi huo, lakini akataja miradi mingine inayotekelezwa chini ya Wizara ya Maji, Nishati na Madini ikiwemo miradi ya umeme jua na umeme wa upepo.
Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, hatua hizo zinazochukuliwa, wananchi wajiandae kwani katika siku chache zijazo wataunganishiwa umeme kwa Sh100,000 kutoka Sh200,000 ya sasa.
“Muda mfupi ujao kuunganisha umeme itakuwa Sh100,000, itakumbukwa wakati tunaingia madarakani ilikuwa kuunganisha umeme ni zaidi ya Sh400,000, tumeshusha hadi Sh200,000 na sasa tunakwenda kuushusha zaidi, hii ndio habari,” amesema huku wananchi na waliohudhuria katika hafla hiyo wakishangilia.
Amesema ndani ya miaka michache changamoto ya umeme katika visiwa vya Zanzibar itakuwa historia.
Ametumia fursa hiyo kuitaka Wizara ya Nishati na Zeco kuutunza mradi huo na kubuni miradi mingine mipya ili kuwasaidia wananchi kuondokana na changamoto hizo.
Awali akitoa taarifa za kitaalamu Meneja Mkuu wa Zeco, Haji Mohamed Haji amesema katika mradi huo wameweka vifaa maalumu vya kudhibiti umeme.
Amesema kabla ya kufunga vifaa hivyo kiwango cha umeme kilikuwa kinashuka hadi kufikia kilovoti 114 na ndio maana kulikuwa na katikakatika nyingi na maeneo mengine kukosa nishati hiyo.
“Kutokana na mradi huu tumeokoa fedha nyingi tulizokuwa tunazitumia katika matengenezo maana kila wakati ilitulazimu kufanya matengenezo, lakini kwa sasa hiyo hali imebadilika,” amesema Haji bila kutaja kiwango
Amesema kulikuwa na malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi kutokana na changamoto hiyo, hatua ambayo pia ilisababisha hasara kwa wananchi hao kushindwa kuendesha biashara zao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Novavis International, Eric Kasarika amesema wametekeleza mradi huo kwa kutumia vifaa na teknolojia ya kisasa ambavyo vimesaidia kusawazisha, kuimarisha utulivu wa umeme kwa kupanda na kushuka na kuongeza nguvu za umeme mdogo.
Amesema vifaa vilivyotumika kufanikisha mradi huo vimetoka Marekani, China, India, Australia na Afrika Kusini.
Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Joseph Kilangi amesema mradi huo ulitiwa saini Julai, 2023 baada ya kuona hali ya umeme inakuwa mbaya na umekamilika kwa wakati.
Amesema “Hatuwezi kubaki na kiwango hiki cha umeme wakati wawekezaji wanaongezeka kwa hiyo mipango mingi inakuja kuhakikisha tunakuwa na utoshelevu Zanzibar, tuna sera yetu ya uchumi wa buluu lakini bila umeme hatuwezi kuifanikisha.”
Baadhi ya wananchi wamepongeza hatua hiyo wakidai ilikuwa kero kubwa kiasi cha kufanya biashara zife kutokana a changamoto hiyo.

“Kwa sasa kuna unafuu mkubwa, kwa sababu hakuna biashara ilikuwa inafanyika tena maana kukatika umeme ilikuwa kawaida,” amesema Omar Said mkazi wa Mtoni.